Dakika 5 - Part 2 - Ujio wa Magufuli na Udikteta wa Sheria

Mzee Mwanakijiji

Platinum Member
Mar 10, 2006
33,739
40,863
DAKIKA 5: UJIO WA MAGUFULI NA UDIKTETA WA SHERIA -

lady-justice-blindfolded_55d3389af74020f6.jpg
Na. M. M. Mwanakijiji

Mojawapo ya mambo mabaya sana kiutawala yaliyowahi kutokea nchini na ambayo yamevuruga watendaji wajuu, watumishi na wananchi wa kawaida ni dhana ya “utii wa sheria bila shurti”. Sijui ni ‘genius’ gani alikuja na wazo hili na sijui alikuwa anamaanisha nini lakini kwa muda sasa vyombo vya utawala na usimamisi wa sheria (kama Polisi n.k) vimekuwa vikisisitiza wananchi “watii sheria bila shurti”. Kimsingi wanachosema na ambacho wamejaribu kukitangaza sana – kwenye luninga, radio na mabango yasiyohesabika ni kuwa wananchi wanapaswa kutii sheria kwa hiari; yaani, bila shurti.

Wazo hili na dhana hii ni muflisi, haina msingi katika filosofia ya sheria na haina mantiki katika nchi ya kidemokrasia au ile inayojaribu kujenga demokrasia kama nchi yetu. Tatizo la msingi na kubwa la dhana hii potofu ni kuirahisisha Sheria (nimetumia herufi kubwa hapa kumaanisha ujumla wote wa sheria – Katiba na sheria zinazotokana nayo) na kuifanya kuwa ni kitu cha uamuzi wa mtu mmoja mmoja tu. Kwamba mtu ana hiari na halazimishwi kuitii sheria yenyewe isipokuwa kwa kuamua tu – kuitii bila shurti.

Matokeo ya kukubalika kwa fikra hizi ni kuwa watu wamechukulia sheria kama kitu cha kuchagua (optional). Kwamba wanaweza wakatii au wasitii; kwamba wasipotii basi lolote na liwe na wakitii basi watii bila kujisikia kulazimika kutii (bila shurti). Hivyo, sheria inavyosema watu wafuate utaratibu fulani mtu anajisikia kama ana hiari ya kukubali au la; sheria inaposema “usifanye hili” au “fanya hili” mtu anajiona kana kwamba ana hiari; halazimiki. Kiongozi ambaye ana madaraka fulani ya kisheria basi na yeye anajisikia ana hiari ya kutumia madaraka yale au la; chombo cha umma kinapotakiwa kutekeleza jambo fulani watendaji wake wanafikiria labda hilo ni “pendekezo” (suggestion) tu iliyomo kwenye sheria na siyo takwa (demand).

Ndugu zangu, kwa muda mrefu sasa Watanzania wameishi katika fikra hizi, wamezizoea, wamezikumbatia na wengine wameona kama ndivyo inavyopaswa kuwa. Sheria ikapoteza nguvu zake, matakwa ya Katiba yakawa kama mapendekezo, na yale ambayo sheria inasema yanapaswa kufanyika yamechukuliwa kama usumbufu wa aina fulani hivi! Ndivyo tulivyokuwa tumefika na utaona kilio cha “utawala wa sheria” na “uongozi bora” msingi wake ni kuwa watu wanaonekana ama hawatii sheria au hawataki kutii sheria; hawajui kuwa watu wameambiwa sheria au kutii sheria ni hiari!

Hili linaelekea kubadilika sasa baada ya ujio wa Rais John P. Magufuli. Magufuli anawasumbua watu wengi kiasi kwamba wapo ambao kutokana na kulewa nadharia ya “utii wa sheria bila shurti” wanaona kana kwamba Magufuli anawalazimisha kufuata sheria na wengine wanabakia kujiuliza kama yeye mwenyewe Magufuli anatii sheria au anafuata sheria. Matokeo yake wale wanaotatizika namna hiyo wamefikia kumuona Magufuli kuwa kiongozi mkali, havumilii “makosa madogo madogo” na kuwa anaonesha sifa na hulka za kidikteta!

Ndugu zangu, Magufuli anaipeleka Tanzania kama nchi ya kidemokrasia kwenye alama kuu ya demokrasia ya kweli – utawala wa sheria! Kimsingi, anchofanya Magufuli na wachache wetu tunakiona na tunakishangilia ni kuleta udikteta wa sheria (the dictatorship of the law). Kwamba, katika nchi ya kidemokrasia kama ya kwetu – sheria ndiyo mtawala pekee wa kiimla; anayepaswa kuogopwa , kutiiwa na kulindwa kwa nguvu zote.

