jumanne saa tano asubuhi jamaa na ulabu
NA HEMED KISANDA
Hii ndiyo Bongo bwana, wenyeji wa jiji la Dar es Salaam wanamisemo mingi ya kulitukuza jiji lao na mara nyingi utawasikia wakisema tumia Bongo uishi Bongowakimaanisha kuwa ili uweze kuishi maisha safi ukiwa ndani ya jiji hili basi inakubidi utumie akili nyingi, achilia mbali kujifunza utapeli wa hapa na pale.
Licha ya kuwa jiji liko kwenye moja ya nchi maskini duniani ambazo zimefanikiwa kufutiwa madeni katika mpango wa kusamehe madeni wa Kundi la Nchi Nane,lakini limeendelea kuwa ni moja ya miji mikubwa yenye umaarufu wa starehe kuliko maendeleo yake kimazingira.
Hii inaamanisha kuwa wakazi wengi wa Bongo wanapenda kustarehe zaidi kuliko kufanya kazi, hivi sasa hapa jijini imeshakuwa kawaida kukuta watu wakiendelea kuchapa kilevi (Kunywa pombe) muda wa kazi na mambo yakawa safi kama kwamba walikuwa kwenye ofisi zao siku nzima.
Unapotembelea mitaa ya Sinza, Kinondoni, Tegeta, Mbezi Beach, Temeke utakuta siku hizi baa zipo hatua chache kutoka ilipo nyingine na si ajabu kukuta baadhi ya baa zilizoko meneo hayo zimefurika watu wakipiga soga na juu ya meza zimetapakaa bia lakini ukiangalia saa yako mkononi utagundua kuwa ni saa za kazi na hapo ndipo utakapo jiuliza maswali mengi kuwa watu hawa wamefanya kazi wakati upi?
Haielewiki hali hii inasababishwa na nini, uvivu wa wananchi ama hali ya amani iliyopo hapa nchini ndiyo inasababisha watu kujisahau na kuhisi maendeleo ya nchi yanapatikana baa na siyo kwa kufanya kazi kwa bidii kwenye shughuli zao za kuzalisha mali.
Lakini Kitu cha ajabu ni kuwa wakazi na wenyeji wa jiji la Moscow huko nchini Urusi ndiyo wanashikiria rekodi ya wapiga mtungi (walevi) kuliko sehemu nyingine yoyote duniani lakini mbona wako juu kimaendeleo?
Maswali bila majibu: Tufanye nini Bongo ifanane na Tokyo ama Seoul?, ishu ni viongozi wabovu ama uzembe wa wananchi kwenye kazi kwa kukimbilia ulabu, hakuna mtu kutoka Ulaya ambaye atakuja kutuelezeka tufanye kazi kama sio sisi wenyewe.
Iliwahi ripotiwa kuwa wafanyakazi wa idara za Serikali na sekta mbalimbali huko nchini Japani hufanya kazi masaa 24 ndiyo maana wameweza kufika hapo walipo. Je, mfumo huu unafaa kuigwa hapa Bongo? Je, Wabongo watalipokeaje hili endapo litapitishwa?
source:global publishers