The Sheriff
JF-Expert Member
- Oct 10, 2019
- 746
- 2,099
Jerry Silaa, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari.
Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limeeleza kutoridhishwa na kitendo cha Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Jerry Silaa, kukosa kuhudhuria mikutano muhimu ya wadau wa habari.
Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, ametoa kauli hiyo leo Novemba 7, 2024, katika Mkutano Mkuu wa Nane wa TEF uliofanyika Dar es Salaam. Waziri Silaa, licha ya kualikwa, hakuweza kuhudhuria na badala yake alimtuma Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo.
"Tukiwa kama wahariri, hatufurahishwi na mwenendo wa Waziri Silaa. Amealikwa kwenye Mkutano wa PST, hakufika; amealikwa kwenye tuzo za waandishi wa habari, hakuhudhuria; amealikwa Mbeya kwenye tukio la wadau wa habari, hakuwapo; na sasa Mkutano Mkuu wa TEF pia hajaja. Hii inaashiria kwamba Waziri hana nia ya kushirikiana na wadau wa tasnia ya habari."
Balile ameleza kuwa mikutano kama hii ni jukwaa muhimu ambapo wadau wa habari wanapata nafasi ya moja kwa moja kujadiliana na Waziri kuhusu mustakabali wa tasnia, na kutoonekana kwake kunakwamisha juhudi za ushirikiano.
"Mikutano hii ni fursa kwa Waziri na wadau wa habari kukutana na kuzungumzia changamoto na maendeleo ya tasnia. Kutokuwepo kwa Waziri ni dalili ya kukosekana kwa dhamira ya kushirikiana nasi."
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Nicholas Mkapa, ambaye amemwakilisha Waziri Silaa katika mkutano huo, amesema Waziri alikuwa na majukumu mengine ya kiofisi, na hivyo kumtuma yeye kuhudhuria kwa niaba yake.
Balile pia amekumbusha kuwa wakati Waziri Nape Nnauye aliposhikilia Wizara hiyo, alionesha ushirikiano wa hali ya juu kwa kuhudhuria mikutano yote muhimu ya wadau, na kuwa shirikiano huo ulikuwa na mchango mkubwa kwa maendeleo ya tasnia ya habari.
Pia, soma: