Wanajamvi,
Napenda nichukue fursa hii kuanzisha somo la siasa kwa Waswahili wote wa Shirikisho letu tukufu la Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa Zanzibar,
Hii itakuwa fursa kwa vijana wengi wanaochipukia katika siasa za kileo,
Mambo makuu muhimu nitakayofundisha ni:
1. Maana ya siasa.
2. Itikadi za vyama vya siasa
3. Katiba za vyama vya siasa
4. Siasa za kisasa
5. Maisha ya mwanasiasa.
Nitatumia lugha yetu adhimu ya kiswahili katika kuwafunza haya.
Sehemu ya Kwanza.
Siasa ni nini?
Siasa ni itikadi inayofuatwa na kundi au jamii fulani ambayo ni msingi kuendesha uchumi, utamaduni na mwenendo mzima maisha ya jamii hiyo.
Itaendelea......
.............................. ......
Kabla hatujaangazia itikadi za vyama, nataka tujifunze na tuelewe, Itikadi ni nini?
Itikadi ni mkusanyiko wa imani unaoshirikiwa na kikundi cha watu fulani.
Kuna aina kuu mbili za itikadi:
Itikadi za kisiasa, na itikadi za kiepistemolojia (ni sehemu ya falsafa ambayo inahusu utafiti wa jinsi tunavyojua mambo).
Itikadi ya kisiasa ni upangiliaji unaohusu mawazo ya kimaadili na vipi nchi itaendeshwa.
Itikadi za kiepistemolojia ni upangiliaji unaohusu mawazo ya kifalsafa, ulimwengu, na jinsi gani watu wanapaswa kufanya maamuzi.
Kwakuwa somo letu linahusu siasa, hivyo nitajita kufundisha itikadi ya kisiasa zaidi katika kipengele hiki cha itikadi.
ITIKADI ZA KISIASA.
Katika dunia ya leo, Itikadi za kisiasa zimegawanyika katika makundi makubwa sita kama ifuatavyo:
1. Ukomunisti
2. Ujamaa
3. Ujamaa wa kidemokrasia
4. Uliberali
5. Uhafidha Liberali
6. Uhafidhiana
Mpangilio huu wa itikadi hutokea kushoto kuelekea kulia kama ifuatavyo:
Ukomunisti=>Usoshalisti=>Ujama a wa Kidemokrasia=>Uliberali=>Uhafi dhina Uliberali=>Uhafidhina
Kwahiyo kwa mfano, itikadi ya kikomunist, na kijamaa zinatambulika kama itikadi za mrengo wa kushoto, wakati itikadi ya uhafidhiana inatambulika kama itikadi ya mrengo wa kulia.
Itikadi za mrengo wa kushoto (Ukomunisti, Ujamaa na Ujamaa wa kidemokrasia), asili yake ni Karl Max ambae alidai kwamba Ubepari ni muundo wa kinyonyaji na kikandamizaji. Wengi wetu tayari tunalielew vizuri suala hili.
UKOMUNISTI
Utawala: Mamlaka yote ipo chini ya umma, Hakuna chaguzi kwani serikali ya kikomunisti inakubalika na wote. Maisha yote ya jamii, kuanzia utawala, uchumi na maisha binafsi, yapo chini ya serikali.
Hakuna soko wala ubadilishanaji wa aina yoyote; hakuna umiliki binafsi wa mali; bidhaa na huduma zote zinagawanywa sawa katika jamii bila ya ubaguzi wa aina yoyote.Hakuna matabaka ya aina yoyote miongozi mwa wafanyakazi. Kuna mapinduzi yanayolenga kufuta uhaba na pia umiliki binafsi wa mali. Wananchi hupatiwa huduma zote za msingi na serikali bure, kwa mfano elimu, afya, n.k.
UJAMAA.
Masuala ya umma yanaendeshwa kwa nguvu za kimuundo iliyopo chini ya muundo wa halmashauri, kuanzia ngazi ya chini mpaka taifa. Ingawa mara nyingi huwa na chama kimoja cha siasa, huwa kunakuwepo na chaguzi za mara kwa mara, hivyo viongozi kuanzia ngazi ya halmashauri mpaka juu hutokana na watu. Kuna serikali za makusudi za kuunganisha serikali na jamii nzima. Uwepo wa mishahara isiyotofautiana sana; Pia huduma na bidhaa nyingi kwa umma hutolewa na serikali. Kuna muungano wa tabaka la wafanyakazi; uwepo wa fursa sawa kwa watu wote bila kujali matabaka. Kuna mapinduzi ya kuangamiza ubwanyenye. Umiliki wa umma wa njia kuu za uchumi, na matumizi ya rasilimali ya taifa kwa manufaa ya umma pamoja na upatikanaji wa huduma zote za msingi kwa watu wote.
