BAADA ya wapinzani kushusha tuhuma nzito dhidi ya viongozi kadhaa wa serikali, viongozi wa CCM wamezinduka kama watu waliokuwa katika usingizi wa mangamungamu.
Katika kuzinduka kwao, kila mmoja anasema limtokalo mdomoni mpaka wanafikia mahali wanahitilafiana na kuacha swali, ni nani anayesema kweli?
Nionavyo, tatizo la CCM ni kutokubali kukosolewa, yaani kukubaliana na hali halisi ya nchi ilivyo hivi sasa.
Linapokuja suala la kuwa na katiba mpya, CCM huwa kama mtu aliyetoneshwa kidonda kisichopona (donda ndugu). Badala ya kujibu hoja, wao hujibu mashambulizi katika kile kionekanacho kama jino kwa jino.
Madai ya wapinzani kuhusu ufisadi wa baadhi ya viongozi wa serikali, CCM inataka ushahidi upelekwe mahakamani.
Wapinzani walitaka kuutoa bungeni wakafanyiwa mizengwe. Wanapokuja kwa wananchi kueleza yaliyojiri ndani ya jumba lile la kutunga sheria, CCM inasema eti walishindwa kutoa ushahidi, mara walishindwa kwenye uchaguzi na sasa wanawalaghai wananchi.
Nani anayelaghai kati ya mwenye kutaka kutoa ushahidi na yule anayekataa kuusikiliza ushahidi huo?
Kama kumbukumbu zangu ziko sahihi, Rais Jakaya Kikwete aliwahi kusema kuwa inashangaza kusikia suala linaloihusu polisi moja kwa moja watu kutaka iundwe tume ya uchunguzi.
Kama Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali amegundua upotevu/ubadhirifu wa fedha kwa kununua vitu visivyoonekana au kutorejesha fedha za masurufu bila maelezo, kwa nini polisi hawaitwi ili watimize wajibu wao?
Kila mwaka, ripoti ya Mkaguzi Mkuu huonyesha mamilioni ya fedha yaliyopotea, ama kwa uzembe, ubadhirifu au wizi wa kutumia kalamu.
Mpaka sasa si mamilioni tena, bali mabilioni kadhaa ambayo yangeweza kutumika kwa maendeleo ya nchi. Hakuna yeyote aliyefikishwa mahakamani kwa kosa la ufisadi wa fedha za umma.
Hali hiyo inawafanya wajanja wachache waendelee kujichotea fedha kila mwaka na itaendelea hivyo mpaka itakapokuja serikali yenye watendaji makini wasio wa ponda mali kufa kwaja kwa maana ya chukua chako mapema.
Kwa woga walio nao CCM ndiyo maana hata majimbo ya uchaguzi wameyataifisha kwa kuyaita yao kana kwamba wapinzani si raia wa nchi hii, na kwa hiyo hawastahili kugombea wala kuchaguliwa! Kauli za lazima tukomboe majimbo yetu ni ushahidi kuwa CCM inataka kutawala milele.
Kwa nini? Kwa sababu inaogopa kama itashindwa na wapinzani kushika madaraka, wakubwa wataulizwa juu ya mali walizojilimbikizia na ubadhirifu mwingi waliofanya wakati wa utawala wao.
Labda niwakumbushe wana CCM jambo moja muhimu. Kule Taiwan, kuna chama kiitwacho Kuomintang (KMT), yaani chama cha umma kilichotawala kwa miaka 50 mfululizo - 1950 - 2000.
Chama hicho kilitwaa madaraka kwa katiba iliyoundwa mwaka 1947 na kufanyiwa marekebisho mara nne 1992, 1994, 1997 na 1999. KTM ilianzishwa na Dk. Sun Yatsen mwaka 1894 na iliadhimisha karne moja (miaka 100) Novemba 24, 1994.
Lakini pamoja na uzoefu wa miaka yote hiyo katika siasa na kuwa madarakani kwa miaka 50 mfululizo, ilifikia mwisho wake mwaka 2000 kwa kushindwa na Chama cha DPP (Democratic Progressive Party) kilichokuwa na umri wa miaka 14 tu tangu kilipoundwa.
Nataka kuwaambia CCM kuwa kila chenye mwanzo hakikosi kuwa na mwisho na ngoma ivumayo sana haikeshi.
Kama chama kilichoundwa miaka 100 iliyopita na kuwa na uzoefu wa utawala kwa miaka 50 kimeangushwa na chama kichanga, basi siku za CCM kuangushwa kwa kura, tena za kishindo, ziko kwenye kizingiti cha mlango.
Hata kwa mtu aliyekimbia umande, yaani ambaye hakuuona mlango wa darasa, hawezi kudanganywa katika kuhesabu fedha zake. Anaijua fedha kuanzia senti moja mpaka noti ya shilingi elfu kumi.
Vivyo hivyo, ingawa si Watanzania wote, ni wachumi, lakini wanajua uchumi wa nchi umeporomoka na unaendelea kuporomoka, tena kwa kasi.
