TAARIFA YA AWALI YA CHAMA JUU YA KINACHOITWA MATOKEO YA UCHAGUZI TANZANIA
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kinapinga vikali kinachoitwa matokeo ya uchaguzi yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi.
Matokeo haya hayana uhalisia wowote kwani ukweli ni kwamba hakukufanyika uchaguzi Tanzania.
Wananchi hawakushiriki katika uchaguzi wa Oktoba 29 kutokana na mazingira yasiyo huru, haki, na kukosekana kwa uwanja sawa wa kisiasa.
Aidha, Chadema tunasisitiza kwamba Tume ya Uchaguzi imetoa takwimu ambazo hazina uhalisia wowote zaidi ya kudhihirisha nia ovu ya Samia Suluhu Hassan na chama chake ya kuiba uchaguzi jambo ambalo walifanikiwa.
Chadema tumeeleza mara kadhaa msimamo wetu wa "No Reforms, No Election" (Hakuna Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi). Tulionya wazi kuwa bila marekebisho ya kweli katika mfumo wa uchaguzi, na sheria za kisiasa, uchaguzi huu usingeweza kuwa huru, wa haki, na wa kuaminika.
Maandamano yaliyoenea nchi nzima ni uthibitisho wa wazi kuwa wananchi hawakushiriki kwenye kile kinachoitwa uchaguzi na kutomkubali yeyeto anayetokana na mchakato huu mbovu wa kiuchaguzi.
Hivyo Chadema;
- Kutangazwa kwa matokeo leo ni mapinduzi ya wazi dhidi ya matakwa ya Watanzania ambao wamenyimwa haki yao ya kidemokrasia ya kuchagua kiongozi wanaomtaka.
- Haimtambui Samia Suluhu Hassani kama Rais wa Jamhuri ya Tanzania kwa kuwa hajachaguliwa na wananchi wa Tanzania.
- Inaishauri jumuiya ya kimataifa kutomtambua Samia Suluhu Hassan kama kiongozi wa Tanzania kwani hana uhalali huo kwa kuwa hajachaguliwa na wananchi wa Tanzania.