Ccm ya kikwete ikome kusingizia udugu na tanu ya nyerere! | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Ccm ya kikwete ikome kusingizia udugu na tanu ya nyerere!

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by KAMBOTA, Jul 12, 2011.

 1. K

  KAMBOTA Senior Member

  #1
  Jul 12, 2011
  Joined: Mar 21, 2011
  Messages: 176
  Likes Received: 6
  Trophy Points: 0
  [​IMG]
  Na Ilunga Msekela Mpambanaji,


  Wakati tunazidi kuhesabu siku za mwaka huu 2011 kuna mambo kadha wa kadha ambayo watanzania wanayazungumza , watanzania wengi ukiacha wale wenye nacho huwa na sura za huzuni kila wanapoangalia nchi yao inavyokwenda kiholelaholela kama sio kimzobemzobe ,ukiwa ndani ya daladala utasikia watanzania wakilalamikia umasikini wao, ukisoma magazeti mbalimbali hasa yale makini ndiyo yale makini tu kwani nani asiyejua kuna magazeti hapa kwetu yanafanya kazi ya kulinda utawala mbovu badala ya kuukemea?,utakuta kwenye safu zao hawa waandishi makini nao wakihoji kulikoni umasikini wa watanzania kwenye nchi yenye utajiri wa kutisha wa maliasili?.


  Hali ya huzuni ya watanzania haikuanza leo wala jana, haijatokea kwa bahati mbaya au hasira za Mungu hapana kabisa hali hii ni matokeo ya watawala kujitenga na umma, hivyo tunapozidi kuelea ndani ya mwaka huu 2011 ambao kwanza ni mwanzo wa mwongo mpya pia kwa upande mwingine ni safari moja mbele kuelekea uchaguzi mkuu wa 2015 ni muuhimu tukajadili bila kificho mustakali wetu na taifa letu. Hivyo kimsingi mfululizo wa makala hizi utachambua kiundani tofauti kubwa iliyopo kati ya chama cha wazalendo cha TANU kilichopigania uhuru wa Tanganyika kilichoongozwa na mwanamapinduzi Julius Nyerere na hiki kinachoitwa chama cha mapinduzi au kwa kifupi CCM kinachoongozwa na Jakaya Kikwete ambacho watanzania wanakihoji juu ya umasikini wao huku wenyewe wenye CCM yao wakizidi kuneemeka .

  Hebu sasa tumulike na kuchambua kiundani tofauti iliyopo kati ya TANU ya wazalendo na CCM ya sasa ya matajiri. Tofauti ya kwanza kati ya vyama hivyo labda ni nyakati , wakati TANU ilianza wakati wa ukoloni , CCM imekuja baada ya uhuru mwaka 1977 hii tayari inatupa picha halisi kuwa wakati wana TANU wanaujua uchungu wa kupigania uhuru na walishiriki mapambano hayo ya kufa na kupona , wana CCM wao wanafaidi matunda ya uhuru pasipokujua ulipatikana vipi. Hapa kuna hoja ya msingi inayoibuka kuwa mbona CCM ni matokeo ya TANU na ilitokea baada kuunganishwa ASP na TANU na hata wanachama wake walikuwa walewale wakiongozwa na Mwalimu Nyerere iweje mimi nidai TANU siyo CCM? , kwanza kabisa tujiulize ikiwa CCM kwa upande wa Tanzania bara ndiyo TANU je vipi kwa ndugu zetu wa visiwani?

  Je ni kweli kuwa ASP ilistahili heshima hiyo? Nani hajui mkanganyiko wa kihistoria uliopo visiwani humo? Je ni nani kati ya Okello, Karume ,Umma party na ASP alistahili kushiriki kuunda CCM pamoja na TANU? Au tuliache hili hebu tuangalie upande mwingine wa hili, fikiria Jakaya Kikwete alikuwa wapi hiyo mwaka 1961 wakati nchi inapata uhuru? Sembuse miaka ya 1950 wakati hizo harakati za uhuru zikipamba moto? Lakini mimi si mfupi wa mawazo kwani hata hao akina Bill Clinton au Kennedy wa Marekani ambao wanatajwa katika orodha ya mashujaaa wa taifa hilo hawakuwepo hiyo mwaka 1776 wakati Gorge Washington akiapishwa kuwa rais wa Marekani lakini ukiwauliza wamarekani kuwa kwanini viongozi hao walifanikiwwa kufuata nyayo za mwasisi wao? Jibu la moja kwa moja ni kuwa viongozi hao walitamani kufanya au kuwa bora zaidi ya Washingtton lakini pia walisoma alama za nyakati za wakati wao, hawa walikuwa tayari kujifunza na pia walidiriki na kuthubutu kufanya yale ambayo hayawezi kuitwa vingine bali mambo ya kishujaa.

  Sasa hebu tugeeukie kwetu hapa nyumbani je Kikwete na wenzake kweli wanatamani kufanya kama Mwalimu Nyerere? Je wapo tayari kujifunza historia ya nchi hii na watu wake? Wapo tayari kukubali ukweli hata kama unauma( accepting the truth even though it is bitter to swallow), na sio tu Kikwete na wenzake watuambie kuwa wanataka kuwa kama Nyerere kwa maneno mepesi mepesi tu bali iinabidi tuone kupitia matendo yao kuwa kweli wamedhamiria kuwa kama Mwalimu na hata kuzungumza na sura Zao pia ziibebe dhana ya Unyerere lakini hiyo haitoshi kuna hili la kusoma alama za nyakati ili historia iwakumbuke kama ilivyo kwa Nyerere na wenzake ambao historia ya taifa hili inawakumbuka.


  Sasa tufanye hesabu za kawaida za kujumlisha na kutoa tu ambazo hazimhitaji mtu kuwa na degree ya chuo kikuu cha Mlimani, Mzumbe au Dodoma kuhusu CCM ya sasa ya Jakaya Kikwete na wenzake. Hivi ni nani kati ya Kikwete na wenzake anaweza kujigamba hadharani kuwa kweli anamuenzi huyo Nyerere sembuse hiyo CCM ya Kikwete kama itaweza kusema kwa sauti bila kumumunya maneno kuwa kweli imeendeleza yale mema aliyoyaacha Nyerere. Hebu nenda Tanga ambapo Nyerere alipafanya kitovu cha viwanda vya wazalendo nenda kule mtaa wa viwanda kule Tanga sasa hivi halafu utaamini kuwa Nyerere na fikra zake zote zilishazikwa pale Butiama haya CCM inayojidai ni kumuenzi kila tarehe 14 oktoba ni kumzuga mtoto ili aache kulia wakubwa waendelee na mambo yao, kama nikipewa nafasi ya kuwashauri wakazi wa Tanga basi nisingewaficha kuwa waache kujidanganya wenyewe kwa kuuita mtaa huo kuwa wa viwanda bali uitwe ni mtaa wa magofu kwa kuzingatia ukweli kuwa yaliyobaki huko ni magofu tu sio viwanda hata kidogo, huu ni mfano mdogo tu kati ya mingi inayoonyesha kuwa CCM ya Kikwete haina uhusiano wa kimantiki, matendo, dira, maono, kifalsafa,kiitikadi wala ushabiki kwa TANU wala huyo Nyerere hata kidogo.


  Hebu tupime Nyerere aliacha taifa gani? Kweli alituachia taifa la wahuni na wavuta bangi?, alituachia taifa la mafisadi na mapapa na manyangumi wa kupora mali za taifa? Nyerere alituachia taifa lililogawika kwa misingi ya udini ambapo viongozi wanatumia udini huo kama mtaji wao kisiasa bila kujali athari zake .Hivi kweli Mizengo Pinda kautoa wapi ujasiri wa kutangaza hadharani kuwa serikali ipo tayari kulipa Billion 185 kama fidia kwa kampuni tata ya kufua umeme ya Dowans? eti kuwa serikali na TANESCO wameshindwa kesi kwa kuvunja mkataba. Na wakati huohuo Mizengo Pinda huyu huyu anawachezea watanzania akili kwa kutangaza mali zake huku akitaka umma wa watanzania masikini wa kutupwa umfananishe na nabii wao Nyerere. Hivi yeye Pinda na Kikwete wanadhani kuwa watanzannia hawajui ukweli kuwa hii fidia tunailipa kwa mengi sio tu kwa kushindwa kesi na ikizingatiwa kuwa ni lazima tulipe fidia na ilikuwa ni lazima tushindwe kesi hiyo hata kama Mungu angetushushia mawakili kutoka mbinguni.


  Hivi sio Nyerere inasemekana hakutaka upuuzi wa aina hii kwa kigezo cha utawala bora au kuheshimu mahakama. Siongei vitu kwa kukurupuka bali na uhakika kabisa na hili kuwa Nyerere hakutaka mchezomchezo wa aina hii, katika moja ya hotuba zake Nyerere anasema kuwa aliwahi kumshauri Laurent Kabila kugoma kulipa madeni ambayo Kongo iilikuwa ikidaiwa na Ubelgiji ambayo yeye kabila aaliyarithi kutoka kwa mtangulizi wake Mobutu Sese seseko ambayo kwa maneno ya Nyerere ni kuwa pesa hizo Mobutu alizificha hukohuko Ubelgiji sasa iweje tena Kabila azilipe kwa kutumia kodi za wanakongo? Sasa inakuwaje hii serikali ya CCM inalipia deni la kutengenezwa kwa kodi za watanzania masikini? Kwanini kama wao wakubwa wasipokee mishahara, wauze mahekalu yao, warudishe watoto wao kutoka Ulaya waje wasome shule zetu za kata na kupunguza kula kwenye mahoteli ya Nyota tano ili wajichangechange wawalipe hao Dowans kuliko kutumalizia hazina yetu ya taifa kwa madeni ya kupewa?.


  Ukisoma kitabu cha The Modern World since 1870 page 240 katika sura inayozungumzia bara la Afrika ambayo imepachikwa jina la The Impossible Dream yaani ndoto isiyowezekana mwandishi Snellgrove katika aya kwanza anaandika hivi “The first contact between Europeans and Africans was unhappy. White traders came to west Africa to seize slaves and take them to the west Indian and North American plantations. They brought manufactured goods,cloth and tin kettles, which the African chiefs wanted. At first they received in return criminals and prisoners of war. Later the chiefs seized people of other tribes”……..hapa mwandishi Snellgrove anamaana kuwa mahusiano ya kwanza kati ya wazungu na waafrika yalikuwa ya kuhuzunisha.Wafanyabiashara wa kizungu walikuja Afrika magharibi kukamata watumwa ambao waliwapeleka kufanyakazi kwenye mashamba huko Marekani,wafanyabiashara hao wa kizungu walileta bidhaa za viwandani, nguo na mabirika ambayo watawala wa kiafrika waliyahusudu sana, mwanzoni watawala wa kiafrika wakabadilishana kwa kuwatumia wahalifu na wafungwa wa kivita baadaye watawala hao wakaanza kuvamia makabila mengine ili kupata watumwa wa kubadilishana na wazungu.


  Hapa tunaona mambo makuu matatu ya msingi la kwanza ni kuwa bidhaa zile zilizoletwa na wafanyabiashara wa kizungu zilipendwa na watawala na sio wananchi wa kawaida, pili watawala hao wakawa wakiuza wafungwa baadaye wakaaanza kuvamia makabila mengine ili kukamata watumwa , tatu mahusiano haya yalikuwa ya huzuni kubwa na hapa bila shaka wahanga wa huzuni hiyo walikuwa wananchi wa kawaida na sio watawala. Sasa hii CCM ambayo inaongozwa na Kikwete na wenzake ndipo ilipofikia kuwafanya watanzania, kwanza imewagawa katika makabila makuu mawili ya walionacho na wasionacho , halafu ndio sasa inapokuja mikataba mibovu kama ya Richmond , Buzwagi na kule Loliondo ambako bila shaka wananchi ni wahanga wa uharibifu wa mazingira na umasikini wa kutupwa unaosababishwa na uwekezaji haramu wa mabeberu wa ulaya na marekani lakini kwa upande mwingine hii ni faida kubwa kwa CCM ya Kikwete na serikali yake kwani ndio uwekezaji huu umewafanya baadhi ya wakubwa kuwa na utajiri wa kutisha.  Kweli CCM ya Kikwete, Pinda na wenzao haina hadhi ya kujihusisha na Nyerere na TANU yake sembuse kujinadi kwa kutumia jina la kiongozi huyo aliyezaliwa na umasikini wake , akakaaa Ikulu miaka 24 akwatumikia watanzania kwa moyo wote akatoka na umasikini wake kama alivyoingia akasahau hata kujenga nyumba masikini mpaka pale Jeshi letu lilipomjengea nyuma mzee huyu. Nyerere na TANU yake walichukia rushwa hata kwenye amri kumi za TANU iliandikwa waziwazi kuwa rushwa ni adui wa haki na hata kina Mzee Gorge Kahama wanafahamu jinsi gani Nyerere na Sokoine walichukia na kupiga vita rushwa. CCM ya leo ina ubavu gani wa kujiita yenyewe ni matokeo ya TANU? na kwa mapana yapi? , mantiki na kwa hoja zipi?


  Najua wapo baadhi ya wafuasi wa CCM ambao wanaujua ukweli kuwa chama chao cha sasa hakina mashiko wala ujazo, hakishabihiani wala kuoana na TANU ya Mwalimu Nyerere lakini ndiyo hivyo tena wanaogopa kusema wakijua fika kuwa kusema ukweli ndani ya chama hiko ni uasi mkubwa, watafukuzwa na kutengwa pasipo kujua kuwa Mwalimu Nyerere alipenda ukweli na kuuishi daima. Hawa hawajui kuwa Taifa ni la kwanza kabla ya CCM yao. Kwa jinsi CCM ya sasa ilivyo ni kama vile mlinzi aliyesahau lindo, naona wana CCM wa sasa wanajadili mazuri ya TANU na Nyerere huku wanaishi unafiki na kuleana kifisadi bila shaka hawa wanalielezea yai bila kumtaja kuku aliyetaga yai hilo bila shaka wamepotea kabisa hawasomi alama za nyakati wangekuwa wanasoma alama za nyakati basi wangegundua kuwa CCM ya sasa imeshautupa ule mkebe wa siasa adilifu za TANU, umelitupa hata Azimio la Arusha tumaini la wanyonge na imekumbatia ubeberu ambao kimsingi haufanani hata na ule wa magharibi. Kutoka TANU ya Nyerere ambapo mali na utajiri ilikuwa first disqualification ya kumzuia mtu kuwa kiongozi mpaka CCM ya Jakaya Kikwete ambapo mali na utajiri sasa ni first qualification ya mtu kuwa kiongozi ingawa bado chama hiko hakijatangaza rasmi na sijui kinangoja au kuogopa nini?  Yaelekea CCM wamesahau kuwa baba wa taifa aliwahi kusema waziwazi kuwa CCM si mama yake mzazi badala ya kuona chama hiko kikizidi kupotoka na kuacha misingi ya TANU, lakini hili ni moja kubwa zaidi ni kuwa waliojenga CCM hii ya sasa ambayo hatujui baba wala mama yake ni wale waliolelewa kwenye mikono ya mzee huyu ambaye bila shaka watanzania wataendelea kumlilia kwa miaka mingi ijayo , kama kweli kaburini kuna maisha basi ni dhahiri kuwa Nyerere anapindukapinduka kwa uchungu mkubwa kuona watu aliowaamini ndiyo wamemsaliti na sina hakika kama watu hawa wanaijua njia ya kwenda Butiama alipolala mzee huyu ambaye alijenga taifa lenye kujali utu kabla ya wachache kuligeuza la wapenda fedha na vitu.


  Ukipitia nukuu maarufu ya mwanafalsafa na mwanazuoni maarufu Neale Donald Waisch akizungumzia matendo ya watawala anasema “people will not remember what you said, but how you made them feel” akiwa na maana kuwa watu hawatakukumbuka kwa maneno yako bali utakumbukwa kwa jinsi ulivyowafanya wajisikie, haina ubishi kuwa TANU na Nyerere walilijua hili wakafanya walivyoweza kuhakikisha kuwa watanzania tunajisikia tuna chama chetu,nchi yetu na zaidi viongozi wetu makini wakiongozwa na mpenda maendeleo na mwanamapinduzi wa bara la Afrika hayati Mwalimu Julius Nyerere, hakuna ubishi kuwa Nyerere alifanya maammuzi yenye tija kama Herman Simon anavyoeleza kwenye andiko lake maaarufu la “The rational decision” au kwa Kiswahili uamuzi wenye tija, Nyerere alianzisha Azimio la Arusha akajenga utu na utaifa ambapo watu walitambuana kwa utanzania wao na wala sio dini, makabila wala tofauti za kipato.


  Sasa kwa mikataba hii mibovu ya wizi na ufisadi wa kutisha nachelea kusema kuwa CCM hii ya sasa hata kama kuna mmoja wao anafahamu maana ya uamuzi wenye tija achilia mbali kuthubutu kufanya uamuzi huo wenye tija kama Nyerere alivyofanya. Hata kwa dawa na sauti za malaika za vinubi na vinanda CCM ya Jakaya Kikwete haiwezi kumshawishi hata mtoto mdogo kuwa ina uhusiano wa kindugu nna TANU ya Julius Nyerere ambayo iliwataka watanzania kufanya kazi na kujitegemea huku Nyerere akisisitiza na kusema waziwazi kuwa ni lazima watanzania wakubali kuwa maendeleo ni mtoto wa taabu lakini leo hii kila mtanzania ni shahidi kuwa CCM ya Jakaya Kikwete inaawalemaza na kuwapumbaza watanzania kwa kuwaaminisha kuwa maendeleo yataletwa na wawekezaji kutoka nje huku mwenyekiti wake Jakaya Kikwete akiranda huku na kule kutoka anga la nchi moja mpaka nyingine akiomba misaaada na kuhimiza wawekezaji wa kigeni kuja nchini. Kwa makala yangu hii haina ubishi kuwa makada wa chama cha mapinduzi CCM wameanza kuhofu uhai wa chama chao wasiwe na hofu hii ni rasharasha tu mvua yenyewe inakuja, kama ngoma hii ni lele ndio kwanza barafu imeanza kuyeyuka wangoje 2015 wapate kichapo kitakatifu.
  Sasa ngoja nijikite kwenye upofu huu wa CCM ya sasa huku nikijadili zaidi kivipi na kwajinsi gain CCM imefika hapa ilipo ambapo wananchi wameibatiza jina la chama cha mafisadi.


  Kwanza kabisa CCM imefika hapo ilipo kwasababu ya kuleana , kuleana huku kwa CCM kumezaa mfumo wa kitabaka kwa maana viongozi wakubwa wa chama hiko wameunda tabaka lao linalokwenda kwa jina la vigogo ambao wenyewe wapo juu ya sheria, wamejivika umiliki wa maliasili zetu , hawa ndio mabingwa hasa wa mikataba mibovu katika kila nyanja na mwisho wa siku tukiwabamba hawaachi kuanza na kujiuzulu huku wakitudhihaki na kutuchombeza na kawimbo kao ka kijinga kuwa waeonewa na kudhalilishwa sana nafikiri hili halina ubishi hata mkutugenzi wa TAKUKURU Edward Hosea anafahamu na anajua waziwazi kuwa Tanzania kuna untouchables ambao kama mwenyewe alivyonukuliwa na mtandao wa Wikileaks week kadhaa zilizopita kuwa kundi hili ni kama vile rais aliyoko madarakani anawalinda kama sio kutoonyesha nia dhati kuwa anataka washughulikiwe kisawasawa badala yake amekuwa akifanya akifanya kila awezalo kuwalinda hawa watu.


  Pili kuna urafiki ambao bila shaka ni kutokana na kujuana ambako kumezaa mfumo wa kindugu ndani ya chama hiko hadi serikalini, mwanaharakati maarufu na mwandishi Nigeria Kenny Sarro Wiwa aliuwawa kinyama na dikteta na rais wa zamani wan chi hiyo San Abacha , katika moja ya nukuu zake akielezea hatari ya urafiki baina ya viongozi Sarrowiwa anasema…..we do not mind the rulers to be friends what we seek to know is for what reasons they become friends….kwa tafsiri ya Kiswahili ana maana kuwa hatujali watawala kuwa marafiki bali tunachohitaji kujua ni sababu zipi zimewafanya kuwa marafiki. Hii ndio sababu hatuchukii urafiki wa Kikweate na Lowassa au urafiki wake na Rostam Aziz na Andrew Chenge , sisi tunataka kuzifahamu sababu za msingi za urafiki wao, hizi tunazijua kwa kuangalia matendo yanayowahusisha pamoja hapa ndipo watu wenye kuipenda nchi yao wanahoji iweje Lowassa atuibie kupitia kampuni tata ya kufua umeme ya Richmond lakini tunapozwa kwa kujiuzulu tu uwaziri mkuu na mwenyekiti wa CCM Jakaya Kikwete akimwinua mkono wakati wa kamapeani akimwombea kura kule Monduli huku akiwachombeza wamasai kuwa hakuna kama Lowassa sasa sijui hakuna kama Lowassa kwa nini? au kwa rekodi mbaya ya kutajwa kwenye kashfa ya rushwa?. Au huyu mbunge wa Igunga Rostam Aziz anapohusishwa na kampuni ya kitapeli ya Dowans halafu mwisho wa siku Kikwete anamwombea kura huku akimsifia kuwa ni kiongozi bora, sasa kwa mazingira kama haya ndipo tunabaini kuwa urafiki wa Kikwete na Lowassa na Rostam Aziz si mwema kwa taifa letu kwani urafiki huu ni kwaajili ya ulaji tu na mwisho wa siku tunawaona watu hawa wakiendelea kutesa huku Edward Hosea na TAKUKURU yake wakikamata visamaki vidogo na kuacha manyangumi.

  Katika hali kama hii wanapoibuka watu wenye mapenzi mema na nchi yao kama Dr Slaa na kuongea hadharania bila kificho akimtaja moja kwa moja Kikwete kuwa mhusika wa Dowans na kumtaka ajiuzulu wanaibuka watu walioshiba na kusahau shida za wamama wajawazito pale Amana au shida za makuli pale bandarini anaibuka bila aibu na kudai kuwa rais Kikwete hausiki hivi yeye Salva Rweyemamu nani kamwambia sisi ni darasa la kwanza tunaoridhika na majibu ya kweli na hapana , kwa taaluma yake ya uandishi wa habari sikutegemea atoe jibu jepesi kwa hoja nzito kama ile ya Dr Slaa. Rweyemamu ilibidi ajibu hoja ya msingi kama sio kumwacha kikwete mwenyewe atuambie kinagaubaga ni nani haswa mhusika wa Dowans? na kwanini hachukuliwi hatua?. Huu ni ushahidi mwingine kuwa mfumo wa kirafiki umewafikisha hapo walipo kina Kikwete yaani sisi tunalipia gharama za uswahiba wao kwa jasho na damu yetu. Kikwete kama kweli yeye ni msafi kwanini asiwaadhibu watu hao? au kuwataja hadharani au anaogopa mchezo wa kurushiana mawe ilihali eye mwenyewe yuko kwenye jumba la vioo?.

  Mpaka leo unajua siamini na sitaki kuamini kuwa Kikwete alisimama hadharani mbele ya vyombo vya habari akiwataka mafisadi waliokwapua hela kutoka akaunti ya madeni ya nje EPA warudishe pesa hizo, hivi kweli hizi ndizo hatua alizopaswa kuchukua kupambana na ufisadi , huyu ndiye Jakaya Kikwete bwana anayeamini kuwa adhabu ya mwizi ni kurudisha alichoiba basi.


  Halafu mtu huyuhuyu tunapomtaka kuwafikisha mafisadi mahakamani yeye anadai anaheshimu mahakama sasa huwa najiuliza labda kikwete huwa ana msimu maalumu wa kuheshimu mahakama kwa maana kama madai yake ya kuheshimu mahakama ni ya kweli je kwanini hakuacha mahakama ichukue hatua? yeye akaingilia maamuzi ya mahakama kuunda katume kake ambacho hata hivyo ni kama kufunika kombe ili mwanaharamu apite kwani hatujui chochote kilichoendelea na yeye alijigeuza hakimu kwa kuwataka watu hao kurudisha mapesa hayo waliyokwapua. Sasa hii haitoshi sasa hivi kikwete huyuhuyu leo katuundia tume ya katiba, hivi najiuliza kama kweli mtu huyu anaheshimu mamlaka ya Bunge kwanini asliache bunge lifanye kazi yake ya kuunda tume hiyo?,

  Nani alimwambia kikwete atuchagulie watu anaowajua yeye kutusimamia kwenye kuandika katiba?, nani kampa mamlaka na kiburi hiki?, labda nichukue nafasi hii kumwambia kuwa hiyo tume hatuitaki hata kidogo nafikiri hiyo itusaidie kuishinikiza serikali yake kuwakamata na kuwafungulia mashtaka mafisadi na pia kumchunguza yeye mwenyewe kuwa ana usafi kiasi gain lakini swala la katiba tuachiwe wenyewe tulifanye yeye akae chonjo la saivyoa hiyo katiba si yetu ni yake na tume yake aliyoiteua. Huu ndio uswahiba naosema umeiharibu CCM hivi ni Kikwete anajua madhara ya ufisadi anajua kwa kiasi gain sisi masikini tunateseka huku hao maswahiba zake anaowalinda wakiendelea kunawiri kwa pesa haramu. Hivi kama kweli Kikwete anachukia ufisadi asiwaadabishe kina Lowassa na Rostam Aziz au kina Andrew Chenge cha ajabu kiwete, panda na Bilal wotea wanaulaani ufisadi kwa kauli kalikali na kulaani mafisadi wote na kuwataka waachie ngazi lakini mbona hawawataji hao mafisadi au hata kututajia herufi za kwanza za majina yao kama wanawaogopa yaani hapa sielewi kabisa ufisadi ni nini au mafisadi mbona hawatajwi wanaogopwa au ndio hivyo tena hawagusiki the untouchables hii haitoshi bado hawa mafisadi ni watu muhimu kwenye chama hiko huku wakishiriki na kuonekana mashujaa kwenye vikao na ndani ya chama hiko, huku kina Makama wakiwapamba kama mashujaa na kusahau mashujaa wa kweli kama Nyerere na Sokoine sasa hapa kwa mantiki ya kawaida najiuliza tu mtu unawezaji kupinga ukatoliki huku ukiendelea kubusu pete ya papa , kwanini basi CCM wasiwafukuze au kuwachukulia hatua watu hawa, nani wa kufanya hivyo wakati urafiki umetawala ndani ya CCM na serikali yake.


  Ukisoma kitabu cha Chinua Achebe kinachoitwa A man of the people ukurasa wa 194 paragraph ya tatu inasema ….he who that knows not and aknows not that he knows not is a fool….ina maana kuwa yule ambaye hajui na hajui kwamba hajui ndiye haswa mjinga, hivi ni nani hajui kwamba hajui ni CCM au wanaoipinga CCM, akina nani kati ya Rweyemamu na Dr Slaa hajui ukweli? , bila shaka ipo wazi kuwa Kikwete, Rweyemamu na CCM yao hawajui halafu hawajui kuwa hawajui . Hawajui jinsi watanzania tulivyo na uwezo wa kupambanua pumba na mchele, hawajui kuwa tunajua kwanini Kiwete hawezi kuwachukulia hatua mafisadi, hawajui kuwa watanzania tunataka manadiliko , hawajui kuwa tumechoka na ufisadi tunataka siasa za kiungwana na uadilifu kweli wameachwa na wakati hawajui kuwa watanzaia tumechoka kuonewa na mfumo gandamizi na uhafidhina wa CCM.


  Tatu ni matumizi ya nguvu dhidi ya wananchi, kwa hili CCM wanapaswa kulaaniwa kama sio kuzomewa hadharani kabisa. Najaribu kujiuliza hivi ni nani kawafundisha CCM na serikali yake kugeuza vyombo vya usalama kutoka kuwa walinzi wa raia na mali zao mpaka kuwa walinzi wa watala na maslahi yao?. Hivi najaribu kuvuta picha ambazo bado hazijafutika kwenye ubongo wangu za wanafunzi wasio na hatia wa chuo kikuu cha Dodoma na Ardhi wakipigwa mobumu ya machozi wakati wakidai haki yao kabisa au navuta picha ambayo itachukua miaka mingi kufutika kwenye fikra za wapenda amani wa Tanznia, picha za wanachama wa CHADEMA mkoani Arusha wakiandamana kwa nia ya kupinga siasa za majitaka na kuhimiza katiba mpya huku mikononi wakiwa hawana bunduki wala mapanga bali mikono safi iliyobeba ujumbe mtukufu wa amani mara wanavamiwa na polisi na kupigwa mabomu ya machozi na risasi za moto huku baadhi yao wakipoteza maisha na wengine kujeruhiwa vibaya. Hivi nani aliwaambia CCM na serikali yao kuwa Said Mwema na jeshi la polisi ni kwaajili ya akutimiza masalahi yao ya kisiasa?, hivi hawajui kama walichomshinikiza kukifanya Said Mwema ni dhambi kubwa na kinyume cha haki za binadamu na hakivumiliki hata kidogo?, kwanini watu hawa wasijiuzulu na kujipeleka wenyewe mahakamani , au wanasubiri Yesu arudi aje awaumbue?.


  Ukisoma kitabu cha The World’s Greatest Speeches cha mwandishi Jasvinder kaur ukurasa wa 183 katika speech ya I Have A Dream ya mwanahatrakati Martin Luther King Jr paragraph ya tatu Luther King anasema kuwa ….We refuse to believe that the bank of justice is bankrupt….akimaanisha kuwa hatutaki kuamini kuwa benki ya haki imefilisika. Ndiyo hata kina Said Mwema wapotumia risasi za moto na mobomu inapaswa wajue kuwa watanzania hatuamini kuwa benki ya haki zetu imefilisika, hatuamini na kamwe hatutaamini mpaka tuone nchi hii inakuwa ni ya haki na watu wanaishi kwa amani ya kweli siyo amani ya kulazimishwa kwa mtutu wa bunduki au kupumbazwa na CCM huku wenyewe wakineaemeka na kwenda kutumbulia vipele Berlin Ujerumani sisi tukiendelea kufa pale Muhimbili. Luther King anaendelea kwenye ukurasa wa 185 anasema kuwa .. “We can never be satisfied as long as the Negro is the victim of the unspeakable horrors of police brutality” hapa anamaanisha kuwa hatuwezi kuridhika iwapo mtu mweusi ndiye mhanga wa ukatili na ubabe usiosemeka wa polisi. Hili ni kauli nyingine ambayo CCM, Kikwete na kina Said Mwema wanapaswa kuifikiria kwa kina kabla hawajavamia maandamano ya amani ya watanzania wanaodai haki zao . Kutokana na matumizi haya ya nguvu dhidi ya raia wake tena wasio na hatia watanzania sasa wamekichoka chama hiki ambacho bila shaka kwa hesabu za harakaharaka ni kuwa hakina dira hata kidogo.


  Nne ambalo ni baya zaidi ni kwa CCM ya Kikwete kukosa umakini au seriousness katika kushughulikia matatizo ya wananchi. Hii ndio CCM ya Jakaya Kikwete ambayo imeshindwa kusimamia hata mawaziri wake , imeshindwa kutenganisha biashara na siasa ikacheza mchezo wa kitoto kwa kudanganya wananchi kwa lundo la ahadi hewa zisizotekelezeka huku ikiwaimbia watanzania nyimbo zilikinaiwa kwenye masikio yao kama sio zilizokwisha futwa kwenye misamiati ya kamusi za vichwa vya watanzania za tumejenga barabara, tumejenga shule na kujenga barabara. Hizi ni ahadi na kauli za kawaida kila baada ya miaka mitano baada ya hapo ni kwenda kusinzia na kulala bungeni kasha kuakolezwa kwa mikataba ya Buzwagi, Richmond na Dowans na safari hiyo kuhitimishwa kwenye Ikulu ya magogoni kwa kauli kama foleni ya Dar es salaam ni ishara kuwa uchumi wetu umekua au kwa orodha kubwa ya takwimu za maendelea za kwenye makaratasi na hotuba zinazochosha za kila mwisho wa mwezi. Nia ajabu sana kuwa mpaka leo kina Yusuf Makamba bao wana jeurai ya kuadhimisha siku ya TANU na pia kumkumbuka baba wa Taifa Mwl Nyerere kuwa na yeye alikuwa mwanachama wa CCM hii ambayo inaongozwa na matajiria huku wafanyakazi na wakulima wakipoozwa kwa fulana na kofia za kijani.


  Hata kwa dawa siwezi kukubaliana na haili hata Nyerere angekuwa hai angewakana watu hawa ambao wametufikisha tulipofika ambapo sasa ufisadi ni staili mpya ya maisha huku rushwa ikisubiri idhini ya Bunge kuitangaza rasmi kama takrima, huku kutumia ubabe kupiga wananchi ni ushujaa na mapenzi ya dhati kwa CCM . Ndipo tulipofika watanzania, si ajabua CCM hii ina ajenda nyingine za siri ambazo tumeanza kuzitilia shaka kama huu ubinafsishaji usiwawezesha wazalendo hata kidogo huku wagei wakineemeka na kutajirika na maliasili zetu na viongozi wachache wakipata gawiwo kwa kusaini mikataba ya kinyonyaji, yaani ni ajabu sana kuwa tangu Mwl Nyerere aondoke madarakani kwa ridhaa yake mwenyewe hakuna chochote cha maana kilichofanyika , tumeshindwa kupiga hata hatua moja mbele tumerudi nyuma tena kwa kasi ya kutisha huku tukiibomoa misingia ya uzalendo na utaifa na kujenga ubinafsi na ufisadi wa kutisha huku CCM wakituzuga kwa kauli tamutamu za kutuka kutushawishi kuwa kuongezeka kwa majengo marefu na magari ya kifahari ni maendeleo kwani nani hajui kuwa magari hayo na nyumba ni zao wenyewe huku sisi masikini tukiendelea kudidimizwa na kunyimwa fursa za kimaendeleo na waroho hao wachache ambao bila shaka wamesahau walipotoka na kjifanya miungu watu…..  Sarakasi zote za CCM sasa zimekwisha, mbwembwe zote za Kikwete zimegonga mwamba, naona mambo yanazidi kuchacha ndani ya CCM , wenye kuhoji tunashangaa hali hii, lakini kama nilivyotangulia kusema hapo awali kuwa hii si bure ni laana ya ufisadi na kuleana ndani ya CCM hii ya Makamba.
  “ CCM sio mama yangu mzazi” haya ni maneno ya hayati baba wa taifa Mwl J.K.Nyerere alisema hivyo kwa kuona anguko la CCM ambalo bila kupindisha wala kumung’unya maneno ndo muda huu CCM inaanguka hata Kikwete analijua hili ndio maana anakitaka chama chake kufanya kile wazungu wanachoita sloughing au kujivua gamba. Kikwete ana taka chama chake kijivue gamba lakini anashindwa kulitaja hiko anachoita gamba , hapa naona ajabu sana kwamba ndio kusema kuwa Kikwete anawaogopa Rostam Aziz , Edward Lowassa, Andrew Chenge na Yusuph Manji? Au ndo tuseme kuwa Kikwete anahofu kumwadabisha mropokaji Yusuph Makamba?
  Naaliona anguko la CCM, maandishi yalishaandikwa ukutani na sasa utimilifu wa nyakati umefika ambapo CCM imewakataawapigania haki Samwel Sitta na Harrison Mwakyembe ikakumbatia ufisadi na wanaonuka ufisadi, kichek esho sana mwanajeshi, mchumi na mwanasiasa nguli wa CCM Jakaya Kikwete amekaa, kafikiria kachanganua , kajumlisha uzoefu wakewa jeshini na usomi wake na udokta wa kupewa kasha akafanya uteuzi katuteulia Steven Wassira kuwa waziri wa mahusiano eti Wassira ni msemaji wa serikali , kweli CCM imefika ukingoni. CHADEMA wanawaelimisha watanzania, mwanaharakati mpambanaji asiyechoka anapambana kwa nguvu ya hoja majukwaani Dr slaa anaililia Tanzania anaibuka mwanasiasa mmoja mchovu ndani ya CCM anatutaka watanzania tumfananishe Dr slaa na Jonas Savimbi kweli CCM imekwisha!


