Changamato za ufisadi hazina majibu

Joseph Tunu

Member
Apr 8, 2016
55
14
Wazazi, Wanafunzi, Wafanyakazi, Waajiri, Vyuo wenza na wananchi wote kwa ujumla ni wadau wa Chuo cha Ufundi Arusha. Mara kwa mara imekuwepo mijadala kwenye mitandao ya kijamii na hata kwenye magazeti kuhusu chuo hicho na mara nyingi imekuwa ni malalamiko na tuhuma za matumizi mabaya ya ofisi.

Ni wakati muafaka sasa kwa Serikali kufanya uchunguzi ili kuweza kutoa majibu kwa wananchi kuhusu mambo ambayo yanalalamikiwa na wadau mbalimbali wa chuo hicho. Nimefuatilia na kuona kwamba yapo mambo ambayo Serikali haipaswi kuyapuuza. Mara zote na ndivyo ilivyo, kuwa penye moshi pana moto. Serikali inaombwa kufuatilia na kutoa majibu juu ya mambo mbalimbali yanayolalamikiwa kama ifuatavyo:

1) Inaonekana pengine Chuo cha Ufundi Arusha kina uhaba wa malazi ya wanafunzi hasa wanafunzi wa kike. Kama kuna ukweli, ni nini kimefanyika au kinafanyika kuondokana na tatizo hilo?

2) Inaonekana pengine vifaa vya kufundishia na kujifunzia havipatikani kwa wakati na pia vikipatikana ni kwa kiasi kidogo sana. Kama ni kweli ni kwanini?

3) Inaonekana pengine miradi ya ujenzi iliyofanywa katika kipindi cha 2010 hadi sasa ina mashaka. Kama kuna ukweli, serikali imefanya nini kuondokana na mashaka hayo siku zijazo?

4) Inaonekana pengine kampuni inayosikika kuwepo chuoni ijulikanayo kama ATC-PCB ni mchwa unaotafuna fedha ya umma bila huruma. Je Serikali ilishafanya uchunguzi wowote kuhusu uhalali wa kampuni hiyo na jinsi kampuni hiyo inavyojiendesha au inavyoendeshwa?

5) Inaonekana pengine kuna ubaguzi katika kulipana mishahara ndani ya chuo hicho. Kadhalika inaonekana pengine sehemu kubwa ya ajira mpya zinakwenda kwa upendeleo. Ni nini kimefanyika kuwapa wananchi imani kuwa ajira za chuo hicho zinafuata haki na zinagombaniwa kwa haki kwa watanzania wote wenye sifa?

6) Inaonekana pengine wapo wafanyakazi ndani ya chuo hicho ambao hawana vyeti lakini wanalipwa mishahara mikubwa tu na serikali. Je ni uhakiki gani umefanywa kuhakikisha tatizo hili halipo au kama lipo limeshughulikiwa kwa namna gani?

7) Inaonekana pengine Chuo cha Ufundi Arusha kinaendeshwa kwa madeni, kwamba wafanyakazi wanadai stahili zao mbalimbali na wazabuni mbalimbali wanadai kwa huduma mbalimbali walizotoa kwa chuo. Je Serikali ilishafanya uchunguzi wowote kuhusiana na sababu za madeni ya chuo hicho na kujua sababu za madeni hayo?

8) Inaonekana pengine Chuo cha Ufundi Arusha hakina bajeti iliyopitishwa na mamlaka zinazohusika. Kadhalika inaonekana kama Chuo cha Ufundi Arusha hakifuati taratibu za mapato na matumizi. Inadaiwa kwamba bajeti ya chuo ni sawa na andiko tu la kuombea fedha Serikalini. Fedha ikishapatikana zinatumika tofauti na andiko lililotumika kuombea fedha. Je Serikali inafahamu lolote kuhusiana na madai hayo?

9) Inaonekana pengine kuna baadhi ya wafanyakazi wa Chuo cha Ufundi Arusha waliopewa zawadi ya matofali zaidi ya elifu ishirini (20,000) na mkandarasi mmoja aliyepewa kazi mfululizo chuoni hapo. Je Serikali iliwahi kuchunguza na kujua ukweli wa ni nini lilikuwa lengo la zawadi hiyo, na ni wafanyakazi gani walinufaika na zawadi hiyo?

10) Inaonekana pengine wanafunzi wanaosoma masomo ya kilimo cha umwagiliaji Chuo cha Ufundi Arusha hawafanyi mazoezi kwa vitendo kwa kukosa shamba darasa licha ya wafadhili mbalimbali kutoa msaada wa mamilioni ya fedha ili kufanya shamba lililopo eneo la Oljoro kuweza kutumika kwa sababu hiyo. Je Serikali imeweza kufuatilia na kujua sababu za shamba hilo kutoweza kutumika na zilikwenda wapi fedha za wafadhili?

11) Inaonekana katika kipindi cha Januari, 2014 pengine mishahara ya wafanyakazi zaidi ya 20 ilitumika kwenye matumizi mengineyo ya chuo hicho na wafanyakazi hao wamekuwa wakidai haki yao hiyo bila mafanikio. Je kuna ufuatiliaji wowote uliofanyika kujiridhisha kuwa matumizi yaliyofanywa kwa kutumia mishahara ya wafanyakazi hao ilikuwa ni halali au sio halali?

12) Inaonekana pengine kuna kisima cha maji kilichimbwa kwa mamilioni ya fedha za umma chuoni hapo na mpaka sasa hakitoi maji licha ya kuwa chuo kina uhaba mkubwa wa maji kutokana na ongezeko la idadi ya watu chuoni. Je serikali imewahi kufuatilia na kufahamu sababu hasa za kisima hicho kutotoa maji licha ya mamilioni ya fedha kulipwa?

13) Inaonekana pengine kuna uficho katika kuweka bayana mapato na matumizi ya chuo hicho hali inayozua manung’uniko na malalamiko ya mara kwa mara kutoka kwa wafanyakazi kwamba baadhi ya fedha za umma hupotelea kusikojulikana. Je Serikali imewahi kujiridhisha kwamba hakuna upotevu wa fedha za umma au matumizi yasiyoridhisha katika chuo hicho?

14) Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ndiye anayepaswa kukagua hesabu za Chuo cha Ufundi Arusha, lakini kutokana na kuwa na watendaji wachache, CAG alitoa kazi hiyo kwa kampuni binafsi za ukaguzi kufanya kazi hiyo kwa niaba yake. Kwa bahati mbaya au kwa makusudi kampuni iliyopewa kazi na CAG imesahaulika na kufanya kazi chuoni kwa kipindi cha zaidi ya miaka mitano (5). Hali hii ya mkaguzi kukaa shirika au taasisi moja kwa muda mrefu inaonekana hujenga mazoea yasiyo mazuri na chuo. serikali ina mpango gani kubadilisha utaratibu huu?

Katika kuzoeana huko, imeonekana pengine kampuni iliyopewa kazi na CAG wameingia makubaliano na chuo ili kupata hati safi kila mwaka licha ya mapungufu kadhaa ambayo pengine katika macho ya kihasibu na kikaguzi yangeonesha kuna utata. Inafahamika kwamba baada ya malalamiko mengi Serikalini, ofisi ya CAG ilituma wakaguzi wake kufanya ukaguzi maalumu (Special Auditing), lakini mpaka leo haifahamiki ni nini ilikuwa matokeo ya ukaguzi ule. Ila vitendo vinavyoashiria ubadhirifu bado vinaendelea tena pengine kwa kasi zaidi. Serikali ina majibu gani juu ya hili?

15) Kadhalika inafahamika kwamba TAKUKURU waliwahi kuchukua baadhi ya nyaraka kutoka Chuo cha Ufundi Arusha. Kutokana na sababu zisizojulikana, Kamanda wa TAKUKURU Mkoa wa Arusha wa wakati huo Eng Mbengwa Kasomambuto aliamuru kwamba nyaraka zilizokuwa zimechukuliwa kutoka chuoni na maafisa kutoka ofisini kwake, zirudishwe mara moja na uchunguzi ukakomea palepale. Haifahamiki ni kwanini Kamanda wa TAKUKURU Eng Kasomambuto aliamuru kuchukua nyaraka na haifahamiki ni kwanini kamanda huyohuyo wa TAKUKURU Eng Kasomambuto aliamuru nyaraka zirudishwe. Kadhalika haifahamiki ni kwanini kazi ya uchunguzi haikufanyika tena na badala yake alipendekeza baadhi ya maofisa wa chini yake waliokuwa wanashughulikia uchunguzi huo kuhamishwa vituo vyao vya kazi. Je Serikali inafahamu jambo hili? Ni nini kauli ya Serikali huhusu jambo hili?

Ni katika mazingira haya ndio maana wananchi na wadau wote wa Chuo cha Ufundi Arusha wanaomba Serikali yao Tukufu kuwapa majibu ya kuna nini ndani ya chuo hicho? Je, mali yote kwa maana ya wanafunzi, wafanyakazi, fedha, majengo, mashine na mitambo mbalimbali iliyo katika karakana za chuo hicho iko kwenye mikono salama?

Wananchi wangependa kusikia kutoka kwa watendaji wa Serikali yao kwamba je, anachokitaka Rais wetu mpendwa Mheshimiwa Magufuli na Serikali yake, ndicho kinachofanyika Chuo cha Ufundi Arusha? Serikali isaidie wananchi kupata majibu haya!
 
Back
Top Bottom