Kuhusu chanzo cha tukio hilo, Kiule alisema ni kutokana na mgogoro wa ardhi wa eneo la wazi lililogawanywa na diwani wa kata ya Nguvumali, Selemani Mhina (sele boss) CCM, lililopo mbele ya kanisa la Kigango cha Majani Mapana kinyume cha sheria za ardhi.
Alisema kanisa katoliki lilishaomba eneo hilo zaidi ya mara mbili kwa Jiji la Tanga na kujibiwa kuwa ni eneo la wazi na lakini lilitolewa kwa wafanyabiashara kwa madai kuwa ni agizo la mkuu wa wilaya ili kujenga mashine za kusaga nafaka.
Kwa upande wa padre Kabosa alikiri kupatwa na kadhia hiyo lakini alidai kuwa tayari suala hilo linashughulikiwa na viongozi wakuu wa kanisa hilo kwa hatua zaidi za kurejesha amani na mshikamano ulioonekana kukosekana.
Naye Mkuu wa wilaya, Dendego alipotakiwa kuelezea shutuma hizo alikiri ujio wa padre Kabosa ofisini kwake na kutofautiana kimazungumzo lakini alidai kuwa alimuamuru kuondoka ofisini hapo kwa kuwa hakumtambua kama ni kiongozi wa dini.
Hata hivyo Mkuu huyo wa Wilaya alikanusha tuhuma za kueneza udini na kwamba hilo halikufanyika kwa ajili ya udini bali ni moja ya matokeo ya kiutendaji.
Alimtupia lawama na kumtaja diwani Mhina kuwa ndiye anayechochea mgogoro huo kwa kueneza udini kuwa yeye anawapendelea waislamu jambo ambalo ni hatari.
Chanzo: Nipashe Jumapili