Wahenga walisema msemo wa “sheria ni msumeno”. Neno hili kimsingi walikuwa wanataka tuone na kukubali kuwa sheria inakata popote na potepote; inakata ikienda, inakata ikirudi bila kujali nani anayekatwa! Wenzetu wa nchi za Magharibi na sisi tumepokea hivyo wanaionesha sheria kama mama mwenye upanga mkali na mizani ambaye amefumbwa macho (blindfolded lady justice). Wao wanasema sheria haitazami; kwamba mbele yake wote wako sawa; watapimwa (kwenye mizani) na kuamuliwa (kwa upanga).

Mojawapo ya mambo ambayo yanawatatiza watu ni je Magufuli anatumia madaraka yake vizuri? Je Magufuli anavyowawajibisha watumishi mbalimbali tena bila hata kufikiria mara mbili anapata nguvu wapi? Je anautumia Urais vibaya? Ndugu zangu, wenye kuhoji haya ni watu waliodeka na kuzoea nadharia muflisi ya “kutii sheria bila shurti”. Ndugu zetu hawa bado wanaishi katika ile “jana” niliyoisema miezi kadhaa nyuma. Bado wanafikiria Tanzania inaweza kuendelea na kupiga hatua ya haraka ya maendeleo huku watu wake wakiangalia sheria kama kadi ya mwaliko wa harusi! Waende ama wasiende!

Katika vitu ambavyo Katiba imeviweka mikononi mwa Rais peke yake – yaani prerogatives of the President - kuna kitu kimoja ambacho wengi hawataki kukiangalia au hata kukifikiria maana yake na hasa utekelezaji wake kama atapatikana Rais atakeyekitumia kitu hicho. Ibara ya 35 na 36 za Katiba ya Jamhuri ya Muungano zinavipengele ambavyo mtu yeyote aliyewajibishwa na Rais Magufuli miezi hii michache akienda mahakamani kuchallenge atashindwa!

Lakini hasa Ibara ya 36 ambayo inahusiana na “Mamlaka ya kuanzisha na kuwateua watu wa kushika

nafasi za madaraka”; inaweka madaraka makubwa ndani ya mikono ya Rais, madaraka ambayo yanamruhusu kusimamia “nidhamu” katika utumishi na watumishi wa Jamhuri ya Muungano. Ibara hiyo ina vifungu vidogo 4. Kifungu kidogo cha 2 kinampa madaraka Rais ya kuteua watumishi na watendaji mbalimbali wa idara na taasisi mbalimbali za serikali katika nafasi ambazo anatakiwa kuzijaza kwa mujibu wa Katiba au sheria fulani. Na kifungu kidogo cha 3 kinaeleza tu kuwa watumishi na watendaji wengine mbalimbali wataajiriwa, kupandishwa vyeo hata kufukuzwa chini ya Tume husika za utumishi.


Hata hivyo ni kile kilichomo kwenye kifungu kidogo cha 4 ambacho binafsi naona watu wengi siyo tu kwamba hawakijui bali kama wanakijua wanakipuuzia maana (implication) yake katika kusimamia nidhamu. Katiba inasema hivi katika kifungu hicho “Masharti ya ibara ndogo ya (2) na ya (3) hayatahesabiwa kuwa yanamzuia Rais kuchukua hatua za kudhibiti nidhamu ya watumishi na utumishi katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano.”


Kwa ufupi, Rais ana uwezo na madaraka makubwa ya kusimamia nidhamu za watumishi wa umma katika Serikali ya Jamhuri ya Muungano kiasi kwamba inaweza kuchukuliwa kuwa ana uwezo wa kumwajibisha mtu yeyote katika utumishi wa umma isipokuwa pale ambapo Katiba inakataza.


Ndugu zangu, madaraka haya ya Rais hayajatumiwa vizuri sana huko nyuma kiasi kwamba tulikubali na kuamini kuwa Rais ni “dhaifu”. Udhaifu wa mtu ukachukuliwa kama ni udhaifu wa taasisi! Na katika udhaifu huo wapo watu kati yetu wakazoea na kubweteka wakiamini kuwa ndivyo mambo yanavyopaswa kuwa.


Magufuli anapoingia na kuanza kutumia madaraka haya ya kusimamia nidhamu hata kwa watu wanaoonekana wangesimamiwa na watu wengine anafanya kile kilicho mikononi mwake, na kile ambacho anaamini kwa maslahi ya Taifa.


