Dira watakiwa kumuomba radhi Ombeni Sefue

Mangare100

Member
Aug 21, 2012
57
25
JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
IDARA YA HABARI - MAELEZO

P.O. Box 8031, Dar es Salaam, Tel: 2110585, 2122771/3, Fax: 2113814, e-mail: maelezo@habari.go.tz Tarehe: 01/03/2016

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Gazeti la Dira ya Mtanzania, Toleo Na.404 la Februari, 29 – Machi 6, 2016 liliandika taarifa yenye kichwa cha habari kisemacho “Uchafu wa Ombeni Sefue Ikulu”. Taarifa hiyo, ambayo ni muendelezo wa makala nyingine kwenye toleo la gazeti hilo la wiki iliyopita, ilimtuhumu Katibu Mkuu Kiongozi kushawishi juu ya uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa MSD pamoja na Kampuni za “CRJE” na “UGG” kupewa tenda ya kujenga Chuo Kikuu cha Dodoma, Daraja la Kigamboni na Reli ya Dar es Salaam - Kigali. Taarifa zote hizi ni za uongo na za kupotosha wananchi.

Kuhusu uteuzi wa nafasi ya Mkurugenzi Mkuu wa MSD,
Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, hakuhusika kwa namna yoyote kushawishi uteuzi wa Mkurugenzi Mkuu wa MSD. Uteuzi huo ulitekelezwa kwa kufuata kanuni na taratibu zilizowekwa. Nafasi hiyo ilitangazwa na Bodi tarehe 20 Novemba, 2013. Usaili ulifanywa na kampuni huru iliyopewa jukumu hilo na Bodi. Mapendekezo ya majina matatu yalipelekwa kwa Mhe. Rais na Waziri wa Afya, kwa ajili ya uteuzi. Balozi Sefue alikuwa hamjui aliyeteuliwa na wala hakuwahi kuwa na uhusiano naye. Alichofanya Balozi Sefue ni kutangaza tu uteuzi baada ya Rais kuteua. Gazeti hilo pia limeandika uwongo kuwa MSD haijawahi kuongozwa na Mkurugenzi Mkuu asiye Mfamasia. Tangu MSD ianzishwe mwaka 1993 hadi sasa, ni Mkurugenzi Mkuu mmoja tu, Rino Meyers (1996-1999), ndiye alikuwa Mfamasia. Wakurugenzi wengine kama Peter Mellon (1993-1995), Jay Drosin (2001-2004) na Joseph Mgaya (2004-2013) hawakuwa Wafamasia.

Kuhusu Kampuni ya CRJE kuhusishwa na Balozi Ombeni Y. Sefue
Suala la kumhusisha Katibu Mkuu Kiongozi na kampuni hii nalo ni uzushi na uongo wa kupindukia. Wakati kampuni hii ikipewa tenda ya kujenga Chuo Kikuu cha Dodoma mwezi Oktoba 2007, Balozi Ombeni Y. Sefue hakuwa Katibu Mkuu Kiongozi; alikuwa Balozi wa Tanzania nchini Marekani. Kadhalika mchakato wa kumpata mkandarasi wa daraja la Kigamboni, ulipoanza mwezi Machi, 2011, Balozi Sefue hakuwa Katibu Mkuu Kiongozi; alikuwa Balozi wa Tanzania, Umoja wa Mataifa, New York. Hata mkataba wa ujenzi wa Daraja hilo uliposainiwa tarehe 9 Januari, 2012, Balozi Sefue alikuwa na wiki moja tu ya kuwa Katibu Mkuu Kiongozi kufuatia kuteuliwa tarehe 30 Disemba, 2011. Aidha, Kampuni iliyoshinda tenda hiyo wala siyo CRJE kama ilivyoandikwa na gazeti hilo bali ni China Major Bridges Engineering Company (BCEC) kwa kushirikiana na Kampuni ya China Railway Construction (CRCEG).

Kuhusu tuhuma kuwa Katibu Mkuu Kiongozi Chapuo Kampuni ya UGG:
Katibu Mkuu Kiongozi hajawahi kuipigia chapuo kampuni yoyote ile pahala popote. Isitoshe, hakuna kampuni yenye jina la “UGG” iliyowahi kuonesha nia ya kujenga reli ya kati. Hii ni moja ya uthibitisho kwamba gazeti hili linatoa taarifa za kuokoteza zisizo na ukweli kama vile walivyopotosha kuhusu jina la Katibu Mkuu Kiongozi kwenye makala yao ya pili kwenye ukurasa wa tisa wa gazeti hilo yenye kichwa cha habari “Magufuli anaishi na jipu Ikulu” ambapo walimpachika Katibu Mkuu Kiongozi jina la Sifuni, jina ambalo hajawahi kuwa nalo. Balozi Sefue hajahusika, hahusiki na wala hatahusika katika kuchagua wa kupewa tenda hiyo kwa sababu yeye si sehemu ya wenye mamlaka ya kutoa tenda.

Kuhusu Eliachim Maswi:
Gazeti la Dira ya Mtanzania limeandika kuwa moja ya “madudu” aliyofanya Balozi Sefue ni walichoita kumsafisha Bwana Eliachim Maswi. Wanadai hivyo wakati wamekiri kuwa alichofanya Balozi Sefue ni kusoma matokeo ya uchunguzi, ambao hakuufanya yeye. Waliomsafisha Maswi ni Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali; Sekretarieti ya Maadili ya Umma; na hatimaye kamati ya uchunguzi iliyoongozwa na Jaji wa Mahakama Kuu. Kwa hiyo, kwa maoni ya gazeti hili, Balozi Sefue asingepaswa kusoma matokeo ya uchunguzi uliofanywa na vyombo hivyo huru. Kwa maoni yao kusoma taarifa ya uchunguzi ni “madudu”.

