Katika miaka ya hivi karibuni ushirikiano kati ya China na nchi mbalimbali za Afrika umezidi kuwa wa kina, maeneo ya ushirikiano yamepanuliwa kutoka siasa kama ilivyokuwa kwenye miaka ya 70, na kugusa karibu sekta zote kwa sasa, hali ambayo imekuwa na msukumo wa maendeleo ya nchi za Afrika.
Mtaalam wa maswala ya historia wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam Dr. Andrea Kifyasi ni mmoja kati ya wasomi wanaofuatilia mambo ya ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika, na hasa mchango wa China katika kuhimiza maendeleo ya Afrika. Dr. Kiyasi anataka programu mbalimbali zilioanzishwa na China katika kuhimiza ushirikiano kati yake na nchi za Afrika, lakini pia anaona kuwa kiongozi wa China Bw. Xi Jinping yeye mwenyewe ametoia msukumo mkubwa katika kuhimiza ushirikiano kati ya China na nchi za Afrika. Dr. Kifyasi anasema.
“Ni kiongozi ambaye haangalii leo tu, anaangalia mbali. Tukichukulia mfano wa pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia moja”, tunaweza kuona jinsi analivyolisimamia na kulihimiza bila kuchoka, kwa sababu anataka kuhakikisha kuwa malengo yaliyopangwa ya pendekezo hilo yanatimizwa. Programu nyingi za pendekezo hilo zimekuwa zikiendelea katika nchi mbalimbali duniani, barani Afrika na nje ya Afrika, zinaendelea kutekelezwa msukumo wake, na uendelevu wake.”
Kuhimiza programu za maendeleo ni jambo moja, lakini manufaa yake ni jambo lingine. Kumekuwa na maswali na wakati mwingine ukosoaji kutoka kwa baadhi ya nchi za magharibi kuhusu pendekezo la “Ukanda moja, njia moja”. Baadhi ya watu hata wamekuwa wakilipaka matope pendekezo hilo walilitaja kuwa litaleta mzigo mkubwa wa madeni kwa nchi za Afrika zinazotumia fedha za mikopo kugharamia ujenzi wa miradi hiyo. Dr, Kifyasi ana maoni tofauti na wakosoaji hao akisema,
“Pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia moja” limekuwa na manufaa makubwa kwa nchi za Afrika. Ni bahati mbaya tu kuwa mpango wa awali wa kuziunganisha nchi za Afrika zisizokuwa na bandari, kupitia ujenzi wa bandari ya Bagamoyo na reli ya kisasa ulikwamishwa kwa sababu za kisiasa, lakini kwenye mkutano wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) uliopita walikubaliana kuiboresha reli ya TAZARA. Lakini pia kwenye baadhi ya nchi nyingine za Asia, kama vile Laos tayari zinanufaika na utekelezaji wa pendekezo hilo.”
Lakini mbali na manufaa yanayoonekana kwa macho kama miradi ya reli zilizojengwa, au miradi mingine inayotarajiwa kutekelezwa chini ya pendekezo la “Ukanda Mmoja, Njia moja” Dr. Kifyasi anaona kuwa China imeleta funzo adimu kwa nchi za Afrika na nchi nyingine za dunia ya tatu, kuwa kujiletea maendeleo ni jambo linalowezekana. Amesema kutokana na juhudi zake China sasa imekuwa ni nchi ambayo hata nchi za Kaskazini zinaitazama tofauti na zamani. Dr. Kifyasi anasema,
“China imekuwa ni nchi ya mfano wa kuigwa kati ya nchi za kusini (Global South), hasa kutokana na maendeleo yake ya kiuchumi na kiteknolojia, kiasi kwamba inaweza hata kuitetemesha Marekani. China sasa imefika kwenye hatua nzuri, na sasa imekuwa ni funzo kwa nchi za Afrika na nchi nyingine zinazoendelea. Ndio maana hata kwenye masuala makubwa yanayoisumbua dunia kwa sasa, China inaweza kuwa mstari wa mbele.”