UJAMAA WA KIDEMOKRASIA.
Masuala yote ya umma yanaendeshwa na viongozi waliochaguliwa kupitia muundo wa kidemokrasia. Viongozi wa umma hutokana na chaguzi za mara kwa mara zenye uwazi na uhuru kwa wapiga kura; Serikali thabiti huitajika ili kuendesha mipango na sera za kugawanya keki ya taifa. Ubepari unakubalika, na unashamiri kupitia muundo thabiti wa kugawana keki ya taifa na upatikanaji wa huduma bora za kijamii. Kuna umoja wa kitabaka miongozi mwa wafanyakazi kupitia taasisi zinazounganisha tabaka hili. Mapinduzi hayahitajiki kwani ubepari unakubalika hivyo kuendelea kushamiri. Msisitizo mkubwa ni uwepo wa a Welfare State, yenye Social security programs zinazolenga kutoa msaada kwa wote wanaostahili - kama vile huduma ya afya, elimu, makazi, n.k. Pia serikali hugawanya mapato kwa kutoza kodi za aina mbali mbali kwa lengo la kupunguza tofauti za kiuchumi baina ya matabaka mbalimbali, huku pia ikiweka kinga thabiti kwa watu wasio na ajira, wagonjwa, na wastaafu..
Na sasa tuziangalie itikadi za mrengo wa kulia Uliberali, Uhafidhina wa Kiliberali, na Uhafidhiana.
1. ULIBERALI
Asili ya itikadi hii ilikuwa ni kupigania haki za watu katika jamii za mataifa ya magharibi yaliyokuwa chini ya tawala za kifalme; tawala hizi hazikutoa haki na fursa sawa za kiuchumi kisiasa na kijamii kwa wananchi. John Locke ndiye (mwanzilishi), na wenzake walidai kwamba binadamu huru ndio msingi wa jamii imara yenye amani na utulivu; pia walihimiza umuhimu wa kuwepo kwa serikali yenye wajibu wa kulinda haki za msingi za wananchi; harakati hizi ndiyo zilizokuja kuzaa dhana nzima ya demokrasia ya uwakilishi. Baadae harakati hizi ziilichochea kuzaliwa kwa uliberali katika eneo la uchumi, muasisi wake akiwa Adam Smith, ambae alihimiza umuhimu wa serikali kutoingilia shughuli za kiuchumi, kwa mtazamo kwamba, serikali ikiachia shughuli za uchumi zijiendeshe na kujisahisha zenyewe itapelekea ufanisi zaidi katika uchumi. Katika dunia ya leo, Itikadi hii bado ina nguvu kubwa. Kuna jamii nyingi duniani zinazo himiza umuhimu wa serikali kutojiingiza katika shughuli za kiuchumi na kijamii, kwa mfano, serikali kukaa mbali na na utoaji wa huduma za kijamii afya, elimu n.k; na pia serikali kutoshiriki katika uchumi kupitia mashirika ya umma, na badala yake, mashirika binafsi pekee ndiyo yatawale shughuli za kiuchumi.
2. ULIBERALI NA UHAFIDHINA
Itikadi hii ni mchanganyiko wa mawazo, sera na imani za uliberali na uhafidhiana. Itikadi hii inaunga mkono ulegezaji wa masharti mbalimbali ya kiuchumi na utandawazi, Pia inaunga mkono sera kali zinazozuia uhamiaji.
Kiuchumi itikadi hii inaunga mkono uwepo wa uhuru wa kiuchumi miongoni mwa wananchi, hasa kuwapatia wananchi uhuru wa kujiamulia mambo yao wenyewe. Itikadi hii haijihusishi sana na masuala ya kijamii lakini kila inapobidi kufanya hivyo, huwa na msimamo wa kijamii ulio sawa na ule wa kiliberali (rejea dhana ya uliberali hapo juu).
3. UHAFIDHINA.
Asili ya itikadi hii ni harakati za kupinga mapinduzi ya kumwondoa mfalme wa Ufaransa katika karne ya kumi na nane. Uhafi maana yake ni kuhifadhi, hivyo wahafidhina hawaamini katika mabadiliko au uharibifu wa desturi/utamaduni. Edward Burke ni muasisi wa itikadi hii; yeye alipinga mapinduzi ya kumwondoa mfalme wa ufaransa kwa mtazamo kwamba kitendo hicho kitaharibu desturi, imani na taasisi zilizojengwa kwenye jamii kwa muda mrefu ambazo ni muhimu katika maisha ya watu. Katika siasa za leo, wahafidhiana wanapinga ushiriki wa serikali katika uchumi kwa madai kwamba, umaskini ndani ya jamii ni matokeo ya serikali kuingilia maisha ya wananchi kwani kitendo hiki hulea watu wavivu, na kuua dhana ya uchapa kazi na uwajibikaji katika jamii. Badala yake, wahafidhiana wanahimiza kila mtu kujipatia riziki yake kwa jasho lake, na sio kusubiri serikali kupitia huduma za kijamii, n.k. wahafidhiana pia wanapinga uwepo wa mashirika ya umma katika uchumi, na badala yake wanahimiza uchumi uendeshwe na mashirika binafsi.
