Khalidoun
JF-Expert Member
- Feb 12, 2013
- 2,842
- 4,474
Makala murua yenye uchunguzi yakinifu usiomili upande wowote
NA LUQMAN MALOTO
JICHO zembe linatoa pongezi kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeshinda Uchaguzi Mkuu 2015 kwa kishindo. Jicho mfu linasifu upinzani kwa kuonesha msuli imara kiasi cha kuelekea kutwaa mamlaka ya jiji kubwa la Dar es Salaam.
Jicho chongo linakipa heko ACT-Wazalendo, kwamba pamoja na upya wake kimeweza kushinda jimbo na kuchukua mamlaka ya Halmashauri ya Mji wa Kigoma Ujiji. Jicho pofu linaponda kuwa wapinzani wameibiwa kura.
Jicho pevu linaona kufeli kwa vyama vyote. Linatambua tu kuwa kipo chama kilichofanikiwa kushika dola na vingine vimekosa. Hesabu ya juu inaonesha dhahiri kuwa kila chama kinajifariji tu!
CCM kilitambia mgombea urais asiye na makando-kando mengi ya ovyo. Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) pamoja na vyama vya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), walijidaia mgombea turufu kutokana na umaarufu wake.
Mgombea wa CCM ambaye ndiye Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa sasa, Dk John Pombe Magufuli, ushindi wake umebebwa na chama zaidi (Popularity of the party). Mgombea wa Chadema na Ukawa, Edward Ngoyai Lowassa alikuwa na mbeleko ya ukubwa wa jina.
Kwa kutazama wagombea hao, aliyekuwa na tiketi ya mtaji mkubwa wa umaarufu (Kangaroo Ticket) ni Lowassa. Magufuli asingeiona Ikulu bila nguvu kubwa ya chama chake (Political party muscularity).
CCM KIMEANGUKA
Huwezi kuisifu CCM kwa ushindi wa kishindo wakati kina majeraha makubwa. Zaidi kimepata ushindi mwembamba kuwahi kutokea katika miaka 20 ya kufanyika kwa Uchaguzi Mkuu chini ya mfumo wa vyama vingi vya siasa.
CCM kimepoteza majimbo mengi, zaidi kimebaki mufilisi kwenye Jiji la Dar es Salaam. Ni uhakika kuwa kwa idadi ya wabunge na wingi wa madiwani ambao Chadema na Cuf wamepata, ndiyo watakaounda mamlaka katika Halmashauri ya Jiji.
Kwa mara ya kwanza katika historia, CCM kinageuka mpangaji ndani ya jiji muhimu kabisa katika nchi. Kinabaki kuongoza serikali kuu lakini halmashauri imechukuliwa na upinzani. Je, unaweza kuita ushindi kwa CCM?
Tangu mwaka 2010, dalili zilishaonesha wazi Chadema ndiyo wenyeji Jiji la Arusha, na 2015 ndiyo wameifuta kabisa CCM. Ongezea Kilimanjaro kisha Manyara, hakika huwezi kusifu CCM kuwa imefanya vizuri wakati imeshindwa kuzirejesha ngome (strongholds) za wapinzani.
Mpaka Bunge la 10 lilipokuwa linakamilika, idadi ya wabunge wa upinzani ilikuwa 91, Chadema wakiwa na 49, Cuf 35, NCCR-Mageuzi 5, TLP na UDP kila kimoja kikiwa na kiti kimoja, jumla hiyo ikiwa ni pamoja na viti maalum.
Jumla hiyo ilikuwa sawa na asilimia 25 ya bunge zima. Kwa mantiki hiyo CCM ilimiliki asilimia 75.
Kwa upande wa matokeo ya sasa, inaonesha kuwa Cuf ina wabunge 49, Chadema 71, NCCR-Mageuzi na ACT-Wazalendo kila kimoja kina kiti kimoja. Jumla ni 122 ambayo ni sawa na asilimia 32.
