CWT yachochea walimu wakimbie vituo vya kazi

kilimasera

JF-Expert Member
Dec 2, 2009
3,068
268
CHAMA cha Walimu Tanzania (CWT), kimewachochea walimu wapya walioajiriwa hivi karibuni, warejee makwao iwapo Serikali itaendelea kuwazungusha kuwalipa fedha za kujikimu pamoja na mishahara.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Rais wa (CWT), Gratian Mukoba alisema wamepokea taarifa za malalamiko kutoka halmashauri mbalimbali nchini kwamba walimu walioajiriwa Februari mwaka huu, hadi sasa hawajapata fedha za kujikimu pamoja na mishahara.

“Sioni sababu ya walimu kuendelea kuteseka na kuwa ombaomba wakati wapo kazini. Kama Serikali imeshindwa kuwalipa fedha zao za kujikimu pamoja na mishahara wanatakiwa kurudi nyumbani kwao hadi itakapopata fedha ndipo iwaite tena kazini,” alisema Mukoba.

Mukoba alisema kama hali itaendelea hivyo hadi mwisho wa mwezi huu, CWT kitalazimika kuchukua hatua za kuhakikisha walimu wote wanarudi nyumbani ili kuwaepusha na hali ya kuwatia majaribuni kutokana na kuishi katika mazingira magumu.

“Napenda kuwaambia walimu ambao wataweza kuvumilia hali hii hadi mwisho wa mwezi huu na kuona hakuna mabadiliko, nao wanatakiwa kurudi kwao hadi pale Serikali itakapopata fedha. Hebu fikiria mwalimu hana sehemu ya kulala, chakula nacho shida; halafu ananyimwa fedha zake. Unategemea nini?” Alihoji Mukoba.

Alisema kitendo cha kuwalipa fedha za kujikimu za siku tatu badala ya malipo ya siku saba ni ukiukwaji wa sheria za kazi na unyanyasaji wa watumishi jambo ambalo CWT haitalivumilia.

Mukoba alisema malalamiko mengine ni ya fedha za madai ya walimu ambayo yalihakikiwa na Serikali kati ya Novemba na Desemba lakini ulipaji umegubikwa na utata.

“Kwa kweli unyanyasaji wa walimu umekithiri sana maana hata walimu waliopo kazini kwa muda mrefu, fedha za madai ya zamani yaliyohakikiwa na Serikali bado ulipaji wake ni utata mtupu. Walimu wanazungushwa na kunyimwa fedha hizo lakini kwa sasa tunafikia hatua ya mwisho ya kuchukua,” alisema Mukoba.

Kilio Kwimba
Taarifa kutoka wilayani Kwimba, Mwanza zinaeleza kuwa walimu walioripoti mpaka sasa hawajalipwa fedha za kujikimu pamoja na mishahara.

Mmoja wa walimu hao aliyelipigia simu katika ofisi za gazeti hili alisema hivi sasa wana hali ngumu kwani walipewa fedha za kujikimu kwa siku tatu tu tangu Februari 2 na hadi sasa wanaishi kwa kuombaomba.

“Hapa tulipo hatuna fedha ya kula hata sehemu ya kulala. Tatizo jingine ni kwamba hata uwezo wa kurudi kwetu hatuna maana hatuna nauli na baadhi yetu, wazazi wetu hawana uwezo wa kututumia nauli turudi nyumbani,” alisema.

Rungwe maandamano
Kutoka Rungwe mkoani Mbeya, walimu 206 wa shule za msingi na sekondari jana waliandamana hadi Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wakidai fedha zao za kujikimu, mishahara na nauli ambazo hawajalipwa tangu walipoajiriwa mwanzoni mwa mwezi uliopita.

Wakizungumza mbele ya ofisi hizo, walimu hao walisema tangu waajiriwe walilipwa, fedha za kujikimu za siku tatu tu badala ya saba na kwamba wamekuwa wakinyanyasika katika vituo vyao vya kazi.

Mmoja wao, Lucy Mpakati alisema wakati wanaripoti waliahidiwa kwamba fedha zote zitakuwa zimelipwa mwishoni mwa Februari lakini matokeo yake wanajikuta wanapigwa kalenda na mkurugenzi wa halmashauri.

Naye, Baraka Nguvumali alisema wakati wanajaza mikataba ya ajira, hapakuwa na mizengwe kama ilivyojitokeza kwenye stahiki zao ambazo wamekuwa wakijibiwa kwa lugha mbaya zinazowavunja moyo wa kutenda kazi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya ya Rungwe, Noel Mahyenga alikataa katakata kuzungumza na waandishi wa habari kuhusiana na madai ya walimu hao.

Muheza siku tatu
Walimu wapya wapatao 100 wa sekondari waliopangwa kufanya kazi wilayani Muheza wameandamana hadi Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri na kuipa Serikali siku tatu kuhakikisha inawalipa fedha zao za kujikimu pamoja na mishahara la sivyo Jumatatu watagoma.

Walitoa kauli hiyo jana na kudai kwamba ikifika keshokutwa bila kupewa malipo hayo, watagoma kufanya kazi kwa kuwa hali zao hivi sasa ni mbaya.Walimu hao ambao waliomba majina yao yasitajwe walisema mpaka sasa wanadai fedha za mizigo, nauli na za kujikimu na mpaka sasa hawajalipwa licha ya kuwa wameshaanza kazi.

Imeandikwa na Gedius Rwiza, Amanyisye Ambindwile,Tukuyu na Steven William, Muheza
 
Back
Top Bottom