Chondechonde Watanzania wenzangu!

Daddo

JF-Expert Member
Jan 17, 2013
1,433
1,019
Kwanza nianze kwa kusema poleni ndugu na jamaa mliopoteza baadhi ya ndugu katika familia zenu katika mlipuko wa bomu na risasi zilizopigwa pale kwenye mkutano wa CHADEMA Arusha. Huo si msiba wenu peke yenu bali ni msiba wa taifa zima ambalo kwa sasa tunasema limeshafikia pabaya sana
Ndugu zangu wana JF naomba nitumie muda huu kuandika niliyonayo moyoni maana sasa wengi hatuna uhakika wa kuoina kesho. Kama si kwa kudra za muumba nadhani hata leo hii wengi wetu tusingepata nafasi hii ya kuweza kukaa na kuweza kutoa ya mioyoni mwetu. Lakini wakati tunaendelea kuomboleza vifo hivi ambavyo kwa sasa vimekuwa kawaida kitu ambacho kinatufanya wengi wetu kuishi kwa mashaka na kutokuwa na uhakika wa kufika siku inayofata ni lazima tuwe makini, tutafakari na tung'amue kilicho nyuma ya pazia.
Katika kutafakari haya nimejiuliza swali hili ni wapi tulikotoka, wapi tulipo na wapi tunakwenda? Nadhani siyo mimi tu ambaye anafikiria haya bali wengi wetu wanajiuliza maswali mengi kama haya na pengine maswali magumu zaidi hata ya hili. Kipindi cha nyuma tena si mbali ilikuwa ni vigumu sana kusikia matukio ya kinyama kama haya ya mauaji tena ya kutumia silaha za moto kama bunduki na mabomu katika nchi hii iliyo jaa maziwa na asali japo vitu vyote hivyo vinawafaidisha wachache na wasio wazawa. Nakumbuka vifo vingi kama cha Mwangosi, padri kule Zanzibar, Mauaji ya watu kwenye nyumba za ibada (makanisa na misikiti), kamanda wa polisi mkoani mwanza, afisa wa usalama hapo da resalaam na kutekwa kwa watu na majaribio ya kuwaua japo pengine kwa kudra za Mungu wameweza kunusurika na vifo hivyo. Vitu kama hivi tulizoea kuvikia katika nchi za wenzetu sasa hatusikii tena bali tunashuhudia wenyewe, inasikitisha sana.

Nashawishika kusema kwamba pengine haya yanatokea kwa sababu ya watu wachache wenye uchu wa madaraka katika Taifa hili. Naomba niseme kwamba hapa sijamnyoshea kidole mtu yeyote maana mimi siyo mwanasiasa na wala si mshabiki ama mfuasi wa chama chochote cha siasa.
Lakini je kweli hata kama mtu anataka madaraka kuna ulazima wa kumwaga damu ya watu wasio na hatia ilhali katika midomo yetu ni wepesi wa kutamka maneno matamu kama vile watanzania wote ni ndugu‘ kumbe mioyoni mwetu tumejaza chuki na visasi?. Je ni kweli kwamba watanzania wa leo tumekuwa wepesi wa kuburuzwa na kushindwa kuvumiliana huku swala la diplomasia likiachwa nyuma? Nasema hivi kwa maana moja tu kwamba kila mtu anapo jaribu kuweka tegemeo hakuaminiki.

Ukiangalia JF ambapo wengi tunadhani tungeweza kuelimishana na kupelekea utatuzi wa matatizo yetu sasa nako kumekuwa kama huko tunapokukimbia. Kuna wakati unaweza kuona bandiko la siasa hapa, badala y kujadili mambo ya maana watu waelewe na kuacha uamzi wa mtu binafsi watu wanaanza kushambulia kwa kashfa na matusi. Mara CCM wawashambulie CHADEMA mara CHADEMA wawashambulie CCM mara huku CAF waje kinyumenyume ilimradi tu kila mtu aoneshe kidole lakini je huku ndio kujenga umoja wa taifa ambalo tunalitaka?

Katika hili nadhani tunatengeneza mpasuko mkubwa ambao utatumaliza siku za karibuni. Huwezi kunidanganya kwamba kama leo umeweza kumtukana mtu kisa si mwanachama au mkereketwa wa chama chako kesho utaweza kukaa naye na kujadiliana naye mambo ya maendeleo. Nakumbuka msanii Mrisho Mpoto aliimba kwamba waliopo hatuwataki na wanaotaka tuwape hatuwaamini. Jiulize ni kwanini msanii huyu aliimba wimbo kwa kuweka maneno kama haya kwenye wimbo wake. Hii nadhani aliona mbali kidogo juu ya vyama vyetu vya siasa ambavyo badala ya kutangaza sera vimejikita katika kuonesha makosa ya vyama pinzani na kujenga chuki kati ya wapiga kura kwa nia ya kutaka kupata wafuasi.

