DAWASA kumaliza kero ya maji ya miaka 30 Mpiji Magohe

DAWASA kumaliza kero ya maji ya miaka 30 Mpiji Magohe

DAWASA

Official Account
Joined
Oct 7, 2010
Posts
158
Reaction score
103
Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imeanza utekelezaji wa mradi wa kuboresha huduma ya maji kwa wakazi wa Mpiji Magohe, Kata ya Mbezi, Wilaya ya Ubungo, hatua inayotarajiwa kumaliza changamoto ya upatikanaji wa maji iliyodumu kwa muda mrefu katika eneo hilo.

Mradi huo unatarajiwa kukamilika mapema mwezi Julai 2026 na utawezesha wakazi wa maeneo mbalimbali ikiwemo Mpiji Center, Kengai, KKT, Pande, Capetown, Toronto, Sabato, Msikiti wa Igoma, Kwa Mwalimu, Maendeleo A, B, C, D, E na F, Mkurugenzi Road, Huruma, Igoma, Ekarua pamoja na Shule za Msingi na Sekondari za Mpiji Magohe kupata huduma ya maji safi na salama.

Akizungumza kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Kaimu Meneja wa Mkoa wa Kihuduma wa DAWASA Ubungo, Mhandisi Alphonce Magoma, amesema mradi huo unahusisha uchimbaji na ulazaji wa mabomba ya maji ya inchi 6 na inchi 2 kwa umbali wa kilomita 15, ili kufikisha huduma hiyo kwa wakazi wa Mpiji Magohe na vitongoji vyake.

“Mradi huu utasaidia kuwapatia wakazi wa Mpiji Magohe maji safi badala ya maji ya chumvi ambayo wamekuwa wakiyatumia kwa kipindi kirefu. Kutokana na changamoto hiyo kuwa sugu, mamlaka imeamua kutekeleza mradi huu ili kumaliza kabisa tatizo la maji katika eneo hilo,” amesema Mhandisi Magoma.

Ameongeza kuwa mradi huo unatarajiwa kunufaisha wakazi wapatao 300, huku ukichangia kuboresha hali ya maisha na kuinua uchumi wa wananchi ambao wamekuwa wakilazimika kununua maji ya chumvi kwa gharama kubwa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa Mpiji Magohe, Said Diuchile, ameishukuru DAWASA kwa kuanza utekelezaji wa mradi huo akieleza kuwa wananchi wa eneo hilo wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya maji kwa zaidi ya miaka 30.

“Tumeishi na changamoto ya maji kwa takribani miaka 30 na tumekuwa tukitegemea maji ya chumvi kama chanzo kikuu cha maji. Maji hayo ni ghali na baadhi ya wananchi wanalazimika kutembea umbali mrefu kuyatafuta. Hivyo tunachoona sasa ni kama ndoto iliyochelewa kutimia,” amesema Diuchile.
WhatsApp Image 2026-03-10 at 21.20.14 (1).jpeg

Naye mkazi wa Mtaa wa Igoma amesema mradi huo ni msaada mkubwa kwa wananchi wa eneo hilo ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakipata maji kwa gharama kubwa, akieleza kuwa awali ndoo ya maji ya lita 20 ilikuwa ikiuzwa kuanzia shilingi 500.​
 

Attachments

  • WhatsApp Image 2026-03-10 at 21.20.14.jpeg
    WhatsApp Image 2026-03-10 at 21.20.14.jpeg
    186.5 KB · Views: 3
Back
Top Bottom