Dk. Slaa: Nitafumua mikataba ya madini
Mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibroad Slaa, amesema ikiwa atashinda kiti hicho, serikali yake itafumua mikataba ya madini na kufuta misamaha ya kodi katika sekta hiyo.
Dk. Slaa alisema msamaha wa kodi katika kampuni za madini, unapoteza Sh bilioni 700, fedha alizosema serikali yake itazielekeza kwenye elimu. Akihutubia mkutano wa hadhara katika viwanja vya Kwideko mjini Ngudu wilayani Kwimba jana, Dk. Slaa alisema inasikitisha kuona wageni wanafaidika na rasilimali za taifa huku Watanzania wakibaki masikini.
Alisema takwimu zinaonyesha kwamba madini yanaendelea kwisha lakini hayajawanufaisha Watanzania.
"Misamaha ya kodi ya mafuta kwenye makampuni ya madini inapoteza zaidi ya Sh. bilioni 700 kwa mwaka, kama zisingesamehewa sidhani kama leo tungechangishwa kujenga shule," alisema.
Aliongeza: "Madini hayaozi, hata Baba wa Taifa, hayati Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema."
Pia Dk. Slaa alisema akichaguliwa mishahara ya ‘vigogo' serikalini na wabunge itapunguzwa kwa asilimia 20. Alifafanua kuwa taarifa ya serikali iliyotolewa Julai mwaka huu bungeni, inaonyesha kuwa wilaya ya Kwimba ina jumla ya shule za msingi 150 na walimu 109, idadi isiyoendana na hali halisi.
Aliongeza kuwa takwimu hizo ambazo zilitolewa na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, zinaonyesha wilaya hiyo ina shule za sekondari 35 na walimu 41. "Hizi sio takwimu za Dk. Slaa ni za serikali, sasa ujiulize haya ndiyo mafanikio ya CCM, haya ni sawa na majosho ya ng'ombe unampeleka hapo suala la kupe kufa halikuhusu, ni aibu miaka 50 baada ya uhuru adui ujinga bado anatutesa," alisema.
Dk. Slaa ambaye alilakiwa na umati mkubwa wa wananchi, alisema wakati Mpango wa Maendeleo ya Shule za Sekondari (MMES) ulipoanza, Bunge liliidhinisha fedha za kusomesha walimu 15,000 na mwaka uliofuata zilitengwa kwa ajili ya walimu 10,000 ambao hata hivyo hawaonekani.
"Takwimu hizi zinaonyesha pia kuwa mwaka jana watoto waliomaliza darasa saba zaidi ya nusu hawakupata nafasi ya kujiunga sekondari, hawa tumewaharibia maisha yao...mnaweza kujiuliza taifa linakwenda wapi," alihoji. Alisema njia pekee ya kulikomboa taifa ni kurekebisha mfumo wa elimu.
Dk. Slaa alisema shule ni lazima ziwe na miundombinu muhimu pamoja na vitabu na walimu.