Congo: Mwili wa Baba wa Rais wa nchi hiyo upo mochwari ikiwa ni mwaka wa pili huu

Kanungila Karim

Verified Member
Apr 29, 2016
16,636
2,000
NI MIAKA miwili sasa tangu baba mzazi wa Rais Felix Tshisekedi wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Etienne Tshisekedi wa Mulumba afariki dunia huko Brussels, Ubelgiji lakini mpaka sasa mwili wake haujarejeshwa nchini humo kwa mazishi.

Familia yake na chama chake, walituhumu kwamba rais aliyemaliza muda wake wa DRC, Joseph Kabila amezuia juhudi za kurejeshwa na kuzikwa kwa mwili wa kiongozi huyo wa kisiasa nchini.

Sasa imetimia miaka miwili, mwili wa marehemu Etienne Tshisekedi wa Mulumba umesalia ndani ya chumba cha kuhifadhi maiti huko Brussels, Ubelgiji.

Licha ya juhudi za familia yake na chama chake kutaka mwili wake urudishwe nchini Congo, serikali na chama na familia yake walikosa kuelewana kuhusu mahali pa kumzika marehemu.Etienne Tshisekedi.

Chama chake cha UPDS kilitaka azikwe katika makao makuu ya chama, lakini serikali ilikataa na badala yake awali iliagiza azikwe katika makaburi yaliopo kwenye Mtaa wa Gombe na baadaye walikubaliana azikwe katika kiwanja cha familia yake kilichokuwa mbali na mji wa Kinshasa, lakini mipango yote ilisitishwa na serikali.

Gerard Mulumba ni ndugu yake marehemu ambaye alipewa jukumu ya kuandaa mazishi ya kiongozi huyo, katika mahojiano na Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) anasema:

“Waliogopa kwamba kufika kwa mwili wake katika mji huu wa Kinshasa ambapo alikuwa anapendwa sana, kungevuruga utaratibu, walikataa kuzikwa mahali tulipokuwa tunataka sisi.

“Hata tulipoamua kwamba tutamzika nje kidogo ya Kinshasa waliendelea tu kuchelewesha mambo, bila sababu yoyote ya msingi.”Rais Felix Tshisekedi

Familia yake sasa inatumaini kwamba kupitia mtoto wake marehemu,Tshisekedi ambaye sasa ni rais wa DRC , mazishi ya kiongozi huyo mkongwe wa siasa yataandaliwa kwa heshima kubwa.

“Kuchaguliwa kwa rais wa sasa, tunatumaini kuandaa mazishi yanayofaa, familia imeshakutana na hivi kazi inaendelea, nadhani kabla ya mwisho wa Februari mwili wake utawasili nchini na kuzikwa kwa heshima kubwa,” anasema Mulumba.

Kwa mujibu wa familia ya marehemu, hadi sasa mjane, yaani mkewe marehemu Tshisekedi hajatoka nje kwa muda wa miaka miwili, hata siku alipoapishwa mwanawe Felix Tshisekedi, hakuweza kufika kushuhudia kwa kuwa ndivyo mila ya familia hiyo inavyotaka, hairuhusu mjane kusafiri au kufanya shughuli zozote wakati mwili wa mumewe haujazikwa.

Tayari Rais Felix Tshisekedi ameapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) ni wazi kwamba jukumu lake la kwanza ni kulazimika kuandaa mazishi ya kitaifa ya baba yake mzazi aliyepoteza maisha akiwa kwenye matibabu nchini Ubelgiji Februari Mosi, 2017.

Etienne Tshisekedi, alifariki dunia wakati anapatiwa matibabu mjini Brussels akiwa na umri wa miaka 84.

Tume ya Uchaguzi ya DR Congo ilimtangaza mshindi wa urais, Felix Tshisekedi na tayari ameapishwa hivi karibuni na Tanzania tuliwakishiwa na Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu.

Etienne Tchisekedi alikuwa mmoja wa wanasiasa wakongwe waliokuwa mstari wa mbele kupigania demokrasia ya nchi yake.

Alisimama kidete katika utawala wa aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo, dikteta Mobutu Sese Seko, ambaye utawala wake ulidumu kwa miongo kadhaa kabla ya kupinduliwa na Laurent Kabila.
 

Toa taarifa ya maudhui yasiyofaa!

Kuna taarifa umeiona humu JamiiForums na haifai kubaki mtandaoni?
Fanya hivi...

Umesahau Password au akaunti yako?

Unapata ugumu kuikumbuka akaunti yako? Unakwama kuanzisha akaunti?
Contact us

Top Bottom