CHADEMA-Arusha yagundua madudu mengine yaliyofanyika kipindi cha CCM

Edward Sambai

JF-Expert Member
Nov 16, 2013
2,823
3,828
Kamati yagundua ufisadi mkubwa jiji la Arusha

TAARIFA ya Kamati ndogo ya Baraza la Madiwani wa Jiji la Arusha iliyoundwa kuchunguza uhalali wa ufutaji wa madeni ya mapato ya jiji hilo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita imegundua ‘madudu’ ya upotevu wa shilingi 843,137,112.00 za mapato.

Kamati hiyo iliundwa kama sehemu ya kutekeleza Azimio la Baraza la Madiwani katika kikao chake cha Mei 7, mwaka huu na kupewa barua ya uteuzi CD/C.90/11/171, Juni 16.

Kamati hiyo iliongozwa na Mwenyekiti wake, Epahata Nanyaro, ambaye ni Diwani wa Kata ya Levolosi (Chadema) na aliisoma taarifa hiyo juzi mbele wajumbe wa Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji la Arusha.

Wajumbe wengine wa kamati hiyo ni pamoja na Zakaria Mollel, Credo Kifukwe, Amani Reward, Ricky Moiro na vile vile ilisaidiwa kazi yake na wataalamu wa Halmashauri ya Jiji la Arusha ambao ni Kessy Mpakata, Amos Ackim na Tibilengwa Stephen.

Pamoja na upotevu wa kiasi hicho fedha, kamati pia imeainisha katika taarifa hiyo namna watendaji wa jiji walivyohusika kujumu mapato kwa kushirikiana wazabuni mbalimbali waliopewa kazi ya ukusanyaji wa mapato hayo.

Katika taarifa hiyo, Nanyaro alitaja kampuni saba zilizopewa zabuni ya kukusanya mapato ya halmashauri kutoka vyanzo mbalimbali katika mwaka fedha 2010/2013 zilizofutiwa madeni yanayofikia shilingi 843,137,112.00 kinyume cha sheria na katika hali inayoashiria vitendo vya ufisadi.

Kampuni zinazodaiwa kusamehewa kulipa madeni hayo katika taarifa zimetajwa kuwa ni Mkomilo Trade Centre (T) Ltd (Sh 29,139,000) iliyokuwa inakusanya ushuru wa mabasi madogo (daladala), Makumira Filling Station (Sh. 18,500,000) iliyokuwa imepewa zabuni ya kukusanya ushuru wa maegesho ya magari.

Kampuni nyingine ni M/S Pigadeal Investment Ltd (231,000,000/-) iliyokuwa ikikusanya ushuru wa Soko la Kilombero, Jamahedo Health Food Company (256,510,032.00/-), ushuru wa maegesho ya magari, Aquiline Traders Ltd (27,485,500.00/-), Mkomilo Traders Centre Ltd (50,906,100.00/-) na New Metro Merchandise Ltd (229,599,480.00/-).

“Kamati ilibaini uzembe mkubwa uliofanywa na watumishi wa halmashauri kuanzia hatua ya utoaji zabuni hadi utekelezaji wa mikataba ya wazabuni hao,” alisema Nanyaro na kuongeza; “Kamati imebaini wazi kuwa ulikuwapo uzembe wa hali wa juu katika suala zima la usimamizi wa mapato ya halmashauri kwani inaonekana watumishi walitanguliza mbele maslahi binafsi badala ya umma.”

Alisema kamati pia imebaini udhaifu mkubwa katika idara ya sheria ya jiji hilo kwa kushindwa kuwajibika ipasavyo, katika uandaaji na usimamizi wa mikataba ama kwa makususdi au kwa uzembe, mikataba iliyoandaliwa haikuwa na vipengele vya kuilinda Halmashauri ya Jiji la Arusha kisheria.