Magufuli siyo Dikteta, na wala hana mfanano wa dikteta; Dikteta ni mtu ambaye anaamini yeye ndiyo sheria; Magufuli aliapa kuilinda na kuitetea Katiba hii – pamoja na madhaifu yake yote kama wabunge wote na viongozi wa juu wengine walivyoapa. Binafsi ningetarajia wale wote walioapa kuitetea Katiba hii watasimama kuanzia sasa na kutetea madaraka ya Rais ambayo wao waliapa kuyalinda! Wasimame kutetea uwezo wake wa Kikatiba kusimamia nidhamu badala ya kuuhoji!


Kama wanaona hawawezi kutetea kile kiapo chao wao wenyewe jambo pekee wanaloweza kufanya wakimaanisha kuwa hawako tayari kubariki au kuunga mkono Rais kusimamia nidhamu kama Katiba inavyotaka ni wao wenyewe kujiuzulu kwanza ili waje watumishi wengine ambao watakuwa tayari kumaanisha kile kiapo chao!


Kutii Sheria bila shurti kumefikia mwisho; kwani Sheria kwa asili yake ni shurti (ni lazima). Na tunataka viongozi ambao watasimamia sheria hata kama inauma ndugu zao, familia zao, jamaa zao, au marafiki zako. Magufuli anaonesha kutii Katiba zaidi kuliko hisia na vionjo vyake! Ndiye Rais Watanzania walimtaka na kumtarajia.


Tutaendelea kesho InShaaAllah. – Zama Mpya – OZ Inaendelea…
 
Wenje alimlipuwa bungeni Marehemu Kabwe(RIB),na kumbukumbu Zipo,Mnyika alimponda JK nadharani kuwa ni dhaifu.....mara kadhaa wabunge wa upinzani wamekosoa serikali hadi kuwajibishwa kwa mawaziri hadharani.Leo Rais akichukuwa hatua kwa tuhuma za wazi utasikia ...ohhhh ohh hajafata sheria,..ohhh serikali italipa fidia...ohhhh amekurupuka.Hizi ni dalili za mwisho kabla ya kufilisika kisiasa.
 
Mara ngapi watumishi wamepeleka serikali mahakamani na wakashinda?unawakumbuka wale maafisa wa polisi waliotimuliwa na mkapa? Mahakama ikaamuru warudishwe kazini na wakalipwa milioni sabini kila mmoja kama fidia? Ukisoma katiba unajua umemaliza? Hujui katiba inatoa general guidelines lakini baadae kuna sheria zinazotoa procedures? Hujui kwamba mahakama zimeshatoa tafsiri ya neno "maslahi ya umma" na haijumuishi matakwa binafsi ya rais yasiyo na mashiko?anayepima maslahi ya umma ni nani? Usivamie usiyoyajua,,katiba hiyo hiyo ina haki tele za mtumishi na raia wa tanzania a
 
Kama rais ndio mila kitu kwenye utumishi mbona yule askari aliyemkamata Mke wa mahalu hajapanda cheo mpaka Leo?IGP kasema mpaka taratibu za jeshi zifuatwe,mbona katibu tawala mkoa wa mwanza aliyegombana na mulongo bado yuko kazini makao makuu(inavyosemekana) ?
 
Watu wanazungumzia mifumo ya uongozi lakini ukichunguza utagundua hawa ni wale walioshazoeshwa maisha ya uhuru uliopitiliza. Walizoea kudai haki bila ya kukumbushwa umuhimu wa wao kutimiza wajibu wao.

Na malalamiko mengi ya wanaosema rais anafanya maigizo ni kielelezo cha watu kuzoea uongozi wa juu uliokuwa tayari kuwachekea, hivyo bado hawajagundua kuwa uzembe wao uliokuwa ukivumiliwa ni adui wa taifa zima na sio wao tu.

Hatuwezi kufanana na nchi zilizopiga hatua bila ya kwanza kuyajua majukumu yetu na kuwa tayari kukuza ufanisi ili uendane na umuhimu wa majukumu hayo kwenye mustakabali wa taifa zima.
 
MM I like your reasoning. By the way wengi wetu tumeshasahau kwamba kutofautiana kiitikadi si uadui. Of late kuna mengi sikubaliani na wewe kama kufungia bunge lisionekane. Lakini haina maana kwamba siheshimu michango yako-hata ambayo sikubaliani nayo. I do.

Lakini MM labda nikuulize, how sustainable are these changes Magufuli is pushing? I mean the man has good intentions for sure. Most of us who are critical we are simply, doing it kwa sababu he is doing unthinkable. The President is trying rather hard to challenge the status quo. Na wanaoumia ni wale wale beneficiaries. Who are the upper and middle class citizens in our Republic. Lakini je unless, utwambie Plan B, haya mabadiliko ya Magufuli yako kiuhalisia namna gani? To me naona Mkuu wa nchi anapambana kama jeshi la mtu mmoja. I wish kama angejitahidi, sambamba na anayoyafanya, kutuwekea misingi ambayo italinda taifa na viongozi wabovu, wala rushwa nk. Tukianza na Katiba. Kwangu mimi kama ulivyoelezea vizuri, sheria haina budi kuheshimiwa na WOTE. lakini ni vema tuweke mazingira kuonyesha kwamba atakayekwenda kinyume na sheria ataadhibiwa. Tunahitaji hii kasi for the next fifty/hundred years. How do we ensure that happens?

