CHADEMA yaanza kutumia Helikopta
Neville Meena na Mussa Juma, Arumeru
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) jana kilianza kutumia helkopta katika kampeni zake za kumnadi mgombea wake wa ubunge katika uchaguzi mdogo wa Jimbo la Arumeru Mashariki, Joshua Nassari.
Habari ambazo gazeti hili limezipata zinasema helkopta hiyo itaendelea kutumika hadi siku ya mwisho ya kampeni na kwamba itakiwezesha chama hicho kufanya mikutano kati ya mitano hadi minane kwa siku.
Mkuu wa Operesheni wa uchaguzi wa Chadema katika jimbo hilo, John Mrema alisema kuanza kutumika kwa helkopta hiyo kutamwezesha mgombea wao kufanya mikutano mitano kwenye kata tano tofauti.
Mikutano ya jana ilifanyika katika vijiji vya Ngurdoto Kata ya Maji ya Chai, Ngabobo Kata ya Ngarenanyuki, Kijiji cha Sakila Kata ya Kikatiti na vijiji na kata za Kingori na Nkoanrua.
Helkopta hiyo ilianza kuonekana katika anga la Usa River, Arumeru jana asubuhi na hakukuwa na taarifa za awali kuhusu ujio wake kama ambavyo chama hicho kimekuwa kikifanya katika kampeni nyingine zilizotangulia.
Helkopta hiyo yenye maneno makubwa CHADEMA, ilitumika wakati wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho zilizofanyika katika Uwanja wa Shule ya msingi Leganga, Usa River Machi 10 mwaka huu na tangu wakati huo haikuwahi kuonekana tena hadi jana.
Dk Slaa na ardhi
Katikamikutano ya jana, Katibu Mkuu wa Chadema, Dk Willibrod Slaa alimshambulia Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Gudluck Ole Medeye kwamba anahusika na kukodisha shamba la Valesca lililo Jimbo la Arumeru Mashariki kwa wawekezaji kwa bei ya kutupa.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara katika kijiji cha Ngabobo, Ngurdoto na Sakila, Dk Slaa alisema ni aibu mawaziri wa Serikali ya CCM kuomba kura katika Jimbo la Arumeru Mashariki huku wakiwa ni waasisi wa mpango wa kugawa ardhi ya umma kwa walowezi wa kizungu.
Alisema Naibu Waziri huyo, ambaye ni mbunge wa Jimbo la Arumeru Magharibi, kabla ya kukubali kutolewa shamba hilo lenye zaidi ya ekari 400 ambalo Serikali itapata kiasi cha Sh2.4 milioni tu kwa mwaka walipaswa kuwakumbuka wananchi.
Hivi kweli nyie wananchi wa Meru hamuhitaji ardhi hii na mngeshindwa kulipa Sh6000 kwa ekari moja ili muweze kulima, kama alivyouziwa mzungu? alihoji Dk Slaa.
Aliwataka wakazi wa jimbo hilo, kukubali mabadiliko sasa kwa kuchagua mbunge wa upinzani ili aweze kuhoji ardhi ya Meru ambayo kiasi kikubwa kimegawanywa kwa walowezi kutoka nje ya nchi.
MY TAKE: Sasa hivi wazee wa kuiga (CCM) wataleta Choppa, kama hamuamini angalieni after 3 days!!