DCI alistahili kufukuzwa

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,011
DCI alistahili kufukuzwa


JUZI katika gazeti hili kulikuwa na habari iliyoeleza kuwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Robert Manumba, alikutana na adha za kisiasa pale viongozi wa vyama vya siasa, hasa vya upinzani, walipoamua kumtimua katika mkutano wao ulioitishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa.
Uamuzi wa kumtimua DCI katika mkutano huo ulifikiwa baada ya majadiliano yaliyotawaliwa na jazba, ambayo wakati fulani yalielekea kuzua vurugu na kutishia kuvunjika kwa mkutano huo, kutokana na kile kilichoelezwa kuwa DCI hakupaswa kuhudhuria kikao hicho kilichowahusu wanasiasa.

Katika majadiliano hayo, wanasiasa waliokuwa wakipinga uwepo wa DCI katika mkutano huo, pia walimlaumu Tendwa kwa kuwaletea barua za mwaliko ambazo hazikueleza kuwa kiongozi huyo wa Jeshi la Polisi nchini, angekuwapo katika mkutano wao.

Viongozi hao walisema kitendo hicho cha Tendwa kumwalika DCI katika mkutano wao bila taarifa, si tu kwamba kilionyesha dharau kwao, bali pia kingewafanya kuingia hofu na kuogopa kujadili masuala yao ya kisiasa kwa uwazi.

Hofu hiyo imetokana na hoja ya msingi kuwa, DCI si mwanasiasa bali ni Polisi, hivyo wakahoji katika mkutano huo alikwenda kufanya nini au kupeleleza kitu gani? Hilo ndilo swali la msingi ambalo wadau wengi wa siasa wanajiuliza hadi sasa.

Kabla ya kufikia uamuzi huo, Tendwa alisema Manumba ni mmoja wa wadau katika masuala hayo na pia katika utendaji wake wa kazi anasimamia kazi za vyama vya siasa.

Hata hivyo, Tendwa mwenyewe alikiri kukosea kiutendaji kumwalika DCI bila kuwataarifu viongozi hao ambao ndio walikuwa walengwa.

Tunaunga mkono uamuzi wa viongozi wa siasa, kwani hata sheria namba 5 ya vyama vingi vya siasa, haijaeleza kuwa DCI naye ni mmoja wa watu wanaopaswa kuhudhuria mikutano ya kisiasa.

Ni dhahiri kuwa uamuzi wa kumtimua DCI katika mkutano wa viongozi wa vyama vya siasa si tu kwamba umemdhalilisha, bali pia umemvunjia heshima yake katika jamii.

Hata hivyo, Tendwa ndiye wa kubebeshwa lawama kwa kusababisha DCI adhalilishwe, kwani hakutoa taarifa kwa viongozi wa siasa kama DCI angekuwa mmoja wa viongozi waalikwa kwenye mkutano huo.

Si sahihi kusema kuwa DCI ni mmoja wa wadau wa siasa wakati wadau wakubwa katika siasa, waandishi wa habari, walizuiliwa kuhudhuria kikao hicho.

Tunaamini kuwa hakuna ubaya kwa DCI kuhudhuria kikao hicho au kingine chochote cha siasa kama wadau watajulishwa, lakini kwanini Tendwa hakuwajulisha kabla viongozi wa siasa juu ya uwepo wa kiongozi huyo wa Polisi?

Tendwa alikuwa na ajenda gani ya siri kumwalika DCI kwenye mkutano ambao hakustahili kuwepo?

Tendwa lazima ajue kuwa zipo taratibu, na taratibu hizo lazima ziheshimiwe, kwani wana siasa ni watu muhimu na walipaswa kufahamishwa tangu awali.

Tunasisitiza kuwa DCI hakupaswa kuwapo kwenye mkutano huo, kwani uwepo wake ungewanyima uhuru viongozi hao kujadili masuala ya siasa kwa uwazi, hasa katika kipindi hiki ambacho wapinzani wamekuwa mstari wa mbele kutoa taarifa za ufisadi zinazowakabili baadhi ya viongozi wa siasa nchini.

Kama ni suala la kuwa na mwakilishi wa serikali katika kikao hicho, Tendwa angeweza kumwalika waziri mwenye dhamana ya siasa, kwani viongozi wa siasa wa upinzani wana mambo mengi ya kujadiliana na waziri husika.

Tuwaache viongozi wa siasa wafanye kazi ya siasa, na Polisi wasimamie jukumu kubwa walilonalo la ulinzi na usalama wa wananchi na mali zao, ili kudumisha amani, upendo na mshikamo uliopo miongoni mwa Watanzania.

Kutokana na hali iliyojitokea juzi katika mkutano huo, tunaamini kuwa Tendwa atakuwa amejifunza kutokana na kosa hilo, wakati mwingine atakuwa makini.

Source: Tanzania Daima
 
Back
Top Bottom