Chuma ulete yazua songombingo Dar, Wakimbiza pesa benki kwa hofu

mwanaizaya

Senior Member
Apr 26, 2008
133
1
Chuma ulete yazua songombingo Dar, Wakimbiza pesa benki kwa hofu

*Wakimbiza pesa benki kwa hofu

Na Adam Hussein

MZOZO mkubwa huenda ukazuka kati ya baadhi ya wenye nyumba na wapangaji katika maeneo mbalimbali wilayani Temeke huku wapangaji wakidai kuwa wenye nyumba wanaingia mifukoni mwao kwa kutumua juju na kuchomoa pesa zao kimiujiza kwa mtindo unaojulikana zaidi kama chuma ulete.

Uchunguzi wa gazeti hili umebaini kwamba baadhi ya wapangaji katika maeneo ya Kigamboni, Mtoni na Yombo wamekuwa kwenye mzozo mkubwa na wenye nyumba kwa imani kuwa wanaibiwa pesa zao kimiuijiza na kuwaacha kwenye lindi la umaskini.

Baba mmoja anayeishi Kigamboni aliyeomba jina lake lisitajwe kwa hodu ya kutimuliwa kwenye nyumba amedai, anashangazwa na mzee mwenye nyumba ambaye amekuwa akifukiza madawa fulani ndani ya nyumba na kusababisha baadhi yao kuhama kwa kuhofia pesa zao zisichukuliwe.

"Kila anapofukiza dawa hizo, utakuta mpangaji yoyote akiingia na pesa na kuziweka nyumbani, zinapotea katika mazingira ya kutatanisha au matumizi yasiyojulikana na kujikuta pesa inakwisha haraka," amelalamika na kuongeza: " "Lakini asipofukiza dawa utakuta pesa inatulia na unaweza kufanya mambo ya maana."

Akadai kuwa baba huyo ana wake wawili hana kazi na familia inakula na inalala na si kwamba ana watoto wakubwa wanaomsaidia kwani yeye anashinda amekaa akicheza bao katika vijiwe vya eneo hilo na muda wa chakula ukifika anakula na kulala.

Hofu hiyo ya kupoteza pesa kwa njia hiyo sasa imewafanya wakazi wengi wa jiji kukimbilia benki mara tu wanapopokea mishahara au malipo yoyote kutokana na biashara zao wakidai kwamba wanazinusuru na wenye nyumba wajanja.

Mama mmoja ambaye amejitambulisha kwa jina la Apronia amesema: "Ilibidi niende kwa mganga ili atambue nini kinachofanya nishindwe kufanya maendeleo wakati nina uwezo wa kuingiza pesa za kutosha ambazo zinaweza kunipa maendeleo makubwa. Mganga alinishauri nihame nyumba na nikaanza kupata maendeleo."

Hamza Jumanne anayeishi katika Nyumba za Tazara Temeke anashangazwa na matumizi ya pesa siku hizi. "Tuko watu watano kwenye familia ila nikipata shilingi elfu hamsini Ijumaa nikifika Jumatatu ninakuwa sina kitu. Sio bure, naona tunachezewa," amedai.

Mkazi wa Kurasini, Joseph Mlawa amekana akisema kwamba chuma ulete ni imani za watu ambao hawajui kwamba kutokana na mfumuko wa bei pesa inatumika nyingi kununulia vitu vichache.

"Hapa hakuna mchawi. Ni kupanda tu kwa hali ya maisha kwa sababu kama mwaka jana ulitumia sh 10,000 kununua vitu vitano, leo utatumia pesa hiyo kununua vitu viwili vitatu tu. Kama ni chuma ulete inaletwa na hali ya uchumi na wala siyo wenye nyumba," amesema Mlawa.

Amesema kuwa wanaoamini kwamba kuna chuma ulete wanashindwa kwenda na wakati na kufuatilia vizuri mabadiliko ya bei za vitu, mapato na matumizi yao nyumbani na nje ya nyumba.

"Kila siku tunaambiwa shilingi inashuka thamani maana yake ni kwamba unatumia pesa nyingi kununua vitu vichache tu. Hebu angalia kwa sasa nauli zinapanda, vinywaji vinapanda, mboga zinapanda, dawa zinapanda na hata hao waganga wanaotuambia kuna chuma ulete wamepandisha dau. Nasema chuma ulete ipo kwenye hali halisi ya maisha lakini siyo wenye nyumba," amesisitiza.

Imani kwamba kuna chuma ulete inazidi kuota mizizi hasa jijini Dar es Salaam ambapo matumizi ya pesa ni makubwa huku baadhi wakiamini kwamba wanachomolewa pesa kwa kutumia madawa na wengine wakiamini kwamba kupanda kwa bei ya bidhaa na huduma ndiko kunasababisha hali hiyo.
 
du! hii kali hizi imani balaa lkn nashukuru zimesaidia kwani atlast watu wanakimbiza pesa zao bank mahali ambapo ni salama zaidi
 
0 Reactions
Reply
Back
Top Bottom