Mwanahabari Huru
JF-Expert Member
- Mar 9, 2015
- 14,242
- 34,903
Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) ni chama cha kitaaluma cha Madaktari wa binadamu kilichoanzishwa mwaka 1965 kwa madhumuni ya kuendeleza na kuwalea wanataaluma kimaadili na ueledi wa kitaaluma na kusimamia taaluma ya udaktari nchini. Hivyo basi chama hiki kinajukumu la kuwasimamia kwa kushirikiana na Baraza la Madaktari Tanganyika(MCT) katika kutoa huduma iliyotukuka kama inavyokusudiwa na jamii na kusimamia maslahi mapana ya madaktari.
1.0: Utangulizi
Chama cha Madaktari Tanzania (MAT) kimepata taarifa kupitia vyombo mbalimbali vya habari kuwa siku ya tarehe 18 Machi 2017 Serikali ya Tanzania kupitia kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dr John Pombe Joseph Magufuli ilikubali ombi la Serikali ya Kenya kupeleka Madaktari takribani 500 kwa lengo la kutoa huduma za afya katika Hospitali zake.
Pia Chama kimeona nakala ya barua katika mitandao ya kijamii kutoka katika Ofisi ya Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dr. Ulisubisya Mpoki inayotoa maelekezo ya maombi ya kazi kwa Madaktari wahitaji wanaotaka kwenda Kenya kwa ajili ya kufanya kazi.
Hivyo basi ni muhimu kufahamu kwamba jambo hili nyeti limefanyika bila MAT kushirikishwa katika hatua yeyote. Baada ya taarifa hii kutolewa, ni jukumu letu kama chama cha kitaaluma kutoa ushauri ,maoni na mapendekezo ili kuweza kujenga ustawi bora na udugu wa wanataaluma ndani na nje ya mipaka ya nchi yetu.
2.0: Kiwango cha Upungufuwa wa Madaktari
Kwa mujibu wa ripoti ya Task Sharing policy Guidelines for Health Sector Services in Tanzania, ya mwaka 2016, inataja sekta ya afya kuwa na upungufu mkubwa sana wa watumishi wa afya hususani kada ya Madaktari. Mfano, katika Vituo vya afya(Health Centres), Mahitaji ni madaktari 771 wakati waliopo ni 57 tu, kwa Hospitali za Wilaya mahitajini 1,760 waliopo ni 441 tu na wakati kwa hospitali za Mikoa Mahitaji ni 725 walioponi 328 . Kwa ujumla Tanzania ina upungufu wa Madaktari takribani 2,430 ambao ni sawa na asilimia sabini na tano (75%).
Hivyo basi, Tanzania tunahitaji zaidi madaktari pegine kuliko Kenya. Ni vema kufahamu kwamba taarifa iliyotolewa na Chama cha Madaktari cha Kenya kupitia kwa katibu Mkuu Dr.Ouma Oluga inataja kuwa mpaka sasa Kenya ina Madaktari takribani 1,400 ambao bado hawajaajiriwa na wapo katika msururu wa kusubiri ajira kutoka katika Serikali yao.
Pia ni muhimu kutambua ya kwamba Madaktari wa Kenya wamekuwa katikaMgomo kwa takribani siku 100 uliokuwa na lengo la kushinikiza maboresho ya maslai yao pamoja na mazingiraya kazi, Na kwa taarifa tulizonazo ni kwamba pande husika zilisaini makubaliano Tarehe 18 Machi 2017 na kwa sasa wanasubiri utekelezaji wa makubaliano husika.
3.0 :Mtazamo wa Madaktari wa Kenya
Kumekuwa na maoni tofauti juu ya Madaktari wa Tanzania, huku asilimia kubwa wakipinga hatua hiyo kwa kigezo kwamba Kenya ina Madaktari ambao bado wanasubiri ajira na hivyo kuishauri Serikali yao kuajiri kwanza wazawa kabla yawageni. Hili linathibitishwa na kura ya maoni iliyoendeshwa na kituo cha Televisheni cha KTN ambapo zaidi ya asilimia 60 walipinga ujio wa Madaktari kutoka Tanzania.
Baadhi yao wamekuwa na dhana kwamba ujio wa Madaktari kutoka Tanzania unalengo la kuhujumu makubaliano yao ambayo utekelezaji wake bado haujaanza. Licha ya hayo, kumekuwa na jumbe za chuki katika mitandao mbalimbali zinazodhihirisha ukinzani wa wanataaluma wa Kenya dhidi ya Serikali yao, na uamuzi wa kuwaleta Madaktari kutoka Tanzania.
4.0: Mtazamo wa Madaktari wa Tanzania
Pia kumekuwa na maoni tofauti huku baadhi wakipinga na wengine wakiunga mkono na kuona fursa muhimu ya kupata ajira hasa kwa wale ambao hawana ajira. Wengi wanaopinga wanatoa hoja kuhusu hali ya usalama nchini Kenya, tatizo la ukosefu wa ajira na Mtazamo hasi wa jamii ya Kenya dhidi ya Madaktari wa Tanzania.
5.0: MASWALI MUHIMU KWA SERIKALI.
Kwa kuwa MAT haikushirikishwa katika hatua yeyote na hivyo kukosa fursa yakufahamu lolote, Hivyo basi tungependa kupata ufafanuzi kuhusu masualayafuatayo ;Kwa nini Serikali ya Kenya imeshindwa kuajiri Madaktari wake na kuanza kutafuta Madaktari kutokaTanzania huku ikizingatiwa kwamba malipo ya Madaktari wa Tanzania yatakuwa makubwa zaidi ya wenyeji ?
Kwa nini ombi hili limefanyika kipindi cha mgomo, na utekelezaji wake umekuja siku chache baada ya kuweka makubaliano ya kusitisha mgomo?
Kwa nini suala hili linafanyika wakati wa kuelekea katika Uchaguzi Mkuu 2017?
Ni nani atawajibika katika suala la usalama wa raia wetu, ikizingatiwa kwamba tayari kuna viashiria vya chuki, na ikizingatia Kenya bado ina changamoto za kiusalama?
Ni kwa jinsi gani Madaktari wataweza kufanya kazi bila kukamilisha taratibu za kisheria kama vile kufanya mitihani ya Bodi na kusajiliwa ilikupata uhalali wa kutibu?
6.0: HITIMISHO
MAT ingeunga mkono jambo hili kama lingefanyika katika muda muafaka na likiwa shirikishi.
Na kwa kuwa mpaka sasa Serikali ya Kenya bado haijaanza kutekeleza matakwa ya makubaliano baina yake na Madaktari wao.
Na kwa kuwa taratibu za kufanya kazi katika nchi nyingi zinataka daktari husika kusajiliwa na Bodi husika ili kupata leseni kwa kufanya mitihani inayochukua takribani siku (90)
Na kwa kuwa Madaktari wengi wa Tanzania wanaweza kuwa wageni kabisa katika ardhi ya Kenya.Na kwa kuwa Kunaupungufu mkubwa wa Madktari Tanzania hata Kuliko Kenya
MAT inasisitiza kwamba;
Ni muhimu kusitisha zoezi la kuwapeleka Madaktari wa Tanzania mpaka hapo Serikali yaKenya itakapoanza utekelezaji wa makubaliano kati yake na Madaktari wao.
Serilali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itafute namna ya kuwaajiri madaktari wake ili kuziba pengo kubwa la upungufu wa madaktari nchini.
(signature)
IMETOLEWA NA CHAMA CHA MADAKTARI TANNZANIA