Kama uuzaji wa bidhaa na mazao mbalimbali nje ya nchi umeshuka kwa asilimia 39.8 hadi kufikia dola milioni 5.7 za Marekani katika kipindi cha mwezi Julai mwaka huu, ni vipi serikali inajigamba kuwa uchumi unapaa?
Aidha, iwapo uuzaji wa pamba katika kipindi hicho ulipungua kutoka tani 115,952 hadi tani 26,443 (tofauti ya tani 89,509) na korosho kupungua kutoka tani 84,200 mpaka tani 57,400 (tofauti ya tani 26,800) ni vigumu kuamini kuwa uchumi wetu unakua.
Maana uchumi waweza kukua iwapo tunauza mazao na bidhaa nyingi nje na tunanunua bidhaa chache kutoka huko. Hata taarifa ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inathibitisha kupanda kwa mfumuko wa bei kutoka asilimia 5.9 mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu na kufikia asilimia 9.0 mwisho wa mwezi Julai.
Sasa uchumi huo unakua kinyumenyume au kwa miujiza ya Mungu?
Turejee kwenye mada ya wapinzani dhidi ya ubadhirifu wa mali ya umma kwa upande mmoja na CCM dhidi ya wapinzani kwa upande wa pili.
CCM inataka wapinzani wapeleke ushahidi polisi. Ule uliotolewa hadharani kwa wananchi au wa ziada? Kama ni wa ziada mbona ndiyo itaumbuka zaidi?
Tukubaliane na CCM kuwa wapinzani wapeleke ushahidi polisi. Kama mkuu wa wilaya anaweza kuamuru mtu kuwekwa ndani na polisi ikatii bila kutafuta uhalali wa kukamatwa na kutiwa ndani, itakuwaje kwa wapinzani wanaoonekana mbele ya macho ya CCM kuwa mahasimu wao? Watatendewa haki?
Majaji, mkuu wa Takukuru, Mkuu wa Jeshi la Polisi, Mkuu wa Upelelezi nchini, Msajili wa vyama vya siasa na Mkuu wa Usalama wa Taifa wote wameteuliwa na Rais.
Bunge limetawaliwa na CCM na hoja yoyote ya wapinzani hushindwa kutokana na uchache wao, kwani wenzao hukutana kama kamati ya chama na kupanga jinsi ya kuwavunja nguvu.
Kinachotetewa ni masilahi ya chama na si ya wananchi. Kwa hali hii ni nani wa kumfunga paka kengele mkiani?
Idi Amin Dada (Mungu amrehemu) alipotoa vitisho na hata kuivamia Tanzania kule Kagera katika kile kilichokuja kujulikana kama Vita ya Kagera, aliwauliza askari wake kuwa ndege ya kivita ingechukua dakika ngapi kutoka Entebbe mpaka Dar es Salaam na kurudi baada ya kuangusha mabomu.
Vitisho vyake vilitupa muda wa kujiandaa kwa vita na tulipokuwa tayari, tulitangaza nia ya kupigana naye, sababu na uwezo na ndivyo ilivyokuwa. Aliikimbia nchi yake akisahau kofia na bastola yake chumbani!
Waziri mmoja wa serikali ya awamu ya pili, alitangaza kuwa siku inayofuata atakwenda kukagua ghala moja la chakula la kampuni maarufu nchini, baada ya kuambiwa kuwa kampuni hiyo inauza vyakula vilivyopitwa na wakati.
Kilichofanyika ni tajiri wa kampuni ile kukodi vibarua waliofanya kazi usiku kucha kuhamisha vyakula vibovu na kuvipeleka walikojua. Waziri alipokwenda kesho yake, akakuta ghala jeupe.
Hii ina maana gani? Ni kama kumwambia mwenye ghala: Wewe, ficha vyakula vyako vibovu ili nikija kesho na waandishi wa magazeti tusikute kitu. Na kwa Idi Amin vilevile ni kama alituasa tujiandae kwa vita.
Tahadhari hizi hazina tofauti na TAKUKURU inapowatahadharisha viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) na viongozi wenye majumba makubwa ya thamani ya kuogofya kuwa, itawafuata baada ya kazi waliyo nayo kukamilika.
Kwa hiyo, inawapa nafasi wanaotuhumiwa na kushukiwa wajiandae au kuchukua hadhari kabla ya hatari. Atakamatwa nani kwa mpango huo?
Hebu fikiri mtuhumiwa wa ubadhirifu wa fedha za umma, anatetewa kwa nguvu zote na serikali akiachwa aendelee na shughuli zake za kiofisi akiwa na uwezo wa kuharibu ushahidi wote unaohusu tuhuma dhidi yake.
Kwa nchi zinazojua maana ya demokrasia, watu kama hao hujiuzulu au hulazimishwa kujiuzulu ili uchunguzi ufanyike vizuri. Si hivyo kwa Tanzania yetu!
Kama kweli CCM inataka kujikosha, ikubali madai ya wapinzani yachunguzwe na tume huru ili ukweli uwekwe hadharani na sheria ifuate mkondo wake.
Tofauti na hili, itakuwa porojo zisizokuwa na maana zaidi ya kuwasononesha wananchi walio wengi.
marobarnabas@yahoo.com
0756 855 314
0784 334 096