Habari hizo hazina chembe yoyote ya ukweli, na wao wenyewe ndani ya gazeti wamekiri hawana ushahidi, ni wazi kuwa habari hizo ni za kubuni na zimetungwa.

Kwa sababu hiyo, Serikali inalitaka Gazeti la Dira ya Mtanzania kukanusha uongo na uzushi wao na kumuomba radhi Balozi Ombeni Sefue, kuiomba radhi Serikali na kuwaomba radhi wote walioumizwa na uzushi huo kwa uzito ule ule uliotumika kuchapisha taarifa hiyo.

Vinginevyo iwapo gazeti la Dira ya Mtanzania lina ushahidi wa huo “uchafu” wa Katibu Mkuu Kiongozi, waupeleke mara moja kwenye vyombo vinavyohusika ikiwamo Sekretarieti ya Maadili na TAKUKURU. Vinginevyo, hatua zikichukuliwa dhidi yao wasiseme Serikali inavibana vyombo vya habari.

Aidha Serikali inashauri wenye vyombo vya habari, wachapishaji, wahariri na waandishi wa habari wajikite kwenye weledi na ukweli, wafanye utafiti na kuandika mambo waliyo na uhakika nayo, na kamwe wasikubali kutumiwa kuendeleza agenda za watu wengine.

MWISHO.
 
pole balozi Sefue kwa haya, ndio athari za vyombo vya habari,haya yapo hata nchi za dunia ya kwanza, wasamehe na tuendelee na mapambano ya kumweka mtanzania mbele ki maendeleo
 
Hata mimi niliumia sana, Hili Gazeti liombe radhi kabisa tena front page, yawezekana mafisadi wanalitumia Gazeti hili kumchafua Balozi kutokana na kazi kubwa aliyoifanya wakati baraza la mawaziri halijateuliwa na kutangazwa.
 
Tena Mafisadi wameona nongwa kwa nini Magufuli Yupo karibu na amemwamini sana huyu Balozi Ombeni sefue, wanahisi kwamba yawezekana baadhi ya Taarifa au ushauri muhimu Balozi alimpa au alimweleza Rais.

Hakuna kurudi nyuma, Dira lifutwe kabisa na lisahaulike katika kumbukumbu ya magazeti nchini.
 
Hata mimi niliumia sana, Hili Gazeti liombe radhi kabisa tena front page, yawezekana mafisadi wanalitumia Gazeti hili kumchafua Balozi kutokana na kazi kubwa aliyoifanya wakati baraza la mawaziri halijateuliwa na kutangazwa.
Kwa mambo yetu yale ya kukanusha, nasubiria mwisho wa muvi
 
Kiukweli hata mimi sijufurahishwa na niliumia sana. Inabidi watuombe radhi kwanza watanzania halafu wamuombe radhi Balozi Omben Sefue kisha waiombe serikali msamaha. Sitalinunua tena hili gazeti hata wasipolifungia
 
Hata mimi niliumia sana, Hili Gazeti liombe radhi kabisa tena front page, yawezekana mafisadi wanalitumia Gazeti hili kumchafua Balozi kutokana na kazi kubwa aliyoifanya wakati baraza la mawaziri halijateuliwa na kutangazwa.

Ama watupe ushahidi usio na shaka, tofauti ya hapo kuna haja ya kutoa fundisho la kukurupuka tu.
 
W
Kiukweli hata mimi sijufurahishwa na niliumia sana. Inabidi watuombe radhi kwanza watanzania halafu wamuombe radhi Balozi Omben Sefue kisha waiombe serikali msamaha. Sitalinunua tena hili gazeti hata wasipolifungia

Wahariri wa DIRA wana ushahidi wa yale yote waliyoandika. Tatizo idara ya habari MAELEZO haitaki kuwasikiliza ilhali ni wao waliwaandikia barua ya wito kuwataka wafike MAELEZO kujieleza. Wamefika warasimu wa MAELEZO wakakataa kuwasikiliza. Mimi nashauri ushahidi wao waupeleke kwenye vyombo husika kabla ya kuomba radhi.
 
ipo haja ya kupitia upya sera ya habari, hivi vijarida vikishindwa kuuza magazeti vinaanza kuzusha mambo ya hovyo. balozi wala usivitazame wewe endelea kukamia majipu, inaonekana kuna mtoto kakamuliwa ndo maana makelele yameenea wodi nzima.
 
Tunajenga Nchi ya waandishi wasiojua kufanya tafiti!- Ukweli Nchi haiwezi kuendelea kwa hawa waandishi wanaopenda bahasha na kuandika uzushi!
 
Sefie atulie tu, ndo utu uzima huo! Mbona Jk kila siku alikuwa anazushiwa mapya, amewadharau mwisho wamechoka, life goes on!
 
Hamna lolote hapo ni vita ya Charles Kitwanga kipenzi cha Magu dhidi ya Sefue kachero na kipenzi cha Msoga. Ngoma inaanza kulia sana.
 
Kutetea uongo ni kazi ngumu sana! Kanusho ukurasa mmoja ungetosha badala ya gazeti lote hilo.
 
Inawezekana kabisa kwamba kilichoandikwa kuhusu Sefue ni majungu ya kumchafua na kumchonganisha na Magufuli! Lakini kwa nini mhusika/mtajwa/mtuhumiwa asijitokeze mwenyewe kuwataka Dira wamwombe radhi na kukanusha habari hizo? Kwa nini hilo lifanyike na Idara ya Habari- Maelezo? Na kwa nini asiende mahakamani kudai kusafishwa na kulipwa fidia? Maana tuhuma ni nzito sana na madhara yake ni mapana, hayawezekani kurekebishwa kwa Dira kuomba tu radhi!
 
Back
Top Bottom