Wahenga walilonga, miruzi mingi humpoteza mbwa na kuchamba kwingi mwisho kushika mavi.
Baada ya uchaguzi mkuu wa 2015,kamati kuu ya CHADEMA (CC) ilifanya kikao na kutoka na maamuzi ya kutoitambua serikali ya awamu ya tano inayoongozwa na Rais Magufuli.
Msimamo ulipigiliwa msumari na Wabunge wa kambi rasmi ya upinzani bungeni wakiongozwa na kiongozi wa kambi hiyo kutoka nje ya bunge wakatiRais akizindua bunge, ili kuonyesha msimamo wa kuipinga serikali iliyopoteza legitimacy kwa kutokuchaguliwa kihalali.
Dunia ilisikia na iliona athari zake kwa kuwa wawakilishi wa nchi nyingi wakiwamo mabalozi walikuwemo bungeni, hata serikali ilishtushwa na tendo lile.
Huenda tendo lile limchochea mtawala kujenga chuki ya dhahiri dhidi ya wapinzani, hususani kambi ya UKAWA kwa kuishughulikia ipasavyo kwa kuuwa nguvu yao kwa kuidhoofisha CUF na kuwatengenezea kesi viongozi wa CHADEMA.
Hapo ndipo zengwe la kuzuia siasa kwa Presidential Decree lilipotolewa, na udhaifu wa upinzani ulipoanza kujionyesha.
Nachelea kusema hivi kwa kuwa upinzani upo kwa mujibu wa katiba ya Jamhuri ya Muungano, na utekelezaji wa majukumu ya kisiasa yapo kwa mujibu wa sheria, unapozuiliwa kwa nguvu ya matamko kufanya siasa kwa muda anaoutaka mtawala, ukakubali badala ya kusimamia sheria ni mwendelezo wa uvunjaji wa katiba na sheria pia.
Wapinzani mbali na kulalamika wamekuwa wakitoa matamko mbali mbali katika kupinga ili kubatilisha matamko ya mtawala kuzuia mikutano halali ya vyama vya siasa bila mafanikio.
Kinacho sikitisha uhalali wa nguvu ya matamko ya mtawala yalijijenga kimatabaka na hii ni kutokana na udhaifu wa kimapokeo toka kwa wapinzani.
Matokeo yake CCM ikilindwa na vyombo vya dola ndicho chama pekee kinacho fanya siasa na hakikuathiriwa na nguvu ya matamko. Kwa kuwa nacho kama cha siasa hakikuona uhalali wa tamko la zuio hilo, japo walilindwa na nguvu ya dola.
Hilo ni kosa kubwa la kiufundi walilofanya wapinzani kuruhusu utekelezaji wa agizo la mtawala lililokosa mamlaka ya kisheria.
Inaeleweka duniani kote kuwa nchi zote zinazoamini kwenye tawala za mabavu, Presidential Decree ndiyo silaha yao bila kuzingatia decree hiyo inapora haki na misingi ya utawala bora.
Udhaifu na mapokeo ya wapinzani kukubali kutekeleza nguvu ya matamko ya mtawala, kumewafanya ndani ya miaka minne waishi kwa shida sana, kwa wafuasi wake na wale wote pro CCM kuteseka kwa njia mbalimbali kama kutekwa, kuumizwa, kuuwawa na kupotezwa bila kujulikana walipo mpaka sasa.
Kwa udhaifu huo huo wa matamko yasiyo na utekelezaji ya wapinzani, serikali chini ya mtawala iliendelea kucheza rafu nyingi hata kwenye chaguzi ndogo zilizo lazimishwa kufanyika, kwa nguvu ya ushaishwi wa rushwa ya madaraka (corruption of power) ili kudhoofisha nguvu ya upinzani katika kuhodhi mamlaka na kukifanya chama cha mtawala kushika hatamu japokuwa tulipo ingia kwenye mfumo wa vyama vingi ibara hiyo iliondolewa kwenye katiba, ili kukidhi mahitaji ya mfumo ya kusimamia haki sawa.
