Chongolo: Wasiohudhuria vikao vya mashina kukiona

Shadow7

JF-Expert Member
Sep 28, 2020
13,768
20,158


KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Daniel Chongolo akiambatana na wajumbe wengine wa Sekretarieti ya CCM Taifa ameendelea na ziara katika Mkoa wa Mbeya akitokea Songwe.

Akiwa katika kikao cha ndani jijini Mbeya Katibu Mkuu amesisitiza wanaCCM kuhudhuria vikao vya mashina ikiwa ndio msingi wa uimara wa Chama, na kila mwanachama anawajibika katika shina lake.

"Tumekuja huku chini kwenye Mashina kwa sababu huku ndipo kwenye uhai wa Chama Chetu, hapa kwenye Shina tunazungumza na wanachama wote na ndipo penye wananchi." Katibu Mkuu Chongolo ameeleza.

Aidha ameongeza kuwa, "Ukweli ni kwamba sisi wote hapa ni wanachama wa Mashina, hapa hakuna mwanachama wa tawi, kata, wilaya, mkoa wala Makao Makuu, Mwenyekiti wa Chama Chetu ni mwanachama wa Shina, mimi (Katibu Mkuu) ni mwanachama wa Shina, kila mmoja wetu hapa ni mwanachama wa Shina."

Chongolo akifafanua umuhimu wa mahusiano na ushirikiano, ameeleza kuwa hakuna maendeleo ya wananchi yanaweza kufikiwa bila ya kuwa na mahusiano na ushirikiano mzuri kati ya watendaji wa serikali na chama, ama baina yao viongozi kwa viongozi wa Chama na serikali, na yakikosekana hayo mambo mawili hakuna linaloweza kufanyika na kufanikiwa kwa manufaa ya wananchi wetu waliotupa dhamana ya kutuongoza.

"Ni lazima sisi viongozi na watendajj wa Chama na serikali, tuwe na uwezo wa kutenganish masuala binafsi na kazi tunazowajibika nazo, tukiwa na nidhamu kwenye hayo mambo mawili, na kuyapa kila jambo muda wake nawahakikishia changamoto ya mahusiano, migogoro, ugomvi, kutoelewana, kukunjiana sura kuchukiana, havitakuwa na nafasi, maana siku hizi mtendaji ama kiongozi akigombana na mke ama mume wake nyumbani anakwenda kumalizia hasira zake ofisini."

Akiendelea na ziara katika wilaya ya Kyela, Chongolo ametembelea Shina namba 01 Tawi la Lema, shina namba 01 Tawi la Fubu, shina namba 02 Tawi la Njisi , shina namba 02 tawi la Nazaleth ambapo ameeleza kwa undani umuhimu wa mikutano ya mashina.

"Tumekuja kuhimiza vikao hivi vya Mashina, kwetu sisi vikao hivi ni muhimu kuliko vikao vyote, kwa kiongozi yeyote mwakani anayetaka kugombea uongozi ndani ya Chama lazima awe na muhtasari wa mahudhurio ya vikao vya mashina."

Ameongeza kuwa, "Ukiwa mwanachama wa shina, ukaheshimu uongozi wa shina, ukamuheshimu balozi, tukajenga msingi wa kufuata kalenda ya Chama chetu ya vikao, na tukashiriki kwa adabu huku tukimuheshimu Mwenyekiti wa Shina Chama chetu hiki hakitayumba milele."

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu ametembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo mradi wa ujenzi wa shule ya sekondari ya upili (High School) ya Lema a Ukaguzi wa mradi wa ujenzi wa Kituo cha Huduma ya pamoja Mpakani katika eneo la Kasumulu mpakani mwa Tanzania na Malawi.

Ziara hii ni muendelezo wa Sekretarieti ya CCM taifa, kuimarisha Chama hiko kwa kushuka katika ngazi za mashina na kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo iliyoanzia katika mikoa ya Tanga, Rukwa, Songwe na sasa wapo mkoa wa Mbeya kwa kugawanyika katika wilaya tofauti za mkoa huo.
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom