GE2025 Doyo: Tutajenga SGR inayounganisha Kagera na nchi jirani Uganda na Rwanda kuchochea Biashara

GE2025 Doyo: Tutajenga SGR inayounganisha Kagera na nchi jirani Uganda na Rwanda kuchochea Biashara

Matukio, Taarifa, Habari na Mijadala ya Wananchi WAKATI wa Mchakato wa Uchaguzi Mkuu 2025

Richer

JF-Expert Member
Joined
Jun 9, 2025
Posts
1,446
Reaction score
2,093
Mgombea urais kwa tiketi ya Chama cha NLD, Doyo Hassan Doyo ameendelea kujinadi kwa Watanzania akieleza dhamira yake ya kufungua fursa za kibiashara kwa kujenga Reli ya Kisasa (SGR) hadi Kagera pamoja na kununua ndege ya mizigo.

Kwa sasa, reli hiyo ya kisasa imejengwa kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma, na ujenzi unaendelea kuelekea mikoa mingine hadi kufika Mwanza.

Doyo amesema lengo lake ni kuhakikisha reli hiyo inaendelea hadi Kagera, ili kurahisisha na kuharakisha usafirishaji wa mazao ya kilimo kama ndizi, kahawa na mengineyo yanayozalishwa kwa wingi mkoani humo kwenda kwenye masoko jijini Dar es Salaam na nchi jirani.

“Katika kukuza uchumi, ni muhimu Kagera ipate reli ya kisasa na ndege kubwa ya mizigo. Hii itasaidia mazao ya wakulima kusafirishwa haraka na kufika sokoni kwa wakati, hata katika nchi kama Burundi, Rwanda na Uganda,” amesema Doyo katika muendelezo wa kampeni zake mkoani Kagera

Akihutubia mkutano wa hadhara wilayani Ngara, leo Oktoba 1, 2025, Doyo pia aliahidi kujenga hospitali ya kanda na soko la kisasa katika mkoa huo

Amesema, akipewa ridhaa ya kuongoza nchi, hayo yatakuwa miongoni mwa mikakati yake ya kuboresha huduma za kijamii na kuinua uchumi wa wakazi wa Kagera

Amebainisha kuwa hospitali hiyo ya kanda itakuwa na vifaa vya kisasa na wataalamu wa afya, ili wananchi wa Kagera wapate huduma bora za matibabu bila kulazimika kusafiri umbali mrefu

“Sekta ya afya imesahaulika kwa muda mrefu, ilhali afya ndiyo uti wa mgongo wa taifa. Taifa lisilo na wananchi wenye uhakika wa huduma za afya ni taifa dhaifu linalopoteza nguvu kazi kila mwaka. Ndiyo maana dhamira yangu ni kuwekeza kikamilifu katika sekta ya afya,” amesema Doyo

Aidha, ameahidi kujenga soko la kisasa la mazao litakalowawezesha wakulima kuuza mazao yao kwa bei nzuri, kuongeza thamani na kuimarisha uchumi wa mkoa huo unaotegemea kilimo. Pia aliahidi kuliboresha zao la kahawa kwa kuhakikisha linapata thamani stahiki sokoni


 
Back
Top Bottom