Chonde chonde Mizengo Peter Kayanza Pinda!

Herbalist Dr MziziMkavu

JF-Expert Member
Feb 3, 2009
42,315
33,111
Ninalazimika kutumia majina manne ya Waziri Mkuu, Mizengo Peter Kayanza Pinda kuonyesha heshima kubwa kwake, na bila shaka anapaswa kuipokea.

Sitaki aipokee kwa kuitikia ‘naam', la hasha. Sitaki aipokee kwa kukutana na kunishika mkono ikiwa ni ishara ya kuonyesha kuthamini…hata kidogo!

Ninataka na nitafurahi ikiwa hivi, alisome andiko hili akiwa katika hali ya utulivu mithili ya Kasisi wa Kanisa Katoliki anayeshiriki tafakari ya kiroho, hivyo kuipata nafsi yake uhuru wa kuutambua kusudio la ukweli wenye maslahi kwa umma, jinsi lilivyo.

Akijibu maswali ya papo kwa hapo bungeni Alhamisi iliyopita, Pinda alizungumzia mambo mengi, lililonigusa ni kuruhusu Wakuu wa Wilaya, kukitumikia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika utendaji kazi wao.

Ni rahisi kuamini kwamba baada ya tamko la Pinda, alipokuwa ajibu swali la Mbunge wa Nyamagana (Chadema), Ezekiah Wenje, kuhusu ushiriki wao katika majukwaa ya siasa, Wakuu wa Wilaya hasa walio wahafidhina na `waliotekwa' na `kuzama' ndani ya itikadi za kisiasa, hawatauangalia umma.

Kwa maana Waziri Mkuu ametamka wazi, kwamba si kosa kwa Wakuu wa Wilaya kuitumikia CCM katika utendaji kazi wao.

Yaani wawe huru ikibidi kusimamama majukwaani wanaposhiriki shughuli za kijamii, hata kusalimia kwa kusema, ‘kidumuu Chama Cha Mapinduziiiiiiiiiiiii.' Hii ni hatari isiyohitaji kufanyiwa mzaha.
Ninatambua na walio wengi wanatambua kwamba serikali iliyopo madarakani imeundwa na CCM, kwa maana ilishinda Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2010. Kinaweza kuendelea kushinda na kushinda ikiwa wananchi watakipa ridhaa. Si kosa hata kidogo.

Lakini serikali inapoundwa haina maana ijikite katika fikra za ki-chama. Watendaji wa serikali hawatekelezi majukumu yao kwa wanachama na wafuasi wa CCM tu, kwa maana hawalipwi kutokana na viingilio na ada za uanachama wa CCM, bali kodi ya umma mpana wa Watanzania.

Ni ukweli usiotiliwa shaka kwamba wapo watendaji serikalini wenye hulka ya kuisahahu jamii, kusahau majukumu na wajibu wao wa kikatiba, badala yake ‘kuzikumbatia' itikadi za vyama vyao.

Kwa maana mtu anaweza kuwa serikalini, lakini akawa katika kuzikubali itikadi za TLP, NCCR-Mageuzi, UDP, APPT-Maendeleo, NRA, CCK, CUF, Chadema, CCM ama chama chochote kilicho na usajili wa kudumu.

Lakini anapokuwa katika utumishi wa umma, hapaswi, hata kwa sekunde moja iliyo ndani ya siku 365 za mwaka, kushirikisha imani yake katika itikadi za kisiasa ndani ya utumishi wa umma. Ndivyo inavyowapasa Wakuu wa Wilaya. Pinda anatupeleka wapi?

Anapotokea kiongozi kama Pinda, kuliambia Taifa na ulimwengu kwa ujumla, kwamba ni ruksa kwa Wakuu wa Wilaya kuitumikia CCM katika utekelezaji wa majukumu na wajibu wao kwa umma, haistahili kukubalika hivyo.

Kwa maana ruhusa hiyo haitakuwa kwa Wakuu wa Wilaya tu, itaenea pia kwa mawaziri, makatibu wa wizara, wataalamu wa masuala ya jamii kama afya, ustawi, miundombinu, elimu na wengine wanaoweza kuongezwa kwenye orodha ya waliopo hapa nchini!

Kwa tamko la Pinda, wale wasioiishi itikadi ya CCM, watajitenga na watendaji wa serikali katika hatua zote, ikibidi kutoshiriki michango inayotambulika kwa mujibu wa sheria-kupitia kulipa kodi, kwa maana kufanya hivyo ni kuipa nguvu CCM.

Hali hiyo itapunguza ari ujenzi wa taifa lenye umoja na mshikamano hasa katika kushiriki shughuli za maendeleo zinazohitaji nguvu ya raia wake.

Wapo wanaoweza kuhoji, inakuwaje utoe kodi inayowalipa Wakuu wa Wilaya ambao serikali kuu kupitia kwa Pinda, imeweka bayana kwamba wapo huru kuitumikia CCM?

Nchini Marekani kama zilivyo nchi nyingine ikiwemo Tanzania, Rais wa nchi anatokana na chama cha siasa. Lakini akishinda uchaguzi na kuapishwa kuiongoza nchi, anakuwa mtumishi wa umma anayelipwa na umma. Hivyo anapaswa kuwajibika kwa umma na si kwa chama cha siasa.

Lakini kutokana na uanachama wake, mathalani wa Rais Barrack Obama katika Democratic, anawajibika kushiriki shughuli za kisiasa za chama chake.

Pamoja na ukweli huo, akiwa katika shughuli za kisiasa, gharama zote zinazohitajika kwa muda, rasilimali na nyinginezo, vinagharamiwa na chama chake. Fedha ya umma haiguswi. Kuna daraja linalotenganisha siasa na utumishi wa umma.

Taifa lililogubikwa na umasikini wa kutupwa kama Tanzania, anatokea Mkuu wa Wilaya, anayetumia gari la umma, mafuta yanayolipiwa kwa fedha za Watanzania wakiwemo watoto wanaozaliwa wakiwa na dakika moja ya kuwepo duniani, aache kuzungumzia maslahi ya umma, anaipigia debe CCM! Kwa Pinda hiyo si kasoro! Kweli?

Kwani CCM isipojitokeza katikati ya vinywa vya Wakuu wa Wilaya, hakuna fursa mbadala ya kuliekeza taifa namna bora ya kuondokana na umaskini, ili ipige hatua za maendeleo?

Ama ni kutokana na dhana iliyojengeka, kwamba Wakuu wa Wilaya walio wengi hawana uwezo wa kuongoza, kwa sababu wametokana na utashi na maslahi ya kisiasa!

Hivyo hawana namna nyingine ya kuficha udhaifu wao wa kiuongozi isipokuwa kulikimbilia jina la CCM na kulitaja mara kwa mara kwenye mikutano inayopaswa kuwa ya kuhamasisha maendeleo?

Ndani ya jamii yenye kukabiliwa na ukosefu wa huduma bora za afya, elimu, umasikini wa kipato, mgawanyo usio sahihi wa rasilimali za umma, ‘kuporwa' kwa sehemu ya ardhi yao, jina la CCM lina manufaa gani kiasi cha kuwatia jeuri Wakuu wa Wilaya wajinasibu kwa hilo?

Chonde chonde Mheshimiwa, chonde chonde mtoto wa mkulima, chonde chonde Waziri Mkuu, chonde chonde Mizengo Peter Kayanza Pinda, kubali ukweli huu, kwamba Tanzania ni bora kuliko CCM.

Waliopewa dhamana ya kuutumikia umma wajiepushe ya u-CCM, waurejee umma wa Watanzania, mahitaji na matakwa yao.

Vinginevyo utakuwa unachangia kuisafisha njia ya kutafuta mbadala wa chama kinachojikumbatia badala ya kuukumbatia umma.Ni hayo tu Mzee!

Mashaka Mgeta ni Mwandishi wa Habari za Siasa wa NIPASHE. Anapatikana kupitia simu namba +255754691540, 0716635612 ama barua pepe;mgeta2000@yahoo.com.




CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

 
Wanaelewa basi tu ujeuri!pinda huwa hafkirii hata dakika moja kabla yakutoa kauli,alishawahi kuhalalisha kujichukulia sheria mkonon kwa wanaoua albino,mara liwalo na liwe.2shamzoea
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom