Chagua Vita Vyako...

maggid

JF-Expert Member
Dec 3, 2006
1,084
1,246
Ndugu zangu,

Maishani kuna kushinda na kushindwa. Hata hivyo, ushindi una gharama. Siku zote, mwanadamu jiandae na gharama ya ushindi.

Mana, ushindi waweza kuwa ghali mno. Ndio, unaweza kupambana ukashinda, lakini, gharama ya ushindi yaweza kuwa jamaa na marafiki wa wote uliowashinda watageuka kuwa maadui zako. Yawezekana
watakuwa maadui kwako kwa muda mrefu tu. Watakukasirikia, watafanya yote nawe upate maumivu.

Hivyo, mwanadamu usifikiri tu gharama ya kushindwa, fikiri pia gharama ya ushindi. Na wakati mwingine, ni gharama inayostahili kulipwa. Franklin Roosevelt alikuwa Rais wa zamani wa Marekani. Alifahamu faida na hasara za kuwa na maadui. Waliompinga katika sera zake za kiuchumi aliwaita " Watiifu wa Kiuchumi". Na akasema; wamejiunga kwa pamoja kunichukia na nakaribisha chuki zao kwangu!

Ndio, kama unapigana vita ya muhimu. Na kama vita hivyo vyaweza vikawa vya kushinda (winnable). Na kwamba umejiandaa kulipa gharama ya chuki ya muda mrefu ya utakaowashinda, basi, ingia vitani. Na kama la, basi, tafuta suluhu, au rudisha majeshi nyuma kimpangilio ( tactical retreat).

Swali ni hili; utafikiaje uamuzi wa ama kuingia vitani au la?

Miaka mingi iliyopita alitokea Mfalme wa Epilus aliyeitwa Pyrrhic. Mfalme huyu aliamua kuingia vitani kulikabili jeshi kubwa na lenye nguvu nyingi. Ni jeshi la Warumi. Lakini, kabla ya Mfalme kuingia baharini na vikosi vyake ili kuitafuta Italia ya Warumi, msaidizi wake wa karibu, Cineas, aliomba mazungumzo ya faragha na Mfalme. Alitaka kumwuliza maswali na kumshauri.

Cineas alimtamkia Mfalme; “ E bwana Mfalme, Warumi wanasadikika kuwa na jeshi kubwa , lenye nguvu na lenye mashujaa wengi. Ndio maana wameteka nchi nyingi. Je, Mungu akitusaidia, tukaja kuwashinda Warumi,
tutafanya nini na ushindi wetu? Mfalme akajibu: “ Mbona hilo ni swali jepesi sana. Mara ile tukiwashinda Warumi, hakutatokea jeshi kutoka mji wowote wa Italia litakaloweza kupambana nasi.”

Cineas alitulia kidogo, kisha akamwuliza Mfalme: “ Tukishaikamata Italia ya Warumi, kipi kitafuatia?”
Mfalme akajibu: Sicily ni kisiwa chenye hazina za thamani kubwa, itakuwa rahisi sana kukiteka kisiwa hicho.”

Cineas aliendelea kuuliza: “ Bwana Mfalme, unaongea juu ya mambo ya kusadikika, lakini una maana kukitwaa kisiwa cha Sicily kutakuwa na maana ya kukoma kwa vita?” Mfalme akajibu: “Hapo tutakuwa tumeikaribia Afrika. Na tukishaikamata Afrika ni nani hapa duniani atathubutu kutukabili kivita?”

“Hakuna” Alijibu Cineas, kisha akauliza;

“ Na baada ya hapo tutafanya nini?”

Mpaka hapo Mfalme hakujua Cineas alikuwa anampeleka wapi kwa lojiki ya kifikra. Mfalme akajibu:
“Baada ya hapo, tutapumzika, tutakula raha. Tutakula na kunywa. Tutabaki tukichekeshana na kucheka, siku nzima.”

Kama ni hivyo, alisema Cineas; “ Ni kitu gani kinachotuzuia kufanya hayo yote sasa bila kwenda vitani?
Mfalme hakuielewa mantiki ya Cineas. Akakaidi ushauri. Akavipeleka vikosi vyake kupambana na Warumi. Baada ya vita ngumu, jeshi la mfalme liliwashinda Warumi. Hata hivyo, lilipata hasara kubwa ya kupoteza watu na kuwa na majeruhi wengi. Jeshi lake likadhohofika sana. Likajaribu kuitwaa Sparta, likashindwa vibaya sana. Mfalme aliwindwa na hatimaye akakakamatwa kama kuku. Akauawa kwa kupigwa mawe kwenye mitaa ya Argos.

Naam, chagua vita vyako, na hilo Ni Neno fupi la usiku huu.


Maggid,
Iringa.
 
[EMAIL=" maggid" maggid[/EMAIL], Mzimu wa Mwangosi inakusumbua huna lolote...
 
Last edited by a moderator:
Huu ni utabiri wa kifo kibaya sana kwa CCM.
Kwamba, ama hawana au wameshindwa kabisa kuelezea ni nini hasa kinawafanya wao watake kuendelea kuongoza serikali yetu tena na tena na tena japo imethibitika bila shaka kwamba hawana uwezo wa kuyatatua na huku wakijua uma wa watanzania umedhamiria kukiweka chama hicho pembeni.

Tatizo la rushwa limekuwa kubwa sana na ni wazi CCM hawawezi kukabiliana nalo lakini bado wanaendelea kusisitiza kwamba wako vitani dhidi ya rushwa,kila mtu anaona na sasa ni wazi muendelezo wowote wa igizo lao dhidi ya rushwa unakisababishia chama hicho matatizo zaidi. Mwisho wao ni mbaya.

kwa ujumla wameshindwa kuboresha maisha ya watanzania, lakini bado wanasisitiza kwamba wamefanikiwa sana katika hilo na wanaendelea kuhimizana kutembea vifua wazi tena vikiwa mbele,Mwisho wao ni Mbaya.
 
Back
Top Bottom