“Halmashauri ilipata hasara na kupoteza mapato yake, jinsi ofisi sheria iliyosimamia uandaaji na usimamizi wa mikataba inaoonesha dhahiri kuwa mwanasheria alikuwa na uhusiano wa karibu na mawakala (wazabuni) na kwa kutumia taaluma yake alihusika kutengeneza mazingira mbalimbali kuhujumu mapato ya halmashauri,” alisema mwenyekiti huyo.

Kwa mujibu wa mwenyekiti huyo, kamati yake pia ilibaini pia kuwapo kwa viashiria vya rushwa katika mchakato wote wa ukusanyaji mapato na kufutwa kwa madeni hayo na kwamba, mfumo mzima uligubikwa na mgongano wa maslahi.

“Madiwani na watumishi wa halmashauri ndio waliokuwa wamiliki wa idadi kubwa ya maduka na hivyo kufanya kazi ya kukusanya mapato na ushuru kuwa gumu. Wajumbe wa kamati mbalimbali za Baraza la Madiwani, kwa wakati huo, zilizoundwa kumaliza migogoro walikuwa na malsahi ya kibiashara ama walijihusisha na rushwa,” alisema.

Kamati hiyo imependekeza kuwa kutokana na mazingira ya utata yaliyogubika utaratibu mzima wa kufutwa kwa madeni hayo, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), ifanye uchunguzi na hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya watumishi na kamapuni hizo.

“Kwa vile watumishi wote wakiwemo mkurugenzi, mwanasheria, mweka hazina na afisa manunuzi waliokwapo wakati huo wamekwishahamia sehemu nyingine, mawasiliano yafanyike ili hatua za kinidhamu zichukuliwe dhidi yao kwa uzembe na kushindwa kuishauri halmashauri na kuisababishia hasara,” yanasomeka mapendekezo ya kamati hiyo ndogo ya baraza la madiwani.

Nanyaro katika taarifa yake anapendekeza kuwa halmashauri ihakikishe mikataba, hasa ya ukusanyaji wa mapato inakuwa na kipengele kinachoweka masharti kwamba unapotokea mgogoro yafanyike majadiliano (arbitration) na migogoro hiyo imalizwe kabla kesi kupelekwa mahakamani.

Pia wamependekeza kampuni zote zilizohusika ambazo kimsingi zimekosa uaminifu zizuiwe kufanya biashara na halmashauri (black listed) na wamiliki wa kampuni hizo pia wasiruhusiwe tena kufanya kazi na halmashauri hiyo.

Akizungumza baada ya kusoma taarifa kwa waandishi wa habari, Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Zakaria Mollel ambaye ni Diwani wa Kata ya Olorien, alisema taarifa hiyo pia wataikabidhi kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, ili atoe maelekezo kwa Takukuru kuanzisha uchunguzi dhidi ya waliohusika.

“Kwa kuwa Mkuu wa Mkoa amekuja na kasi mpya ya kufanya kazi na sisi tunampa ‘homework’ ya kufanya. Kwa kutumia vyombo vya ulinzi na usalama vilivyoko chini yake basi ahakikishe wahusika wanachunguzwa na kuchukuliwa hatua,” alisema.

Kwa upande wake Meya wa Jiji la Arusha, Kalist Lazaro, alisema ni wajibu wa serikali kuwachukulia hatua wahusika.

“Kama nilivyoeleza mara nyingi kwamba katika miaka iliyopita Halmashauri ya Jiji la Arusha ilihujumiwa sana kutokana na usimamizi mbovu kuanzia kwa Baraza la Madiwani hadi watendaji wake lakini chini ya uongozi wangu nitahahakikisha kuwa mambo kama hayo hayatokei tena,” alisema meya huyo.

Juhudi za kumpata Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, Athuman Kihamia, ambaye hata hivyo aliteuliwa mwezi uliopita kushika wadhifa huo hazikuzaa matunda kama ilivyokuwa wakati wa kumtafuta Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo.

Chanzo: Raia Mwema
 
Back
Top Bottom