Katika siasa mpya, itikadi hizi kuu zimezaa itikadi nyingine tatu kubwa ambazo ni: (1) Mrengo wa Kati; (2) Mrengo wa Kati-kulia; na (3) Mrengo wa Kati-kushoto;
Ukomunisti>Ujamaa=>Ujamaa-wa-Kidemokrasia=>Uliberali=>Ulibe rali wa Kihafidhina=>Uhafidhiana
1. Itikadi ya Mrengo wa Kati
Huu ni mrengo kati ya Uliberali na Ujamaa wa kidemokrasia. Kwa kawaida, Itikadi ya mrengo wa kati inaamini na kuunga mkono mambo makuu yafuatayo:
· Ongezeko la kodi linaloenda sambamba na ongezeko la vipato vitokanavyo na shughuli za uchumi, Umiliki binafsi wa mali; Uhuru na haki ya wananchi mbele ya sheria;
Uliberali wa kiuchumi na uliberali wa kijamii.
· Kuwapatia wananchi uhuru wa kujiendeshea shughuli zao bila ya kuingiliwa na serikali; Umiliki wa mali binafsi; Serikali kuratibu/rekebisha uchumi, lakini wanapinga serikali kukwaza uhuru wa biashara na ushindani katika soko; wanaunga mkono sera za serikali za kuondoa ukiritimba binafsi kwa imani kwamba ukiritimba huu unaumiza wananchi maskini;
Uliberali wa jamii kwa maana
· Haki ya kijamii na uhuru kwa watu wote; Wajibu wa serikali kuinua hali za maisha ya wananchi kwa njia kama vile ajira, afya, elimu, huku haki za wananchi zikizidi kuimarishwa.
2. Mrengo wa Kati-Kulia.
Huu ni mrengo uliopo katikati ya Uliberali na Uhafidhina-Uliberali.
· Kwa ujumla, itikadi hii inaunga mkono kanuni nyingi za soko huru; lakini vilevile inapinga serikali kujiingiza kupita kiasi kwenye shughuli za kiuchumi (kupitia mashirika ya umma); inapinga serikali kujingiza kupita kiasi kwenye utoaji wa huduma za kijamii (kama vile afya na elimu); na inaunga mkono umiliki wa mali binafsi;
3. Mrengo wa Kati Kushoto
Huu ni mrengo uliopo kati ya Ujamaa wa Kidemokrasia na Ujamaa.
Mrengo huu unaamini katika yafuatayo:
· Jamii endelevu na serikali endelevu; Uliberali wa kijamii (rejea hapo juu), na siasa za kijani, pia ina amini katika mchanganyiko wa sekta ya umma na sekta binafsi kuendesha huduma za kijamii kama vile elimu, afya n.k; Uwepo wa uhifadhi wa akiba ya kutosha kwa wananchi wanaostahili tu (sio katika kiwango cha Ujamaa na Ukomunisti) ili kupunguza kasi ya umaskini na kulinda vipato vya wananchi wanaioshi katika mazingira ya uzee (wastaafu), wagonjwa, walemavu na wasio na ajira; mrengo huu pia una amini katika haki na fursa sawa kwa wote; inaunga mkono uwepo na umuhimu wa taasisi za serikali zinazoratibu sekta binafsi kwa nia ya kutetea wafanyakazi na walaji, kwa kuhakikisha uwepo wa vyama imara vya wafanyakazi, na pia ushindani wa haki katika soko; pia wanaunga mkono ongezeko la kodi linaloenda sambamba na ongezeko la vipato katika uchumi, lengo kuu likiwa kukusanya kodi ya kutosha ili isaidie kutoa huduma muhimu za kijamii kwa wale wanaostahili
Itaendelea.....
Sasa tuangazie itikadi za vyama vinne vyenye ufuasi mkubwa nchini ambavyo ni NCCR MAGEUZI, CUF, CHADEMA na CCM.
1.NCCR MAGEUZI=>Mrengo wa KUSHOTO (Ujamaa wa kidemokrasia)
2. CUF=>Mrengo wa KULIA (Uliberali)
3.CHADEMA=> Mrengo wa KATI (Uliberali na Ujamaa wa kidemokrasia)
4.CCM=> Mrengo wa KUSHOTO (Ujamaa)
Itaendelea.........