Hesabu hiyo ni nje ya majimbo nane ambayo uchaguzi wake utarudiwa kutokana na sababu mbalimbali. Kuna ambayo kulitokea hitilafu za uchaguzi, mengine wagombea walifikwa na mauti kabla ya uchaguzi.
Hii ni kuonesha kuwa uchaguzi wa mwaka huu una matokeo ya kuimarika zaidi kwa upinzani ndani ya bunge. Hivi sasa, idadi ya wapinzani bungeni ni takriban theluthi moja.
Idadi hiyo inatosha kabisa kuyumbisha baadhi ya mijadala na miswada ya serikali kama wapinzani watasimama kama kitu kimoja, huku wakiongeza na wale wana CCM watukutu, wafia nchi kuliko chama.
Uimara huo wa upinzani ndani ya bunge linalokuja, unatosha kuonesha kwamba CCM imefanikiwa kushinda dola lakini meno yake yamepungua. Kimefeli kulinda ubabe wake ndani ya bunge. Kinavutwa sharubu.
Kwa asilimia 32 ambayo wapinzani wamepata, maana yake wamebakiza 18 tu kuweza kwenda sawa na CCM. Hii inatoa taswira kuwa Chama Cha Mapinduzi kina kazi kubwa ya kufanya kuelekea 2020, vinginevyo kinaweza kupoteza nguvu na mamlaka yake.
CCM kilikuwa na makusudi makubwa ya kurejesha majimbo yaliyokuwa chini ya wapinzani, hususan Chadema, zaidi yale ya mijini. Mafanikio yao yamekuwa kidogo mno kuliko kushindwa. Labda kijipange tena!
Pamoja na idadi ya wapiga kura kuwa kubwa mwaka 2015, lakini uwiano wa asilimia ambao CCM wamepata, umepungua tofauti na ilivyokuwa mwaka 2010. Hiyo imesababisha hata idadi yake ya viti maalum kushuka.
Mwaka 2010, CCM kilipata viti maalum 67 kati ya 102, sawa na asilimia 66, mwaka huu CCM kimepata viti 63 kati ya 113, sawa na asilimia 56. Kimeshuka kwa asilimia 10 nzima.
Juu ya yote hayo, linafuata anguko la CCM kwenye ruzuku kutoka serikalini. Maana kadiri kura zinavyoshuka ndivyo na kiwango cha ruzuku kinavyopungua. Mwaka 2010-2015, CCM kilikuwa kinalipwa zaidi ya shilingi milioni 800 kwa mwezi. Msajili wa Vyma vya Siasa, Jaji Francis Mutungi anakamilisha hesabu zake.
UKAWA WAMEFELI
Upande wa pili Ukawa wamefeli. Pamoja na kuongeza idadi ya wabunge lakini kiwango walichopata hakioneshi matokeo ya umoja wa vyama vikubwa vya upinzani vilivyofanya kazi kwa miaka mitano.
Wameshindwa kutumia nguvu ya mgombea karata dume (Kangaroo Ticket) waliyekuwa naye. Kushindwa kwao na CCM ni matokeo ya kuwa waliingia kwenye uchaguzi kwa majaribio. Hawakuwa wamejiandaa!
Lowassa alipojiunga na Ukawa, taswira iliyoonekana kwenye siasa za nchi ni kuwa Lowassa aliwabeba Ukawa kuingia kwenye uchaguzi, hili ni kosa kubwa la kiufundi.
Picha ilikuwa kwamba Ukawa walimuona Lowassa mbeleko ya kutimiza malengo yao ya kuchukua dola. Lowassa kwa Ukawa ilikuwa tiketi tu, hata uhusika wake ulijionesha kuwa ni jeshi kamili, lililoamua kutumia uwanja wa Ukawa kuikabili CCM.
