CUF: Ruksa mwanachama yeyote kumkabili Profesa Lipumba | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

CUF: Ruksa mwanachama yeyote kumkabili Profesa Lipumba

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by MziziMkavu, May 13, 2010.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  May 13, 2010
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,616
  Trophy Points: 280
  Uteuzi wa wagombea urais Bara, Visiwani kujulikana mwezi ujao
  [​IMG]
  Mwenyekiti wa chama CUF, Profesa Ibrahim Lipumba.  Chama Cha Wananchi (CUF), kimesema ni ruksa kwa wanachama wengine kumkabili Mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba katika kinyang'anyiro cha Urais kwenye uchaguzi mkuu wa Oktoba, mwaka huu.
  Aidha, CUF pia kimetangaza kuwa uteuzi wa wagombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa tiketi ya chama hicho utafanyika mwezi ujao.
  Hatua hiyo imetangazwa ikiwa ni siku moja baada ya Mwenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba, kutangaza nia ya kuwania Urais wa Muungano.
  Ratiba ya uteuzi wa wagombea wa nafasi hizo ilitangazwa jana na Profesa Lipumba, alipokuwa akisoma maazimio 27 yaliyofikiwa na Baraza Kuu la Uongozi Taifa, baada ya kikao chake cha kawaida kilichofanyika jijini Dar es Salaam juzi.
  Maazimio hayo ni matokeo ya ajenda saba zilizojadiliwa ikiwemo maandalizi ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2010.
  Nyingine ni taarifa ya uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura Tanzania Bara na Zanzibar, ratiba ya uendeshaji wa kura za maoni kuwapata wagombea wa CUF, maandalizi ya Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa na halali ya kisiasa nchini.
  Profesa Lipumba alisema Baraza Kuu limeridhika na maandalizi ya Mkutano Mkuu Maalum wa Taifa wa CUF uliopangwa kufanyika Juni mwaka huu kwa ajili ya uteuzi wa wagombea Urais kupitia chama hicho.
  Alisema Baraza Kuu limeitaka kamati ya utendaji ya chama hico, kuhakikisha kuwa hatua muhimu zinachukuliwa ili kufanikisha mkutano huo. “Baraza limempongeza Mwenyekiti wa Chama Taifa, Mheshimiwa Profesa Ibrahim Lipumba, kwa kuamua kuwa miongoni mwa wanachama watakaogombea nafasi ya urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba mwaka huu kwa lengo la kuwapatia Watanzania uongozi makini chini ya chama mbadala na makini hapa nchini-Chama Cha Wananchi (CUF),” alisema na kuongeza:
  “Baraza Kuu linatoa wito kwa wanachama wengine wa CUF wenye sifa na uwezo kujitokeza kutangaza nia na kuchukua fomu za kugombea nafasi hiyo ya urais wa Jamhuri ya Muungano, urais wa Zanzibar na nafasi nyingine zote.”
  Aidha, alisema katika kufikia hatima njema ya maridhiano hayo, Baraza Kuu linaitaka Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kurekebisha mapungufu makubwa yaliyojitokeza katika zoezi la uandikishaji wapigakura katika Daftari la Kudumu la Wapigakura (DKWK) visiwani humo.
  Alisema hadi sasa katika majimbo yaliyokusanywa takwimu tu, zaidi ya Wazanzibari 15,000 wenye haki ya kuandikishwa katika DKWK, wamenyimwa haki yao hiyo ya kikatiba na kusema kuwa hali hiyo inathibitisha kuwa kuna wananchi wengi zaidi, katika majimbo, ambayo takwimu hazijakusanywa, ambao wamekosa haki zao za kujiandikisha.
  Kutokana na hali hiyo, alisema Baraza Kuu linasisitiza haja na wajibu wa ZEC na serikali, hasa Idara ya Usajili wa Vitambulisho vya Uzanzibari, kutokuwa chanzo cha kuvuruga dhamira njema ya maridhiano yaliyofikiwa na wahakikishe wanatimiza na kutekeleza kwa vitendo agizo la Rais wa Zanzibar, Amani Abeid Karume la kutaka wananchi wote wenye haki ya kujiandikisha kwa mujibu wa katiba, wapatiwe haki yao hiyo.
  Alisema pia, Baraza Kuu limesikitishwa sana na matokeo mabaya ya kiwango cha kufaulu mitihani ya Kidato cha Sita kwa mwaka huu, hali ambayo inaendeleza hali ya kuporomoka kwa kiwango cha elimu hapa nchini.
  Profesa Lipumba alisema tatizo hilo linasababishwa na serikali kutokuwa na sera makini za uendelezaji wa sekta ya elimu. Alisema hali hiyo kwa kiasi kikubwa imetokana na serikali ya CCM kuchukua sera ya CUF ya kujenga shule za sekondari kwa kila kata, lakini ikashindwa kuisimamia ipasavyo kama ilivyokuwa imekusudiwa na chama hicho (CUF).
  Alisema Baraza Kuu pia linalaani tabia iliyoanza kujengeka tena ya Jeshi la Polisi kutumika vibaya kwa kuwakamata na kuwabambikizia kesi za kubuni viongozi na wanachama 138 wa CUF katika sehemu mbalimbali za nchi ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuendesha vitisho ili kutimiza kauli mbiu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya “Ushindi ni lazima 2010”.