Pengine ukiangalia matukio mengi ya kinyama yanayotokea huku yakiacha mkanganyiko wa nani kahusika huku vyama nguli pinzani vikiishia kurushiana mpira utagundua maana nzima ya wimbo wa wa mzee Mpoto. Chukulia tukio jipya la juzi pale arusha kila chama kinadai chama kingine ndicho kilihusika na mauaji hayo. CHADEMA wanasema ni CCM waliohusika kwa nia ya kuvuruga mkutano na CCM wanasema kuwa CHADEMA ndiyo wahusika na walifanya hivyo ili waweze ku draw attention na kuonewa huruma kwenye uchaguzi. Sasa hapa nani anahaki? Kama si CCM walio husika ilikuwaje mhusika asikamatwe palepale maana ulinzi ulikuwepo na kwanini basi Polisi walianza kufyatua mabomu ya machozi na inasadikika na risasi pia na je kama si CHADEMA waliohusika ni kwanini mlipuko haukutokea katikati ya hotuba maana kama mlipuajia alilipua karibu na eneo la jukwaa ni kweli kwama mlengwa mmojawapo alikuwa kiongozi mkubwa wa chama lakni mlipuko ulitokea baada ya yeye kutoka eneo lile la jukwaa.

Okay hayo wanayosema hayaniumizi kichwa bali kinachoniuma ni huu uhai wa watu uliopotea na majeruhi waliopo ambapo wengine wanaweza kuwa na vilema vya maisha. Sasa watu kama hawa unajua maisha yao mbeleni yatakuwa ya namna gani na je influence yao kwenye jamii baada ya kulishwa sumu hii ya chuki dhidi ya vyama watawezaje kubadilika na kukubali kukaa na kujenga nchi pindi watakapo kuwa wamerudia hali yao ya kiafya? Pengine hata vizazi vitakavyo fata vitakuwa vikirithi sumu hii na kukua katika hali ya chuki kwamba miaka ya nyuma baba au babu alitaka kuuawa na chama fulani hivyo hata kama atakuwa yuko kwenye sekta nyeti ya serikari anaweza kwa kiasi kikubwa kufanya kazi kwa bias kutokana na chuki hiyo.

Mimi nadhani watanzania ni bora tukakaa tukajitafakari na kurudia uzalendo ambao sasa umekuwa ni historia. Vifo hivi ambavyo tunasema vinakingiwa kifua na viongozi wa kisiasa na tukiilaumu serikali kwa kushindwa kudhibiti kutokana na mfumo wa serikali ambao nguvu kubwa inatoka kwenye chama kwa maana kwamba kiongozi mkuu wa nchi ndiyo huyohuyo mwenyekiti wa chama tawala. Kitu ambacho ndiyo kitanzi chetu kinachotumaliza. Inamaana kiongozi anaposhindwa hana wa kumkanya na wala chama kinapokosea hakiwezi kukanywa maana kiongozi wake wa kwanza ni yeye sasa atakanya vipi wakati yeye ndiye mhusika wa kwanza. Kwa hiyo badala ya kukubali kosa lazima ifanyike mbinu ya kuweza kutafuta jinsi ya kulirushia upande mwingine yaani kwa wapinzani.

Lakini si kama chama tawala ndicho kinachopaswa kulaumiwa bali lazima tuangalie pia kupitia dirishani pengine tunaweza kuona kinachoendelea nje. Namaana gani basi hapa, jibu ni rahisi tu kwamba ni kweli tunapaswa kukubali kila tunachoambiwa na upinzani wa chama tawala? Vip kuhusu vurugu na maandamano yanayopelekea watu kupoteza maisha? Haya hatuyaoni ni kweli kwamba ukiwa mpinzani ni lazima uwe unaitisha maandamano ambayo mara nyingi yanaishia kukwaruzana na kupelekea uharibifu na maumivu kwa watanzania? Kama kweli uchungu tunao katika vyama vyetu kwanini basi tunapoyaona haya tusitafute njia mbadala kwa nia ya kuepusha maafa na upotevu wa mali za watu.

Jamani watanzania wenzangu mimi nadhani hapa tulipofikia panatosha kujifunza na pia si lazima ushabiki wa vyama ni mzuri sana lakini usiwe ule wa kujenga chuki katika kizazi kilichopo na kijacho bali uwe wa kuitakia Tanzania amani na maendeleo. Kwa mzalendo wa kweli anapaswa kukubali na kuchukua kile kizuri kutoka kwenye vyama vya siasa na siyo kukubli kujenga chuki kutokana na propaganda za vyama. Mwisho wakati wa kupiga kura mtu unakuwa peke yako na wala hausimami na mwenyekiti wa chama chako hivyo hapo waweza kumchagua unayeona anafaa kuwa kiongozi kwa maslahi ya watanzani na si kwa maslahi ya chama. Ila ukiingia na chuki za vyama lazima ukifika pale utaenda kuchagua chama na si kiongozi matokeo yake ndiyo hayo tunakuwa na lundo la viongozi wasiokuwa na uzalendo na wasioangalia maslahi ya taifa.

Oooh Tanzania nakulilia sana ninapoona amani na maslahi ya tanifa yanaondoka. Mungu ibariki Tanzania, mungu ibariki Afrika. Kilio changu naomba ukisikie. Samahani kwa kuwachosha ila inaniuma sana.
 
Back
Top Bottom