Baada ya Lowassa kutua Ukawa, ndipo ilipobainika kuwa kumbe nguvu ya upinzani ni ndogo kuliko kelele zilivyokuwa. Hawakuwa hata na wanachama au mashabiki vindakindaki (Ukawa-mania). Upinzani ukapambwa na watu wa Lowassa (Lowassa-mania).
Mgawanyo wa kura ambazo Ukawa wamepata, hususan Tanzania Bara, zinaonesha kuwa vyama vinavyounda umoja huo bado dhaifu mno. Hata wabunge ambao wamepata kwa kuangalia maeneo, ni matokeo ya wimbi la Lowassa (Lowassa coattail effect).
Coattail effect ni msamiati wa kisiasa wenye maana ya mgombea mkubwa au kiongozi wa chama kusaidia wagombea wa nafasi za chini kushinda viti. Mfano mgombea urais anapowabeba wabunge, au mgombea ubunge anapowanyanyua madiwani kushinda.
Matokeo ya Uchaguzi Mkuu 2015, yanatoa picha kuwa nguvu ya Lowassa ilikuwa chanya na iliwabeba mno Ukawa. Ngome za Lowassa, hususan yale maeneo ambayo alifanya kampeni kubwa ndipo alipata kura nyingi na Ukawa kushinda viti vingi vya ubunge na madiwani.
Lowassa alifanya kampeni kubwa ndani ya Jiji la Dar es Salaam na matokeo yamewabeba mno Ukawa. Mafuriko ya Kaskazini yamedhihirisha kwamba Lowassa ndiye baba mwenye nyumba wa kanda hiyo.
Udhaifu wa Ukawa ulijidhihirisha mno kipindi cha kampeni. Timu yote ilimzunguka Lowassa katika ziara zake, hawakujigawa kimakundi. Ndiyo kusema wenyeviti wa Ukawa, Freman Mbowe (Chadema) na James Mbatia (NCCR-Mageuzi), hawakuwa na ubavu wa kufanya mikutano yao wenyewe kumnadi na kumtetea Lowassa.
Kingine ambacho kilionesha udhaifu wa Ukawa ni jinsi ambavyo kiliwapokea Waziri Mkuu Mstaafu, Fredrick Tluway Sumaye na mmoja wa waasisi wa CCM, Kingunge Ngombale Mwiru. Sumaye na Kingunge wakawa wazungumzaji wakuu wa upinzani. Wakati kwa akili ya kawaida, ilifaa tu watu hao kutumiwa kama maonesho.
Wageni kubeba ajenda ya upinzani wakati wenye upinzani wao wapo ni udhaifu ambao Ukawa waliuonesha. Na ndiyo maana matokeo ya Uchaguzi Mkuu 2015, yameakisi nguvu ya Lowassa katika ngome zake na yamedhihirisha msuli mdogo wa Ukawa.
Kama Ukawa wangekuwa wamejitengeneza vizuri kimtandao, ingekuwa rahisi mno kwao kuishinda CCM mwaka huu. Asilimia 40 ya matokeo ya mgombea urais, kama yangechagizwa na nguvu ya vyama vya Ukawa, huu ni mwaka ambao CCM wangegeuka kuwa wapinzani.
Ni ukweli kuwa Ukawa wamepata jumla ya wabunge 121 lakini nyongeza hiyo haishabihiani na mtaji waliokuwa nao wa kuunganisha vyama vikubwa vitatu, yaani Chadema, Cuf na NCCR-Mageuzi ambavyo kila kimoja kimepata kuwa taa ya upinzani nchini.
Hapo sijakizungumzia NLD cha marehemu Dk Emmanuel Makaidi kwa sababu hakijapata kuwa lolote wala chochote katika siasa za nchi.
Lowassa alipokatwa tu jina lake kuelekea kupata Mgombea Urais wa CCM, chama hicho kilipungua nguvu. Alipohamia Ukawa, ghafla yakaja matokeo ya wapinzani kutamba kuliko CCM.
