Yashindwa kuwasilisha taarifa kama ilivyoagizwa na TRA
Na Mwandishi Wetu
CHAMA cha Demokrasi na Maendeleo (CHADEMA) kimeingia matatizoni kuhusiana na masuala ya ukwepaji kodi baada ya kushindwa kuwasilisha taarifa ya ulipaji kodi kama walivyoagizwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), imefahamika. Awali, TRA ilikiagiza CHADEMA kuwasilisha taarifa yao ifikapo Ijumaa iliyopita baada ya kudaiwa kuwepo kwa ukwepaji wa kodi unaofanywa na viongozi wa chama hicho kupitia mishahara ya watumishi na ununuzi wa vifaa mbalimbali vya chama. Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, Placidus Luoga, alikiri jana kushindwa kwa CHADEMA kuwasilisha taarifa hizo kama walivyowaagiza katika barua waliyowaandikia mwanzoni mwa wiki iliyopita. Barua hiyo ya TRA ilitokana na kutolewa kwa habari za kuaminika kutoka ndani ya chama hicho ambazo zilichapishwa na MZALENDO zikidai kuwa uongozi wa juu wa CHADEMA umehusika katika ukwepaji wa kodi katika mishahara na ununuzi wa vifaa vya uenezi vya chama hicho. Bado hatujapata taarifa yao... TRA hatuwezi kusema jambo lolote kama kweli wanalipa kodi ya mishahara kwa watumishi wao au la... ila taarifa zitakapoletwa ndiyo tutajua nini cha kufanya, alisema Luoga. Sheria ipo wazi kwa mtu au taasisi isiyolipa kodi, hivyo uamuzi wa adhabu si vizuri kuweka wazi kwa sasa hususan kipindi ambacho TRA haina taarifa zao za ulipaji kodi," alisema Luoga. Alisema baada ya kupokea taarifa hiyo ndiyo watajua nini cha kufanya kama TRA kwa mtu ambaye halipi kodi kupitia sheria na taratibu za mamlaka hiyo pamoja na kupata ukweli wa chama hicho kuwa kinakwepa kulipa kodi.
Mwajiri atawajibika kumlipia kodi mtumishi wake ikiwa TRA itaona mfanyakazi anastahili kulipa kodi, hivyo nao CHADEMA wakibainika kwenye hilo basi itabidi walipe kodi,alisema. Uongozi wa CHADEMA unadaiwa kukwepa kodi katika uingizaji wa vifaa mbalimbali ikiwemo vya uenezi ambavyo viliingizwa kutoka China kwa njia ya panya kupitia eneo la Holili mkoani Kilimanjaro. Vifaa hivyo vilinunuliwa na chama hicho kwa ajili ya uchaguzi mkuu wa 2010 baada ya kupata msaada wa sh. milioni 100 kutoka kwa mmoja wa wafanyabiashara nchini. Hata hivyo, ununuzi wa vifaa hivyo unadaiwa kughubikwa na utata kutokana na uamuzi wa Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe kudai kuwa aliongeza sh.milioni 188 ili kununua vifaa hivyo na kufanya kiasi cha fedha kilichotumika kuwa sh.milioni 288.
Utata kuhusiana na ununuzi huo unathibitishwa na habari za kuaminika kutoka ndani ya CHADEMA pale Mbowe aliposema anakidai chama hicho sh. milioni 188 ambazo aliongeza ili kununua vifaa, lakini ameshindwa kuonyesha risiti aliyotumia kulipa wakati wa kuviingiza nchini ili kuthibitisha madai yake. MZALENDO ilifichua kuwa mshahara wa Dk. Slaa ni zaidi ya sh. milioni saba ambazo ni nyingi kuliko za wabunge alizowahi kuzipigia kelele akidai ni nyingi, ambapo pia mshahara wa katibu mkuu huyo haukatwi kodi na TRA.
Baada ya kufichuliwa kwa taarifa hizo, Mkurugenzi wa Utawala na Fedha wa CHADEMA, Anthony Komu na Mjumbe wa Kamati Kuu, Mabere Marando waliitisha mkutano na waandishi wa habari kukanusha, jambo ambalo baadhi ya viongozi wa CHADEMA wamefichua kwamba ufafanuzi uliotolewa na viongozi hao ni wa uongo.
Habari zilisema Komu kudai Dk. Slaa analipwa mshahara wa sh. 1,725,000 na lita 1,000 za mafuta kila mwezi ni uongo wenye lengo la kutaka kuficha jinsi baadhi ya viongozi waandamizi walivyounda mtandao wa kutumbua fedha za CHADEMA.
MZALENDO ilifanikiwa kupata waraka ambao unaonyesha kuwa mapendekezo ya posho ya Dk. Slaa kama Azimio la Kamati Kuu iliyokaa Januari 29 hadi 30 mwaka huu, Dar es Salaam ni tofauti na maelezo waliyotoa Komu na Marando.
Kwa mujibu wa waraka huo ambao hauonyeshi kiwango kinachokatwa kodi, posho ya Dk. Slaa imegawanywa katika sehemu sita ambazo ni posho ya mwezi, fedha za mafuta, majukumu, viburudisho, nyumba na utendaji kazi.
Wakati Komu katika ufafanuzi wake alisema Dk. Slaa analipwa mshahara (basic) wa sh. 1,725,000 waraka unaonyesha analipwa sh. 2,300,000. Mbunge analipwa sh. 2,305,000 kabla ya kukatwa kodi.
Kwa upande wa posho, Slaa analipwa mafuta sh. 1,387,500 kwa lita 750 kwa mwezi huku fedha za majukumu zikiwa ni sh. 575,000, mawasiliano sh. 460,000 na nyumba sh. 1,000,000.
Posho nyingine ni kwa ajili ya viburudisho sh. 462,500 na utendaji kazi sh. 989,000. Mshahara huo umefanywa ni maalumu kwa Dk. Slaa pekee na iwapo chama hicho kitapata katibu mkuu mwingine hawezi kulipwa hivyo.
Dk. Slaa akiungwa mkono na Mbowe anadaiwa kujipatia posho ya nyumba mara mbili kwani ilishapendekezwa alipwe sh. milioni 40 kwa ajili ya kumalizia ujenzi wa nyumba yake eneo la Mbweni nje kidogo ya jiji la Dar es Salaam.
Licha ya kupewa fedha hizo, Dk.Slaa ameendelea kupewa posho nyingine ya nyumba ya sh. 1,000,000 kila mwezi huku akiwa tayari amelipwa na chama sh. milioni 40 kumalizia nyumba yake ambayo sasa anaishi.
Chanzo: Gazeti la Mzalendo, Mei 22, 2011
Kodi ni wajibu haina hiari!