In all, I am one of those who still believes that Tanzania needed Magufuli. Anafanya exactly yale ambayo tulikuwa tunayalilia humu (I wish watu wangefungua threads humu za 2010-15 dhidi ya JK na serikali yake). Sasa leo kutwambia tunatamani utawala wa JK it is an insult to our collective intelligence. To me bado naamini kabisa kwa dhati, Magufuli is the REAL DEAL for Tanzania.
 
... Leo Rais akichukuwa hatua kwa tuhuma za wazi utasikia ...ohhhh ohh hajafata sheria,...
Mimi naomba ufafanuzi wa 'tuhuma' na 'tuhuma za wazi', na ni mamlaka gani inayotakiwa kisheria kuthibitisha tuhuma kuwa sasa ni za kweli au hazina ushahidi. Kama kisheria kuna mamlaka ya kutoa adhabu kwa tuhuma au tuhuma za wazi, naona litakuwa ni jambo jema maana itasaidia kupunguza mlundikano wa mahabusu kwenye magereza wenye tuhuma mbalimbali
 
I wish kama angejitahidi, sambamba na anayoyafanya, kutuwekea misingi ambayo italinda taifa na viongozi wabovu, wala rushwa nk. Tukianza na Katiba. Kwangu mimi kama ulivyoelezea vizuri, sheria haina budi kuheshimiwa na WOTE. lakini ni vema tuweke mazingira kuonyesha kwamba atakayekwenda kinyume na sheria ataadhibiwa. Tunahitaji hii kasi for the next fifty/hundred years. How do we ensure that happens?

Magufuli anafanya vitu vya kwanza kwanza; na kitu cha kwanza ni kushock the system. Na bado kidogo anahitaji kufanya hili; baada ya kufanya mabadiliko ya baraza la mawaziri tutaanza kuona sasa msisitizo unatoka kwenye watu na kuelekea kwenye vyombo mbalimbali vya kiutendaji.

Usikate tamaa.
 
Watu wanazungumzia mifumo ya uongozi lakini ukichunguza utagundua hawa ni wale walioshazoeshwa maisha ya uhuru uliopitiliza. Walizoea kudai haki bila ya kukumbushwa umuhimu wa wao kutimiza wajibu wao.

Kuna watu zamani mtaani kwangu walikuwa wanataka iwekwe taa ya nje kumulika eneo letu sababu ya vibaka n.k TANESCO wakaja na kufunga milingoti miwili ya taa; kwa hiyo kulikuwa na mwanga mzuri tu. Haikuchukua muda watu wakaanza kuzipopoa zile taa na baada ya kutengeneza mara kwa mara TANESCO wakaachana nazo. Kumbe siyo wote walikuwa wanataka zile taa; wengine taa zile zilikuwa ni mwisho wa wao kupata riziki "zao". Wapo watu kati yetu walizoea uongozi mbaya kiasi kwamba wameanza kuumiss! go figure that.
 
Kuna watu zamani mtaani kwangu walikuwa wanataka iwekwe taa ya nje kumulika eneo letu sababu ya vibaka n.k TANESCO wakaja na kufunga milingoti miwili ya taa; kwa hiyo kulikuwa na mwanga mzuri tu. Haikuchukua muda watu wakaanza kuzipopoa zile taa na baada ya kutengeneza mara kwa mara TANESCO wakaachana nazo. Kumbe siyo wote walikuwa wanataka zile taa; wengine taa zile zilikuwa ni mwisho wa wao kupata riziki "zao". Wapo watu kati yetu walizoea uongozi mbaya kiasi kwamba wameanza kuumiss! go figure that.
Mtaa ulikuwa unatawaliwa na genge la wahuni kiasi cha kuonekana ni utamaduni wa mtaa huo.
 
Hakika MM ni hazina kubwa sana ya Taifa hili. Labda tu watu wabaki kushupaza shingo zao. lakini sisi tunaona direction ya hii nchi. Magufuli anafanya kama Kiongozi.
Kuna hazina za aina nyingi,nyingine hazina thamani,au ilikuwepo ikaisha,hii unayoisema.naifananisha hazina ya mafuta yaliyo expire
 
Back
Top Bottom