Mwenyekiti wa CCM, Dk Jakaya Kikwete alikejeli nguvu hiyo ya Lowassa na Ukawa kwa kuiita ni moto wa mabua. Na bila kutarajia, Lowassa alianza kupoteza kasi yake. CCM ikarejea kwenye kilele chake cha kufanya kampeni zenye nguvu kisha kutamba katika vyombo vya habari.
Kwa mtu aliyefuatilia mchakato wote wa Uchaguzi Mkuu 2015 katika jicho la tathmini, atakubaliana na mimi kuwa Lowassa alitamba sana mwanzoni, alipotea katikakati kisha akaibuka mwishoni.
Tathmini hiyo inakuja na majibu kuwa Ukawa haijavibeba vyama vyote vya upinzani vilivyomo kwenye umoja huo. Kilichonufaika ni Chadema ambacho kimeongeza idadi ya wabunge. Cuf kimepata afadhali, maana kimeongeza wabunge hadi kufikia 49, wakati kipindi cha mwaka 2010 mpaka 2015, kilikuwa na wabunge 35.
NCCR-Mageuzi kimefilisika, kutoka wabunge watano 2010-2015, sasa kimebaki na mbunge mmoja tu. Huku pia ni kufeli kama taasisi yenye malengo ya kukua kwa pamoja.
ACT-WAZALENDO HAKIJAFURUKUTA
Yapo maneno ya kujifariji kuwa ACT-Wazalendo, angalau kimepata mbunge mmoja, kimeshinda madiwani zaidi ya 50, vilevile kimejinyakulia mamlaka ya Halmashauri ya Kigoma Ujiji.
Kwanza, huwezi kujivunia kushinda ubunge jimbo moja wakati mshindi mwenyewe ni Zitto Kabwe ambaye ni kiongozi wa chama hicho. Huu siyo ushindi, ni utetezi wa mtaji wake.
ACT-Wazalendo waliingia kwenye uchaguzi wakiwa na mtaji wa ubunge wa Zitto, na kama angeshindwa basi matokeo tungesema mtaji umeliwa. Ila kwa Zitto kushinda, maana yake chama kimeunusuru mtaji wake.
Chama hicho kilisimamisha watu ambao walikuwa wabunge katika mihula iliyopita. Moses Machali alikuwa mbunge wa Kasulu Mjini (NCCR-Mageuzi) lakini ameshindwa. Huu pia ulikuwa mtaji wa ACT-Wazalendo lakini umeliwa.
ACT-Wazalendo kiliwasimamisha Modestus Kilufi, aliyekuwa mbunge Jimbo la Mbarali (CCM), Salvatory Machemli (Chadema) Ukerewe, Mustafa Akonay (Chadema) Mbulu, Charles Mwera (Chadema) Tarime, wote hao walikuwa wabunge nyakati zilizopita, na wameshindwa. Hapa mtaji wa ACT-Wazalendo umekata!
ACT-Wazalendo pia kilisimamisha wagombea ubunge waliopata kuwa wabunge wa viti maalum nyakati zilizopita, Chiku Abwao (Iringa Mjini), AnnaMaryStella Mallac (Mpanda Vijijini) na Mkiwa Kimwanga (Ilemela) ambao wote wameshindwa. Hapa pia mtaji umeliwa!
Chama hicho kina wasomi na watu wakubwa, kiongozi wake Zitto, mshauri Profesa Kitila Mkumbo na wengineo, wamewezaje kushindwa kuwa na mikakati ya kushinda majimbo japo machache na kubaki na moja tu?
Kitila na Zitto ni vichwa vilivyochagiza mafanikio ya Chadema kugeuka kuwa chama kikuu cha upinzani mwaka 2010.
ACT-Wazalendo kilisimamisha wagombea 202 nchi nzima, kitendo cha kuambulia jimbo moja, maana yake kimefanywa vibaya kwenye majimbo 201. Kwa hili, chama hicho inabidi kijipange na kubadili mfumo wa kampeni zake kuelekea Uchaguzi Mkuu 2020.
