CTI, wakulima, Tucta waichambua bajeti | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

CTI, wakulima, Tucta waichambua bajeti

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by MziziMkavu, Jun 14, 2010.

 1. MziziMkavu

  MziziMkavu JF-Expert Member

  #1
  Jun 14, 2010
  Joined: Feb 3, 2009
  Messages: 39,620
  Likes Received: 4,616
  Trophy Points: 280
  [​IMG]
  Mwenyekiti wa CTI, Felix Mosha.  Shirikisho la Viwanda Nchini (CTI), limepongeza bajeti ya serikali hasa kusudio la kushushwa na kufutwa kwa baadhi ya kodi na kueleza kwamba maeneo kadhaa kama kodi ya saruji ilipaswa kuongezwa ili kulinda viwanda vya ndani.
  Mwenyekiti wa CTI, Felix Mosha, aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa eneo lingine ambalo serikali ingepaswa kuliondolea kodi ni vinywaji baridi, ushuru wa forodha kwa vifungashio vya viwanda vya dawa na kurudisha ushuru wa asilimia 10 kwa viwanda vya dawa za binadamu.
  Alisema CTI inapendekeza kuwa serikali itoze kodi kwa majengo yote badala ya sasa inavyotoza kwa watu binafsi pekee, kuondoa ushuru wa asilimia 120 kwenye mifuko ya plastiki yenye micron 30 na kuweka ‘green levy’ ya asilimia 50 na kupunguza kodi ya kuendeleza taaluma (SDL), kutoka asilimia sita hadi mbili ili kuruhusu uwekezaji wenye tija.
  Alitoa mfano kuwa kodi ya maendeleo ya taaluma ni kubwa na kwamba hiyo pekee inatosha kukwamisha uwekezaji nchini pamoja na ajira za Watanzania wengi.
  Kuhusu suala la ushuru kwa viwanda vya saruji, alisema serikali ilipaswa kupandisha hadi asilimia 35 ili kulinda viwanda vya ndani badala ya kuushusha.
  Alisema CTI iliwasilisha mapandekezo hayo serikalini mapema wakati wa maandalizi ya bajeti na kushangazwa kuona kwamba serikali haijayafanyiakazi.
  Hata hivyo, shirikisho hilo limepongeza hatua ya kuongeza bajeti ya kilimo na kufuta baadhi ya kodi kwenye zana za kilimo na kueleza kuwa hatua hiyo itasaidia kuongeza uwekezaji hasa kwenye viwanda vya kusindika mazao ya kilimo.
  Alisema CTI imefurahishwa na hatua ya serikali kuongeza bajeti ya miundombinu na kwamba hilo litasaidia kuboresha kilimo hasa usafirishaji wa mazao ya wakulima.
  Nao Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Wadogo Tanzania (Mviwata), umesema kuwa bajeti ya mwaka 2010/11 haijatoa fursa kwa mkulima mdogo ambaye anategemea utashi wa wakulima na wafugaji wakubwa, wafanyabiashara na wawekezaji wanaopewa misamaha mingi ya kodi.
  Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na vingozi wa Mviwata katika mkutano wa waandishi wa habari, wakati wakitoa maoni yao kuhusiana na mwelekeo wa bajeti hiyo katika sekta ya kilimo.
  Mwenyekiti wa Mviwata, Marcelina Kibena, alisema misamaha hiyo ipo kwenye usafirishaji wa mazao ya miwa, mkonge, chai, uagizaji mashudu na usafirishaji wa maua ambapo mkulima mdogo hanufaiki moja kwa moja.
  “Bajeti hii imedhamiria kuanzisha benki ya kilimo, lakini haikufafanuliwa ni wakulima wadogo au wakubwa… ingekuwa vyema serikali iangalie kimkakati zaidi husasani umiliki wake, msambao wake hadi vijijini na namna mkulima mdogo atakavyonufaika ingawa hakopeshiki,” alisema.
  Kwa upande wake, Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (Tucta) limesema linakubali yaishe ingawa serikali imeshindwa kutekeleza mambo waliyoyatarajia licha ya kupunguza kodi katika mishahara pamoja na kuongeza mshahara wa kima cha chini.
  Kaimu Katibu Mkuu wa Tucta, Silivester Rwegasira, alisema kiasi cha asilimia moja kilichopunguzwa katika kodi ya mishahara ni kidogo na hakiwezi kumsadia mfanyakazi.
  Alisema hata kima cha chini cha mishahara kinachotarajiwa kutangazwa na serikali kitakuwa kidogo, lakini akasema wanalazimika kukubali matokeo kwa kuwa viongozi wa vyama vya wafanyakazi walishiriki kujadili suala hilo.
  “Tunakubali hali hii ingawa hatujaridhika kwa asilimia mia moja lakini kwa kuwa tulishiriki itabidi tukubali,” alisema.

  Imeandikwa na Restuta James, Hellen Mwango na Richard Makore.
  CHANZO: NIPASHE
   
Loading...