Corona kusababisha condom kutoweka

The Sheriff

JF-Expert Member
Oct 10, 2019
613
1,776
Condoms.jpg

Kutokana na viwanda na mipaka ya nchi kufungwa, uzalishaji wa zana hizo za kujikinga unatarajiwa kushuka, huku usambazaji ukikumbana na ugumu na hivyo kusababisha upungufu mkubwa wa condom duniani

Dunia inatarajiwa kukumbana na upungufu mkubwa wa condom kutokana na mlipuko wa virusi vya corona kusababisha viwanda kufungwa, watengenezaji wa zana hizo za kujikinga wamesema, huku Umoja wa Mataifa (UN) ukionya kuwa hali hiyo inaweza kusababisha matokeo ya kutisha.

Zaidi ya nusu ya idadi ya watu duniani imejifungia majumbani wakati ugonjwa wa virusi vya corona, Covid-19, ambao unaambukiza kwa kasi, ukizidi kuizunguka dunia, huku serikali duniani zikiagiza kufungwa kwa biashara zinazoonekana kutokuwa na umuhimu.

Malaysia -- moja ya nchi zinazozalisha mpira kwa wingi duniani na mzalishaji mkubwa wa condom -- ilitangaza marufuku ya kutoka nyumbani nchi nzima wakati maambukizi yakifikia kiwango cha juu katika taifa hilo la Asia Kusinimashariki.

Lakini mazuio yaliyowekwa dhidi ya kiwanda kikubwa cha uzalishaji wa kinga hizo cha Karex, ambacho huzalisha condom moja kati ya tano zinazopatikana duniani, yanamaanisha kiwanda hicho kitatoa condom milioni 200 pungufu ya uzalishaji wa kawaida kuanzia katikati ya mwezi Machi hadi katikati ya Aprili.

Huku wazalishaji wengine duniani wakikabiliwa na uwezekano wa kuvurugwa kwa shughuli zao na ugumu wa kuzisafirisha condom hadi sokoni kutokana na matatizo ya usafiri, usambazaji wa zana hizo za kinga utakumbana na vikwazo, alionya mtendaji mkuu wa Karex, Goh Miah Kiat.

"Ni dhahiri dunia itakumbana na upungufu wa condom," Goh aliiambia AFP.
"Ni changamoto, lakini tunajaribu kila tuwezalo. Ni wazi kuwa hilo linatia wasiwasi -- condom ni zana muhimu katika tiba.

"Wakati tukipambana na ugonjwa wa Covid-19, pia kuna mambo mengine muhimu sana ambayo tunatakiwa tuyaangalie," alisema, akieleza wasiwasi wake kuhusu kupeleka condom katika nchi zinazoendelea.

Karex, ambayo husambaza condom kwa kampuni nyingi, serikali mbalimbali duniani pamoja na kusambaza kwa ajili ya programu za misaada, ililazimika kufunga viwanda vyake vitatu nchini Malaysia kwa muda mwanzoni mwa marufuku ya wananchi kutoka nyumbani na ambayo inatarajiwa kuendelea hadi Aprili 14.

Tangu wakati huo, kampuni hiyo imeruhusiwa kuendelea na shughuli zake, lakini ikitumia asilimia 50 tu ya nguvu kazi yake ya kawaida, na Goh anataka ruhusa ya kuongeza uzalishaji.

Umoja wa Mataifa pia unaonyesha ishara ya hali ya hatari, huku shirika lake linalohusika na masuala ya uzazi likionya kuwa linaweza kupata karibu asilimia 50-60 ya condom ambazo limekuwa likizipata kutokana na athari za virusi vya corona.

"Kufunga mipaka na hatua nyingine za mazuio zinaathiri usafirishaji na uzalishaji katika nchi kadhaa na kanda," alisema msemaji wa shirika la UN linalohusika na idadi ya watu, akiongeza kuwa wanachukua hatua kama kuongeza wazalishaji wengine wa condom kusaidia mahitaji makubwa ya sasa.

Mwananchi, AFP
 
Back
Top Bottom