  Kutokana na hali hiyo, alisema Baraza Kuu linalitaka jeshi hilo kuacha kutumiwa na CCM na kuiacha demokrasia ichukue mkondo wake na wananchi wafanye maamuzi yao kwa uhuru bila ya vitisho au hujuma.
  Pia, linalaani matumizi ya nguvu kubwa ya polisi hadi kutumia risasi za moto dhidi ya wananchi wa Kata ya Mgusu, wilayani Geita waliokuwa wakiandamana kuitaka serikali kuufungua mgodi wa dhahabu wa Mgusu ambao umekuwa ukitumiwa na wachimbaji wadogowadogo na ambao umeendelea kufungwa kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa licha ya Waziri Mkuu kuahidi kwamba ungefunguliwa ndani ya kipindi cha miezi mitatu.
  Alisema pamoja na kutambua umuhimu na mchango wa wawekezaji wakubwa wa nje katika ukuzaji wa uchumi wa nchi, Baraza Kuu linasisitiza hilo lisiwe sababu ya kuwanyanyasa wachimbaji wadogo wa Tanzania ambao ndiyo wanaopaswa kunufaika kwanza na rasilimali za nchi yao.
  Profesa Lipumba pia alisema Baraza Kuu linawapa pole Watanzania kutokana na kupanda kwa gharama ya maisha kila uchao kutokana na kutowajibika ipasavyo kwa serikali kunakotokana na kuwapo kwa ombwe kubwa la uongozi lililomo nchini.
  Aliitaka serikali kuacha kutoa ahadi zisizotekelezwa za kudai kuongeza ajira kwa wananchi, hasa vijana, huku taarifa ya Benki ya Dunia ikionesha kuwa katika kila watu 100 wanaoajirika nchini, 89 wana ajira za mashaka na wasiwasi.
  Alilaumu serikali kwa kukosa vipaumbele katika kupanga mikakati na mbinu bora za kukabiliana na hali mbaya ya uchumi na umaskini wa Watanzania uliokithiri kwa kutumia fedha nyingi kuwa mwenyeji na kuendesha Mkutano wa Hali ya Uchumi Duniani badala ya kwanza kuandaa Mkutano wa Kujadili Namna ya Kuinua Uchumi wa Tanzania.
  Alisema Baraza Kuu pia, limesikitishwa na matokeo mabaya ya kiwango cha kufaulu mitihani ya Kidato cha Sita kwa mwaka huu na hivyo kuendeleza hali ya kuporomoka kwa kiwango cha elimu nchini kunakosababishwa na serikali kutokuwa na sera makini za uendelezaji wa sekta ya elimu.
  Alisema Baraza Kuu linatanabahisha kwamba kutokana na hali hiyo, Tanzania itaendelea kubaki katika hofu ya kuzidiwa na majirani zake pale inapofungua milango ya Soko la Pamoja la Afrika Mashariki ambalo linajumuisha pia soko la ajira.
  Alisema pia Baraza Kuu limeshangazwa na hali ya kuwa licha ya kutangaza mradi wa ‘Kilimo Kwanza’ na kutambua kuwa kilimo ndio uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania, serikali imeshindwa kuisimamia kauli mbiu hiyo kivitendo na kuwa na sera makini na hatua madhubuti za utekelezaji wa sera hizo na badala yake inaendeleza hadithi za kusadikika.
  Alisema katika maazimio hayo, Baraza Kuu linaitaka serikali kuacha kuwadhulumu wakulima kupitia mfumo wake wa manunuzi wa mazao ya wakulima hasa wale wa mikoa ya kusini na Kanda ya Ziwa uitwao “Stakabadhi Ghalani”, ambao umepelekea kuwalipa bei ndogo isiyolingana na bei ya soko na kuwalipa kwa awamu sera ambazo alisema zinawakatisha tamaa na kuwavunja moyo wakulima maskini.
  Alilipongeza Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kupitisha Sheria mpya ya Madini, hatua iliyotokana na madai ya muda mrefu ya Kambi ya Upinzani Bungeni ya kutaka kutungwa sheria hiyo na kusema linaamini sheria hiyo itapelekea Tanzania na Watanzania kunufaika zaidi na rasilimali za madini zilizomo nchini na kuhakikisha kuwa nchi inapata faida za kiuchumi kwa kuunganisha sekta hiyo ya madini na sekta nyengine za kiuchumi.
  Limempongeza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na Ofisi yake kwa kazi nzuri ya kuchunga fedha za walipa kodi wa Tanzania na kubainisha mabilioni ya fedha za Watanzania yanayopotea kutokana na usimamizi mbovu na matumizi ya ovyo na kifisadi ya Serikali ya CCM na kuitaka serikali kutekeleza mapendekezo yote ya CAG yakiwemo yale ya kupitia upya sera ya misamaha ya kodi na uwekaji wa dhamana za mikopo.
  Pia, linaunga mkono madai ya msingi yaliyotolewa na wafanyakazi kupitia Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi nchini (Tucta) wanaotaka serikali kuboresha mishahara yao pamoja na maslahi yao kwa ujumla.
  Vilevile, limepongeza Baraza la Wawakilishi Zanzibar kwa kupitisha kwa kauli moja Sheria ya Kura ya Maoni na linawaomba Wazanzibari wote kutumia nafasi hii ya kura ya maoni kwa kutumia demokrasia yao kwa kupiga kura ya NDIO kuunga mkono Serikali ya Umoja wa Kitaifa na hivyo kuijenga Zanzibar mpya na kwa maslahi ya Wazanzibari wote na Watanzania kwa ujumla.  CHANZO: NIPASHE
   
Loading...