DOWANS yaidai Tanesco Sh bilioni 122.5

R.B

JF-Expert Member
May 10, 2012
6,296
2,564
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) linakabiliwa na mzigo mkubwa wa deni la kuilipa Kampuni ya Dowans, ambalo sasa limefikia Sh bilioni 122.5 kutoka Sh bilioni 90 walizoamuliwa kulipa awali baada ya kuvunja mkataba.

Wakili wa Kampuni ya Dowans, Kenedy Fungamtama, alidai hayo jana katika Mahakama ya Rufaa Tanzania, wakati maombi ya TANESCO ya kuomba zuio la kuilipa kampuni hiyo lilipokwama kusikilizwa.

“Hadi Novemba 20, mwaka huu nilipokuwa nawasilisha majibu kwa kiapo kuhusu maombi ya TANESCO, deni lilifikia Sh bilioni 122.5 kutoka Sh bilioni 90.

“Kiasi hiki cha fedha, kimetokana na riba ya asilimi 7.5, wanayotakiwa kuilipa Dowans kila siku,” alisema Fungamtama.

Hata maombi ya zuio la kuilipa Dowans kiasi hicho, yalikwama kusikilizwa na jopo la majaji watatu, Benard Luanda, Nathalia Kimaro na Catherine Urio, baada ya kubaini mmoja wa majaji hao aliwahi kusikiliza kesi hiyo ikiwa Mahakama Kuu.

“Maombi tumeyapokea, tunaahirisha shauri hili hadi tarehe nyingine itakayopangwa, kwa sababu Jaji Urio aliwahi kuisikiliza kesi hii ikiwa Mahakama Kuu…hawezi kuendelea kusikiliza rufaa,” alisema Jaji Luanda.

Kesi hiyo, iliahirishwa na kusubiri tarehe na jopo lingine, baada ya Jaji Urio kuondolewa.

Rufaa hiyo ya kuomba zuio, iliwasilishwa Septemba 19, mwaka huu na Wakili Richard Rweyongeza, anayeitetea TANESCO, kuomba kusitishwa utekelezaji wa hukumu ya Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Kibiashara (ICC) kama ilivyoamuliwa na Mahakama Kuu, iliyolitaka shirika hilo liilipe Dowans.

Katika rufaa hiyo, TANESCO inaomba kusitishwa kwa utekelezaji wa uamuzi huo hadi kesi ya msingi ya kupinga uamuzi wa Mahakama ya Kimataifa itakapomalizika.

“Kiasi cha fedha wanachotakiwa kulipa TANESCO ni kikubwa na endapo itaamuliwa kilipwe, shirika litapata hasara kiuchumi, shirika liliwasilisha dhamana ya Dola za Marekani milioni 30 Mahakama ya Kimataifa kutokana na amri waliyopewa na mahakama hiyo,” ilisema sehemu ya maombi hayo ya zuio.

Septemba 6, TANESCO iliwasilisha ombi hilo katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, mbele ya Jaji Dk. Fauz Twaibu, ambaye alilitupilia mbali kwa madai kwamba mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza shauri hilo.

Novemba 15, 2010, TANESCO iliamriwa kuilipa Dowans Holding SA na Dowans Tanzania Ltd (Dowans), Dola za Marekani 65,812,630.03 pamoja na riba asilimia 7 kila siku na gharama za kuendesha kesi, baada ya kuvunja mkataba.

Hata hivyo, TANESCO ilipinga hukumu hiyo, lakini Septemba 28,2011, Jaji Emilian Mushi wa Mahakama Kuu alikubali kusajili tuzo ya malipo ya Dowans na kuiamuru TANESCO kulipa fedha hizo pamoja na gharama za uendeshaji kesi.

Jaji Mushi katika hukumu yake, alisema baada ya kuipitia hukumu ya ICC kabla ya kusajili tuzo hiyo, alibaini kuwa haina makosa ya kisheria kama lilivyodai shirika hilo.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

0 Reactions
Reply
Top Bottom