Dar: Mkazi wa Manzese afikishwa Mahakama ya Kisutu kwa madai ya kukutwa na risasi 45

beth

JF-Expert Member
Aug 19, 2012
3,877
6,326
Asha Juma (44), mkazi wa Manzese Argentina jijini Dar es Salaam, amefikishwa mahakamani akikabiliwa na mashtaka mawili likiwamo la kukutwa na kumiliki risasi 45 kinyume cha Sheria.

Mshtakiwa huyo alisomewa mashtaka yake katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Augustina Mmbando.

Wakili wa Serikali, Adolph Lema, alidai kuwa shtaka la kwanza, mshtakiwa anadaiwa kuwa Mei 17, mwaka huu, katika eneo la Manzese jijini Dar es Salaam, alikutwa akimiliki risasi 29 zenye kipenyo milimita 12 kinyume cha sheria ya usimamizi wa silaha na risasi.

Katika shtaka la pili, ilidaiwa kuwa Mei 17, mwaka huu, eneo la Manzese, alikutwa akimiliki risasi 16 zenye kipenyo cha milimita 9 kinyume cha sheria ya usimamizi wa silaha na risasi.

Wakili Lema alidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo aliomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Mshtakiwa hakutakiwa kujibu chochote kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi hiyo na alirudishwa rumande kwa kuwa mashtaka yanayomkabili hayana dhamana.

Kesi hiyo iliahirishwa mpaka Agosti 26, mwaka huu itakapotajwa.
 
Back
Top Bottom