Elimu bora inahitaji walimu bora

drclark

Member
Feb 10, 2016
57
95
Katika kukidhi haja ya kuwa na walimu wa kutosha, serikali za nchi nyingi hususan barani Afrika, zimekuwa zikichukua hatua mbalimbali kuhakikisha shule zina idadi ya walimu wa kutosha.

Hata hivyo, ili maarifa tunayokusudia kuwapa wanafunzi yawe bora yatakayowawezesha kukabiliana na mazingira ya kiuchumi, kijamii na hata kisiasa, tunapaswa kuwa na walimu bora na walioiva vyema na si bora walimu.

Kwa bahati mbaya, hapa nchini mwalimu anachukuliwa kama mtu duni, ni mtu aliyefanya vibaya katika masomo yake na hivyo kukosa namna nyingine ya maisha au kujiendeleza katika nyanja nyingine.

Hali hii imetokana na mfumo mzima uliokuwa unatumika kuwapata vijana wanaojiunga na vyuo vya ualimu hasa Daraja la Tatu A kwa ajili ya kufundisha shule za msingi. Ilizoeleka kuwa waliokuwa wakifeli kwa kupata daraja la nne walipangwa kwenye vyuo vya ualimu na kuandaliwa kwa muda mfupi kuwa walimu.

Tunapaswa kujiuliza; je, ni halali kuwaamini watu waliofeli masomo yao kuwa walimu tena kwa kiwango hiki cha elimu msingi?

Kwangu jibu ni la moja kwa moja, hatupaswi kuwaamini watu hawa kwa ajili ya kuwapa vijana wetu maarifa.

Serikali yetu inapaswa kuandaa mfumo utakaohakikisha wanafunzi wanaofanya vizuri katika masomo yao ndiyo wanaopewa nafasi ya kusomea taaluma ya ualimu ili hatimaye wawe chachu ya elimu bora.

Sambamba na hilo, ili taaluma ya ualimu iheshimike, mwalimu anapaswa kuwa na taswira ambayo inaheshimika katika jamii. Jamii ibadili mtazamo juu ya ualimu na mwalimu. Serikali inapaswa kutizama upya masilahi ya mwalimu katika nyanja zote.

Kwa mfano, kama walimu watalipwa na kutazamwa kama ilivyo madaktari, ni dhahiri kuwa hata hao wanaofaulu na kuchaguliwa kwenda ualimu, hawatokataa wakijua wanakwenda mahala sahihi.

Katika utekelezaji wa mpango wa elimu bure, kama ilivyo katika Waraka wa Serikali Namba Tatu wa mwaka 2016, hakuna sehemu ambayo mwalimu ametajwa kwa maana ya kuboreshewa mazingira yake ya kufanyia kazi pamoja na masilahi yake kwa jumla.

Mwalimu ameongezewa idadi ya wanafunzi huku ajira mpya zikiwa zimesitishwa kwa muda usiojulikana hivyo kumuongezea mzigo wa kazi bila kuboresha hali yake kimaisha.

Ukipitia vyombo vya habari, suala la kero za walimu limekuwa wimbo wa kila siku na hatua hazichukuliwi kulingana na uzito wake. Hii ni kutokana na ukweli kwamba madhara yake hayaonekani hapo kwa hapo ila ni suala la muda tu.

Juhudi za Serikali katika kuhakikisha wananchi wake wanapata elimu bora na yenye ushindani lazima ziendane na uboreshaji wa taaluma ya ualimu kwa ujumla wake. Watu wanaopewa dhamana ya kutoa elimu wawe na uwezo kitaaluma katika taaluma husika.

Ikiwezekana walimu wafanyiwe usaili kabla ya kuingizwa katika ajira ili kuwapima kama kweli wana uwezo wa kutoa elimu.

Aidha, mafunzo kazini yawe lazima na siyo suala la hiari, Serikali kupitia wizara husika inapaswa kuwapa walimu mafunzo wakiwa kazini ili kuwajengea uwezo utakaowasaidia kukabiliana na mabadiliko mbalimbali yanayotokea duniani na katika sekta nzima ya elimu

Nitoe rai kwa wanasiasa, watunga sera na wasimamizi wa sekta ya elimu kwa ujumla wake, walipe kipaumbele suala la elimu kwa upana wake na kuacha kasumba ya kila mara kutaja tu vyumba vya madarasa kama mahitaji yao; lazima wazungumze suala la walimu bora walioiva kitaaluma na masilahi bora ya walimu.


Chanzo: Mwananchi
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom