barafu
JF-Expert Member
- Apr 28, 2013
- 6,739
- 32,866
MKUU wa wilaya ya Longido, Daniel Chongolo ameiomba serikali isiwapatie wananchi wake chakula cha njaa wala cha gharama nafuu, badala yake wajifunze kuuza sehemu ya mifugo yao na kununua chakula kwa ajili ya kaya zao.
Chongolo alisema hayo jana mbele ya wajumbe wa kamati ya ushauri ya mkoa cha kupitisha bajeti ya mkoa ya mwaka 2017/2018.
Kwa mujibu wa Chongolo, wananchi wa wilaya yake asilimia 90 ni wafugaji kwa asili yao na kwamba wana mifugo mingi lakini hawataki kuuza kwa ajili ya kununua chakula tofauti na nyama.
Alisema amefanya ziara katika kata 18 za wilaya hiyo na kubaini kuwa wananchi hao wana mifugo mingi lakini wanalalamika njaa ili serikali iwape chakula cha bure.
“Huu ni upuuzi kuwadekeza wananchi ambao wanakumbatia mamia ya mifugo waliyo nayo na kugoma kuiuza kwa ajili ya kununua chakula.
Nasema serikali msutupe chakula cha njaa wala cha bei nafuu, wauze mifugo wanunue mahindi wao siyo wakulima,” alisema.
Alisema wilaya hiyo ina maghala ya bure ambayo yamejengwa na PWC kwa ajili ya wananchi kununua mazao kipindi cha mavuno na kuyahifadhi bure ili waweze kupata chakula cha njaa lakini wananchi hao hawataki kuuza mifugo.
Alisema kipindi cha Mei mpaka Julai ni kipindi cha mavuno ambapo pia mifugo inakuwa na afya nzuri na ng’ombe mmoja anauzwa kati ya Sh 700,000 mpaka milioni moja na fedha hizo zinatosha kwa mfugaji kununua hata gunia 12 na kuzihifadhi kwenye maghala hayo kwa ajili ya chakula, lakini wanagoma.
Aidha alisema kutokana na kutotaka kuuza mifugo mwaka huu kupitia maofisa maendeleo ya jamii ikifika kipindi cha mavuno watachukua ng’ombe mmoja kutoka kila familia na kumuuza kisha kununua mahindi na kuyahifadhi kwenye ghala kwa ajili ya familia husika.
Kwa upande, Mkurugenzi wa halmashauri ya wilaya hiyo, Juma Mhina alisema wananchi hao wana dhana potofu kuwa chakula ni mahindi pekee jambo ambalo si kweli.