Chadema yashushia serikali tuhuma nzito

Ngongo

JF-Expert Member
Sep 20, 2008
18,894
31,106
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kimeibua tuhuma nzito kwa kuyahusisha moja kwa moja matukio mawili yaliyompata mbunge wa Karatu kwa tiketi ya chama hicho, Dk. Wilbroad Slaa na njama za kutaka kumuua, kwa madai kuwa anasimamia kidete sakata la mradi wa vitambulisho vya taifa wenye thamani ya Sh200 bilioni.


Dk. Slaa, mmoja wa wachangiaji wakubwa na wakosoaji wa serikali bungeni, alidai mwishoni mwa wiki iliyopita kuwa amekuta vifaa vya kunasa sauti vikwia vimetegwa kwenye kitanda chake, jambo ambalo alisema anaamini kuwa lilifanywa na watu wasiopendezwa na tabia yake ya kufuatilia kwa makini masuala ya ufisadi.


Chadema imesema matukio hayo ni mwendelezo wa njama za vigogo wa serikali dhidi ya viongozi wao na kulitaka Jeshi la Polisi kumuhakikishia usalama mbunge wao na kama haliwezi kufanya hivyo liseme.


Akizungumza na waandishi jijini jana, kaimu katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika alisema wanaamini kwamba matukio hayo yanahusiana moja kwa moja na vigogo wa dola walioisaliti kazi na wajibu wao na kuwa walinzi wa mafisadi na kutaka kumuua mbunge huyo.


"Sisi Chadema tunaamini kwamba matukio haya yanahusiana moja kwa moja na baadhi ya wanausalama wa taifa na maafisa wa vyombo vya dola waliozisaliti kazi zao na kuamua kusimamia usalama wa mafisadi dhidi ya haki za wazalendo wa taifa hili," alidai Mnyika bila ya kutaja mtu maalum anayehusika.


"Pamoja na kwamba polisi wako chini ya wizara inayohusika na ualama wa raia ambayo waziri wake ni Laurence Masha na kumekuwa na hoja ya Dk. Slaa dhidi yake kuhusu mradi wa vitambulisho vya uraia, hivyo tunataka polisi wawe huru kuchunguza kama wataona haja ya kumchunguza waziri huyo au kiongozi mwengine yeyote kutokana na mtiririko wa matukio."


Alidai kuwa ujasusi wa kuyaweka rehani maisha ya viongozi wa vyama umekuwa ukifanywa kwa muda mrefu na kwamba walisharipoti Jeshi la Polisi bila ya kufanyiwa kazi na kwamba sasa umefika wakati wa kutoufumbia macho tena.


Alilitaka jeshi hilo kuyafanyia uchunguzi mpana matukio hayo na kuyatolea ripoti haraka iwezekanavyo ili kuwaondolea mazingira ya kuonekana wanashiriki kulinda mafisadi nchini.


"Tunalaani matukio yote ya kukutwa kwa vinasa sauti katika vyumba vya wabunge wa Chadema na CUF na pia tunasikitishwa sana na uharamia wa namna hii kwa viongozi wetu ambao wanafanyiwa kutokana na harakati zao za kupinga ufisadi," alidai Mnyika.


Alisema vitendo vya kuvamia faragha ya mtu ni jambo ambalo kimataifa ni kinyume na haki za binadamu na kwamba linahatarisha usalama na amani ya mtu.


"Jeshi la Polisi limetoa taarifa kuhusu vinasa sauti hivyo lakini halikueleza kwa kina, vinatoka wapi, vimewekwa na nani na kwa nini cha mbunge wa Konde, Dk. Ali Tarab kilikuwa kimezimwa na cha Dk. Slaa kilikuwa kinawaka. Pia halikueleza kwa kina kuhusu chupa ya mvinyo, hivyo tunalitaka Jeshi la Polisi kuweka wazi haya," alisisitiza.


Alidai kuwa taifa lipo shakani na kwamba wanawataka Watanzania wa dini zote kuliombea taifa livuke majaribu na kuongeza kasi ya kuibana serikali kuhakikisha mafisadi wote wanafikishwa mahakamani, kufungwa na kufilisiwa iwapo watakutwa na hatia.


Alilitaka Jeshi la Polisi kutoa taarifa ya matukio ya vitisho kwa viongozi wa Chadema yaliyotokea mwaka juzi na mwaka jana na kuandikiwa barua.


Alidai kuwa vyombo vya dola na Usalama wa Taifa vinashiriki katika kuwalinda mafisadi na hivyo kuvitaka vyombo hivyo vichunguzane ili kuona mapungufu yalipo.


"... tunasisitiza kuwa baadhi ya wanausalama wetu waache tabia ya kutumiwa na mafisadi kwa kujaribu kuangamiza viongozi walio mstari wa mbele katika vita dhidi ya ufisadi," alisema Mnyika na kuongeza:


"Tunayasema haya kwa sababu mwaka 2007 wakati sakata la kashfa ya Benki Kuu (BoT), tulikuwa na taarifa tuliyoiweka hadharani ikitoka kwa ofisa mmoja wa usalama wa taifa kwenda kwa waziri mkuu kiofisi kumsisitiza kuwa hoja hiyo haipokelewi bungeni kwa kuwa serikali haiwezi kuwa na majibu ya kutosha".


Pamoja na hayo Mnyika alidai kuwa wameamuwa kutoa tamko hilo kama hatua za awali kwa kuwa bado wanaendelea kulifuatilia kwa karibu sana tukio hilo na kwamba watatoa tamko baada ya kumalizika uchunguzi.


Aliutaka umma wa Watanzania kuelewa kwamba kadri serikali inavyochukua muda mrefu kuwafikisha gerezani mafisadi ndivyo inavyotoa mwanya kwa mafisadi kuangamiza uhai na maisha ya wazalendo wanaojitolea kupambana nao.

Source:Mwananchi
 
Back
Top Bottom