MarkoMAANDAMANO yaliyokuwa yafanywe jana na Wanachama wa CUF, yaliahirishwa baada ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kuwaomba wasitishe kama walivyoambiwa na Jeshi la Polisi kutokana na ugeni wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Hillary Clinton.
Cliton ambaye aliwasili nchini juzi kwa ziara ya siku tatu, jana alitembelea mitambo ya kuzalisha Umeme ya Symbion iliyopo Ubungo Dar es Salaam ambapo ndipo maandamano ya CUF yalitakiwa kuanzia na kumalizikia Manzese Bakhresa.
Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Julius Mtatiro aliliambia gazeti hili jana kuwa waliahirisha maandamano hayo kutokana na ombi la Waziri Pinda kupitia Mwenyekiti wa Chama hicho, Profesa Ibrahimu Lipumba ambalo alimtaka asitishe maandamano kutokana na ugeni uliopo.
Mtatiro alisema jana kwamba Profesa Lipumba alipokea barua kutoka kwa Pinda iliyoitaka CUF kusitisha maandamano hayo kwa sababu maeneo yalipotakiwa kuanzia ni moja ya sehemu ambazo mgeni huyo angetembelea.
Alisema Pinda aliwataka kusitisha maandamano hayo kwa sababu za kiusalama kwa kiongozi huyo wa Marekani."Busara za uongozi wa Waziri Mkuu zilitumika, wakatuambia kuwa maeneo ambayo tungefanyia maandamano hayo ndiko msafara wa kiongozi huyo ungepita kwa hiyo viongozi waandamizi wa CUF tulikaa pamoja na kukubaliana tuyaahirishe,"alisema na kuongeza kuwa;"Pinda alitushauri na kutueleza kuwa kama sisi tungekuwa ndiyo viongozi wa nchi halafu kuna ujio wa kiongozi mkubwa kama huyo anayekuja akakuta maandamano ingekuwaje?
Tulimuelewa na ndio maana tumeahirisha."Hata hivyo Mtatiro alilishutumu Jeshi la Polisi kutokuwa wawazi kwa kudai kuwa walikataa maandamano hayo kwa sababu za kiusalama bila kueleza kuwa Clinton atafanya ziara katika maeneo ambayo yatakuwapo maandamano.
"Baada ya ufafanuzi huo wa barua ya Waziri Pinda tulikaa kikao na viongozi waandamizi wa chama tukajadili na kuona ni vema tukaahirisha ili hata msafara wa Clinton ukipata tatizo tusilaumiwe," alisema Mtatiro.
Pia alisema baada ya kuondoka kwa kiongozi huyo wa Marekani, CUF itakaa kikao na viongozi waandamizi wa chama hicho ili kupanga siku ambayo watafanya maandamano. Juni 6 mwaka huu, CUF ilitangaza kufanya maandamano makubwa ambayo yangefanyika jana kuanzia Ubungo hadi Bakhresa Mazense kwa lengo la kupinga mauaji yanayofanywa na polisi dhidi ya raia nchini.
Lakini kulikuwa na mvutano mkubwa baina yao na polisi ambao waliwataka CUF kutofanya maandamano lakini walisisitiza kuendelea na msimamo wao wakidai kuwa Clinton si kiongozi wao, bali ni Mmarekani hivyo hawezi kuzuia maandamano hayo yanayodai haki za Watanzania.
Akitolea mfano Tamko la Umoja wa Mataifa la Haki za Binadamu (UDHR) la mwaka 1945 linatoa haki ya kuandamana ikiwa watu au chama kinataka kuonyesha hisia zake kwa jamii na kwamba Tanzania ni mjumbe wa umoja huo na imeridhia.
"Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977 ambayo tayari ina viraka zaidi ya 14 inatoa haki kwa raia wa Tanzania, vikundi au taasisi kutoa mawazo au hisia zao na hii iko kifungu ch 1 ibara ya 20,"alisema.
Aidha Mtatiro alisema kifungu cha 43(3) kinaeleza kuwa Ofisa wa Polisi hawezi kukataza maandamano chini ya kifungu cha 43 (2), isipokuwa iwapo atajiridhisha kuwa mkusanyiko huo utasababisha uvunjifu wa amani au utaathiri usalama wa nchi.
Alisema maandamano yatakayofanywa na CUF yatakuwa ya amani na kwamba hayatakuwa na silaha za moto isipokuwa watabeba mabango na kufikisha ujumbe walioukusudia kwa wananchi."Kwa mantiki hiyo kukataza maandamano bila polisi kusema yatavuruga vipi amani ni uzembe wa dhahiri na kamwe chama hakiwezi kusitisha maandamano kwa kutekeleza uzembe,"alisema.