  Maandamano ya CHADEMA yanayojaza watu kibao ni ujumbe tosha kwa Makamba na Kikwete wake kuwa watanzania sasa wamechoshwa na siasa za kihafidhina za CCM, huu ni ushahidi kuwa watanzania wamechoshwa na ukoloni katika nchi yao hawataki tena utawala wanataka viongozi kama alivyowahi kusema Dr slaa na Mbowe Mungu awabariki sana wanaharakati hawa. Kikwete anadai kuwa CHADEMA wanataka kumpindua …..hivi sasa vioja kama sio kuishiwa kisiasa mimi nafikiri kazi ya kuchekesha watanzania kwa kauli za kitoto kama hizi sio za Kikwete bali awaachie kina Masanja Mkandamizaji, Joti na Mpoki.Hivi mtanzania gain mpumbavu ambaye atasikiliza kilio cha kuomba huruma cha Kikwete?


  Labda nitumie fursa hii kumwambia Kikwete na maswahiba wake kuwa juhudi zao ziligonga mwamba na hizi za sasa zitagonga mwamba. Kwani sio makada wa CCM walioibua hoja za kipuuzi kuwa CHADEMA ni chama cha wachagga ila watanzania wakapuuza, wakazidi kutapatapa wakaibua hoja kuwaCHADEMA ni chama cha kidini eti cha wakristo nah ii pia ikashindwa sasa naona wamekuja na haya mawili mapya kwamba moja CHADEMA wanapanga kuiangusha serikali ya Kikwete , pili Dr Slaa ni Savimbi watanzania tusimsikilize. Sasa tukianza na hiyo hoja ya kwanza kwamba CHADEMA wanataka kuangusha nchi ,mi nashindwa kuelewa yeye Kikwete ni juzijuzi tu ametoka kujigamba baada ya uchaguzi kuwa watanzania wanampenda ndio maana wameitosa CHADEMA wakaipa CCM kwa “kishindo” sasa nashindwa kuelewa iweje watanzania hawahawa walioichagua CCM kwa kishindo waigeuke kabla hata mwaka haujaisha tangu wamchague hiyo kwa kishindo? Ama la basi kina Kikwete wanatuibulia hoja fikirishi ya kututaka tuamini yale yaliyotapakaa mtaani kuwa “CCM wamechakachua matokeo”


  Na hii hoja ya pili kuwa watanzania tumwogope Dr Slaa kwa madai kuwa yeye ni kama Savimbi….haya sasa hiki kichekesho kingine yaani kwa mantiki hiyo watanzania tunatakiwa tuwe na hofu na Dr slaa , mi naona kikwete hajui hofu yetu watanzania, ngoja niseme wazi kuwa hofu yetu watanzania ni ufisadi unaoendelea kututafuna, hofu yetu ni jinsi waropokaji kama Steven Wassira wanapopewa jukumu la kuisemea serikali, hofu yetu ni Ikulu yetu ambayo tunaamini kuwa takatifu inaponajisiwa na mwarabu wa Oman Al-Adawy ,hofu yetu ni udini uliopandikizwa miongoni mwetu na wanasiasa wachovu wa CCM , hofu yetu ni kuendelea kuporwa kwa maliasili zetu naam! Kikwete na wenzake wanapaswa kutambua kuwa tunachodai sio utajiri wao bali tunalinda utajiri wetu, hatuhoji juu ya malizao wanazomiliki bali tunalinda maliasili zetu , wala hatuhoji kuhusu mapande yao ya ardhi waliyojimegea bali tunahoji kuhusu uporwaji wa ardhi yetu na wala hatuhoji kuhusu watoto wao wanaposoma ulaya bali tunapigania elimu bora kwa watoto wetu sio shule feki za kata.


  Hayawihayawi sasa yamekuwa , waliodhani kuwa CCM haitaanguka wameanza kuamini sasa kwani wamejionea wenyewe kuwa CCM hii ya sasa sio ndugu wa TANU wala swahiba wa TANU hii ni ya “wenyewe” na sasa anguko la CCM linaonekana , mwisho wa CCM upo dhahiri naona utabiri unatimia NAAM! MAANDISHI YAMESHAANDIKWA UKUTANI HUKUMU INAKUJA 2015 HAKUNA WA KUIPONYA CCM TULIWAPA NAFASI KUTUBU WAKAKUMBATIA DHAMBI NA SASA HASIRA ZETU NI JUU YAO. …..!  Mwandishi wa makala haya ni Ilunga Msekela , aliwahi kusoma chuo kikuu Makerere cha nchini Uganda na ni mwanahabari katika moja ya mshirika ya kimataifa nchini ,anapatikana kwa anwani ya barua pepe; mpambanaji@live.com


   
 2. DSN

  DSN JF-Expert Member

  #2
  Jul 12, 2011
  Joined: Feb 2, 2011
  Messages: 2,745
  Likes Received: 76
  Trophy Points: 145
  Wasiwasi wangu waraka huu,kwa walio wengi,ambao kwao wangepata ujumbe na kujua moja na mbili ya kujifunza na kuona sauti ya mwangi ambayo inasambaa,ikijaribu kusihi na kuonya juu ya anguko hilo ambalo sasa linatishia amani,ni zaili hawatausoma kwa kuwa muda huo wao HAWANA.WAKO BUSSY NA SHUGHURI NA MAJUKUMU YA UJENZI WA TAIFA, HAWANA MUDA.

  Ni kawaida sikio la kufa uwa alisikii dawa,kwa ujumla ni mpaka ya tokee,watakuja kutafuta,waraka kama huu,kuona wakati ule ulisema nini.Wakati huo kichwa cha treni kitakua kimeacha mabehewa.

  TIME WILL TELL!!!!!!!!!!!!!!! JAPO HAWAAMINI.
   
Loading...