Pamoja na kuondolewa kwenye katiba ya Jamhuri ya Muungano, kwa awamu hii ibara hiyo imerudishwa kivitendo kama vile nchi ipo chini ya chama kimoja, leo kiongozi wa CCM anaweza kuingilia kazi za watendaji wa serikali ambao hawapo pale kupitia mwamvuli wa kisiasa bila kuzuiliwa na mamlaka yeyote hali inayo leta usumbufu mkubwa kwa watumishi wa umma.
Rais anasema, katibu mkuu wa chama anasema kila mmoja ana sharubu kwa kuwa tumekubalia mwingiliano usio na mipaka ya kiutendaji
Tumeona ukiukwaji mkubwa na upotoshaji wa uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa uliofanyika nchini, mchakato uliopelekea vyama vya siasa vya upinzani kujitoa kushiriki kwenye uchaguzi ulifanyika usiozingatia misingi ya demokrasia.
Kabla ya kujitoa kamati kuu za vyama vya upinzani zilifanya vikao vya dharura na kutoka na maamuzi ya kujitoa kushiriki uchaguzi huo, uamuzi ulioungwa mkono na watetezi wa haki nchini na uchaguzi huo ukiendelea kupigiwa kelele na wahisani ambao wakihoji misingi ya haki huitwa MABEBERU.
Pamoja na tamko la kujitoa ambalo ni mgomo(protest),kamati kuu ya CHADEMA ilisema mbali na kutoutambua uchaguzi huo, haitawatambua viongozi watakao teuliwa ama kuchaguliwa kwa kuwa taratibu za maandalizi ya uchaguzi yalikiuka sheria na kanuni za uchaguzi.
Watanzania wengi,wanachama na wapenzi wa CHADEMA waliwaelewa sana viongozi hawa, kwa kuliona hilo, athari zake zimeonekana.
Sehemu mbalimbali wananchi wamekataa kuwatambua viongozi waliopitishwa bila kupingwa, kwa kuulizwa wamechaguliwa na nani kwa kuwa msingi wa hoja yao unajengwa na ibara ya 8 ya katiba ya Jamhuri ya Muungano.
Wakati wananchi wakitekeleza haki yao ya kikatiba toka ibara ya 8,kamati kuu ya CHADEMA imetoka na tamko lingine la kushiriki sherehe za uhuru ambazo zitahudhuriwa na mtawala waliyekataa kumtambua kutokana na upatikanaji wake.
Lakini mtawala huyu ofisi iliyo wateuwa viongozi wa serikali za mitaa bila idhini ya ibara ya 8, inayotoa haki kuwa serikali itapata mamlaka na madaraka toka kwa wananchi iko chini ya ofisi yake.
Wakristo wanapo pata Kipaimara hutoa kiapo cha kumkataa shetani na mambo yake yote, hiyo ni kiapo cha vita dhidi ya mkristo na shetani.
Kamati kuu ya CHADEMA inakataa kuwatambua wateule wa TAMISEMI,ilikataa kuitambua serikali iliyoko madarakani lakini leo inayakubali mambo ya serikali kwa kupitia sherehe za Muungano kwa kuwataka wanachama wake washiriki kwenye maazimisho hayo,hii haingii akilini kama kiapo tu cha Wakristo kinamkataa shetani na mambo yake ninyi maovu yanayofanywa na serikali hii dhidi yenu mnayapa nafasi gani mbele ya wanachama wenu.
Ndiyo maana nimesema kuchamba kwingi mwisho kushika mavi.
Mnawaaminisha nini Watanzania baada ya viongozi wenu kushtakiwa kwa makosa ambayo siwezi yasemea kwa kuwa yapo mahakamani, baadhi ya viongozi na wanachama wenu kuuwawa bila juhudi ya vyombo vya dola kuwabaini wahusika, wanachama na baadhi ya viongozi wenu kutekwa!!
Haitoshi kusema mtashiriki maazimisho ya uhuru, tupeni sababu nini kimewasibu, kuzungumzia jumla jumla kuna outsmart kamati kuu kama chombo cha maamuzi ya chama.
Tunataka umadhubuti na misimamo isiyoyumba katika vita vya haki dhidi ya batili.
Tuelezeni kama mpo kwenye meza ya maridhiano wananchi wanapaswa kujua nchi ni yao na vyama ni vyao pia.