CHADEMA yaupongeza uongozi wa TEF

figganigga

JF-Expert Member
Oct 17, 2010
25,658
55,487
CHAMA CHA DEMOKRASIA NA MAENDELEO.

SALAAM ZA PONGEZI KWA UONGOZI MPYA WA TEF

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kama mmoja wa wadau wa habari na vyombo vya habari, kupitia Idara ya Habari na Mawasiliano kinatoa pongezi za dhati kwa uongozi mpya wa Jukwaa la Wahariri (TEF) uliochaguliwa mwishoni mwa juma lililopita katika Mkutano Mkuu wa TEF ambao hufanyika kila baada ya miaka 4.

Kupitia taarifa hii tunautakia kila la heri katika kutimiza majukumu yake uongozi huo ambao unahusisha waandishi waandamizi nchini, Teophil Makunga akiwa Mwenyekiti wa jukwaa, akisaidiana na viongozi wengine ambao ni; Deodatus Balile (Makamu Mwenyekiti), Neville Meena (Katibu), Neng’inda Johanes (Katibu Msaidizi), huku Wajumbe wa Bodi wakiwa ni Bakari Machumu, Lilian Timbuka, Joyce Shebe, Salim Said Salim na Jesse Kwayu.

Tukiwa taasisi pekee ya kisiasa ambayo imetia saini Azimio la Dar es Salaam la Uhuru wa Uhariri na Uwajibikaji (DEFIR), tunawiwa kuwajibika kuwapatia ushirikiano wetu katika kutimiza majukumu yao ya kikazi na kitaaluma kadri tunavyoweza, tukiongozwa na dhamira ya kuhakikisha tasnia ya habari inaendelea kuwa mhimili imara na huru kuitumikia jamii ya Watanzania isiyokuwa na sauti ambayo inahitaji sauti ya vyombo vya habari.

Uongozi huo mpya umechaguliwa katika kipindi ambacho mazingira ya utendaji kazi wa vyombo vya habari na wanahabari hata ya kitaaluma pia, yanazidi kuwa magumu kutokana na kutungwa kwa sheria zingine hatari zinazowasaidia watawala wa sasa kuminya uhuru wa habari na upatikanaji wa taarifa, kuliko hata ilivyokuwa wakati wa ukoloni, wakiongezea kwenye sheria mbovu zilizokuwepo.

Ni rai yetu kuwa uongozi huo wa TEF ambao unaundwa na waandishi waandamizi, utaifanyia kazi changamoto nyingine ‘mpya’ ambayo inatokana na watawala kubadili mbinu za kutisha vyombo vya habari nchini ambapo sasa wameamua kwenda hatua ya KUFUTA chombo cha habari, tofauti na huko nyuma ambako walikuwa wanafungia chombo cha habari kwa muda fulani unaojulikana au usiojulikana.

Huo ni udikteta mkubwa ambao haukutarajiwa kutokea katika zama hizi ambazo uhuru wa habari na upatikanaji wa taarifa si tu umesaidia uwajibikaji kuwa nguzo ya ustawi katika jamii za nchi zilizoendelea lakini pia umekuwa kichocheo cha fikra zenye uwezo wa kuzalisha, kutafuta na kusambaza taarifa na maarifa kwa ajili ya maendeleo makubwa zaidi.

Uongozi huo mpya umebeba sehemu ya matumaini ya Watanzania ambao wangependa kuona nchi hii inaondokana na sheria za ‘kijima’ ambazo badala ya kuwahamasisha watu kuwa watafutaji, wasambazaji na walaji wa habari na taarifa, zinawafanya wawe waoga hata wa kusoma na kutumia teknolojia ya mawasiliano kupata habari.

Tukiwa sehemu ya wadau wa habari na vyombo vya habari nchini na nje ya nchi, tunaamini kuwa uongozi mpya wa TEF utaendeleza mazuri yaliyofanywa na uongozi uliopita, kisha kushirikiana na wadau wengine kuwa sehemu ya mapambano ya kuhakikisha nchi yetu inakuwa na sheria bora zinazosimamia tasnia ya habari, ikiwemo uhuru wa vyombo vya habari, hadhi ya wanahabari na haki ya kupata taarifa.

Imetolewa leo Alhamis, Februari 4, 2015 na;

Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA
 
Back
Top Bottom