Kwa hakika, huwezi kusimama na kutamba eti ACT-Wazalendo hawakuwa na mbunge hata mmoja, sasa wanaye. Lazima kutazama uwekezaji na matokeo.
Kama wangekuwa wamesimamisha wagombea 10 nchi nzima na kushinda jimbo moja isingekuwa tatizo, lakini majimbo 202 ni uwekezaji mkubwa mno, kuambulia kiti kimoja ni kushindwa kwa kiwango cha juu.
Chama hicho kilisimamisha mgombea urais, Anna Mghwira. Kwa umaarufu wa Zitto na maarifa ya Profesa Kitila katika uchaguzi, ilidhaniwa kuwa ACT-Wazalendo chenyewe ndicho kingeweza kuamua mshindi kupitia dhana ya kingmaker scenario, kutokana na mvutano mkubwa uliokuwepo kati ya Magufuli (CCM) na Lowassa (Ukawa).
Matokeo aliyopata Mghwira yanaonesha kuwa ACT-Wazalendo kilipata faida pekee ya kusimamisha mgombea urais, kionekane kipo na kupata promosheni ya vyombo vya habari.
Mghwira na wagombea wengine wote wa vyama vidogo, wameachwa kwa nafasi kubwa kiasi kwamba kati ya Magufuli na Lowassa hakuna mwenye kuhisi maumivu au kutamani kura zao.
Mghwira angetengeneza mantiki kama angekuwa athari ya kura za ushindi (spoiler effect), kwamba kati ya Magufuli au Lowassa, mmoja angezifikiria kura za ACT-Wazalendo, kuwa angezipata angeweza kushinda.
Juu kabisa ni kuwa ACT-Wazalendo kimeshindwa kutengeneza matokeo ya kuwa chama cha tatu chenye nguvu. Kinatakiwa kujipanga upya.
MSISITIZO WANGU
Kila upande umebaki na maumivu, sioni mwenye kujisifu kwa ushindi. Tuachane na hoja dhaifu za wizi wa kura na kuibuliwa kwa hoja ya mazowea ya Rais wa Mioyo ya Watanzania.
Jumla ya Ukawa bungeni ni asilimia 32 tu, matokeo hayo bado hayaakisi viashiria vya ushindi kwa Lowassa. Angalau angepata wabunge kati ya asilimia 45mpaka 50, tungeweza kuona hoja hapo.
Mwaka 2010, Chadema walisema aliyekuwa Mgombea Urais wao, Dk Willibroad Slaa alishinda. Kisha wakamtangaza kuwa Rais wa Mioyo ya Watanzania kwa miaka mitano.
Slaa ambaye alipata wabunge asilimia 15, hakuweza kukamata mamlaka za miji (halmashauri) japo kwa asilimia hata tano lakini Watanzania wakaambiwa ndiye aliyeshinda na kwamba aliibiwa kura.
Tuache siasa utoto, ukishindwa na kukubali, unamtengenezea mazingira mpigakura wako kutambua umuhimu wa kuchagua siku nyingine, ukimwambia kura yake iliibiwa, unampa hasira na kutotamani kupiga kura tena. Ndiyo sababu wangine wanaharibu kadi zao za kupigia kura.
Naona upinzani unaimarika lakini matokeo yao yanaonesha wanaendekeza siasa urembo (cosmetic politics), ambazo hazizami zaidi kwa wapigakura, wanaishia tu kutamba mijini na katika mitandao ya kijamii.
Ushindi wa kisiasa ni watu, lazima kuwekeza. Ruzuku za vyama zifanye kazi kukuza mitandao ya vyama. Uzembe na ubinafsi utasababisha kila mwaka wa uchaguzi CCM kinavuna vijijini kisha wanaimba ?CCM mbele kwa mbele?, wapinzani mnalalamika kuibiwa kura.
By Luqman Maloto
MAANDISHI GENIUS