DAR: Polisi wadaiwa kumuua Mwanafunzi kwa kumpiga risasi tumboni wakimtuhumu kuwa ni jambazi

Ghazwat

JF-Expert Member
Oct 4, 2015
23,718
66,266
Askari wa Jeshi la Polisi, Kituo cha Kigamboni wanadaiwa kumuua kwa kumpiga risasi tumboni, Mwanafunzi wa chuo cha Uvuvi Mbegani, Bagamoyo Bonaventure Kimali (25) wakimtuhumu kuwa ni jambazi.

Tukio hilo la kusikitisha lilitokea saa 3:30 usiku wa kuamkia juzi huko Kigamboni Vijibweni, nyumbani kwa kaka wa marehemu aitwaye, Naftan Barampami ambaye alikuwa akiishi naye.

Akisumulia jinsi ilivyokuwa, Barampami alisema usiku huo wakiwa bado wapo nje ya nyumba yao huku kila mmoja akiendelea na shughuli zake ndogo ndogo na wengine wakiwa wamejipumzisha, ghafla walishangaa kusikia milio ya risasi zilizopigwa mfululizo.

"Tulishtuka, milio hiyo ilitokea upande wa uwanjani ambapo ni jirani na nyumbani kwetu, tuliogopa kila mtu ilibidi atafute namna ya kujiokoa, tulikimbia, mimi nilikimbilia ndani, Boni alikimbia kuelekea nyuma ya nyumba yetu", alisema.

Alisema akiwa ndani ya nyumba yake alisikia mtu akilia huku akiwasihi watu waliokuwa wamemzingira wasimuue.

"Ikabidi nisogee jirani zaidi na dirisha, nikakaa kwa utulivu na kuangalia nje kupitia dirishani kilichokuwa kikiendelea, ghafla nilisikia Boni akilia kwa uchungu huku akiugulia maumivu, kumbe walikuwa tayari wamempiga risasi", alisema.

Alisema askari wote walikuwa wamevaa kiraia, marehemu alikuwa akiendelea kuwasihi wasimuue huku akiwasihi wamuwahishe hospitalini kwani alikuwa akisikia maumivu makali.

"Aliwaomba wampeleke hospitali na watujulishe ndugu zake lakini hawakumsikiliza, punde alifika mwenzao ambaye alishtuka na kuwaeleza wenzake wamefanya kosa kwani waliyempiga risasi si jambazi ambaye walikuwa wanamtafuta", alisema.

Alisema japo alitamani kutoka nje ili amsaidie ndugu yake lakini alihofu maisha yake kwani mmoja wa askari hao alionya asitoke mtu yoyote katika eneo hilo.

"Niliogopa mno, ikabidi nibaki pale pale dirishani nikifuatilia, nilihofu iwapo nisingetii amri hiyo na kutoka nje na mimi ningepigwa risasi", alisema.

Barampani alisema akiwa dirishani hapo, alimshuhudia yule askari aliyefika katika eneo la tukio hilo akichukua simu yake na kuwasiliana na wenzake ambao alitaka wawahishe gari haraka katika eneo hilo.

"Lilipofika, walimchukua marehemu wakampakiza ndani ya gari hilo na kuondoka naye, wakati huo alikuwa bado anaugulia maumivu", alisema.

Alisema baada ya muda kupita eneo hilo lilikuwa shwari akatoka nje na baadhi ya ndugu zake na kwenda kituo kidogo cha polisi Vijibweni.

"Pale tuliuliza kama walikuwa wamemfikisha hapo, askari tuliyemkuta alituambia walielekea kituo kikuu cha polisi Kigamboni, tukaenda huko", alisema.

Alisema walipofika walipokewa na baadhi ya askari waliowakuta ambao waliwaeleza ndugu yao alikuwa amepelekwa hospitali ya Vijibweni kwa matibabu.

"Tukaenda hadi huko lakini daktari mmoja alituambia hawakumpokea na kumuhudumia kwani hawakuwa na maelezo yaliyojitosheleza, tukarudi Kigamboni lakini awamu hii hatukupewa ushirikiano kama awali, tulipewa amri tusisogee katika eneo hilo", alisema.

Alisema waliwasiliana na ndugu zao kuwaeleza hali waliyoikuta akiwamo ndugu yao Daudi Gwelenza ambaye anafanya kazi katika Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).

"Tuliwataka wajaribu kupita katika Hospitali mbalimbali kumtafuta hasa Muhimbili, ndipo Gwelenza akaenda pale chumba cha kuhifadhia maiti", alisema.

Gwelenza alisema alipofika hapo alielezwa kuna mwili ambao umefikishwa na askari wa Kigamboni, aliruhusiwa kuuona ndipo akakuta ni ndugu yao huyo.

"Nilimuangalia sura nikakuta ni yeye, nikamwangalia tumboni kweli alikuwa amepigwa risasi eneo la kushoto tumboni, alikuwa na mchanga mwingi wa bahari inaonesha huenda aliburuzwa, nilisikitika mno sikuweza tena kuendelea kuangalia tena", alisema

Aliongeza "Lakini nilishangaa kwanini katika maelezo yaliyoandikwa juu ya taarifa ya marehemu hawakuandika kwamba amepigwa risasi, waliandika tu amepigwa na waliandika haijulikani jina lake, yaani kama walimuokota mahala akiwa ameuawa.

MTANZANIA lilishuhudia damu nyingi iliyoganda ikiwa katika eneo hilo pamoja na sehemu ambayo majirani walidai risasi moja ilipiga na kutoboa ukuta.

Katika eneo hilo kulipatikana maganda mawili ya risasi yenye namba 311 (10) na 10 (77).

Chanzo: Mtanzania
 
Daaaaaah! Jamaa una speed ya light kutoa comments. Naweza kubet kwamba wewe jamaa ni jobless OR ni mwajiriwa wa JF.
Sasa Kama jobless hela ya bando anapata wapi au ndiyo wapiga dili wenyewe ambao Mkuu hataki kuwasikia
 
  • Thanks
Reactions: SDG
Back
Top Bottom