Ccm, tanzania na changamoto za uchaguzi 2010 | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Ccm, tanzania na changamoto za uchaguzi 2010

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by Sengwira, Oct 7, 2009.

 1. S

  Sengwira Member

  #1
  Oct 7, 2009
  Joined: Nov 27, 2007
  Messages: 19
  Likes Received: 2
  Trophy Points: 5
  CCM, TANZANIA NA CHANGAMOTO ZA UCHAGUZI MKUU 2010

  Chama cha Mapinduzi hivi karibuni kimeunda kamati inayoongozwa na rais Mstaafu alhaji Mwinyi ili kuchuguza chanzo na baadaye kupendekeza njia sahihi ya kuondoa tofauti zilizozuka kati ya wabunge/wawakilishi na serikali ya chama hicho.
  Haja ya kufanya utafiti huo inakuja baada ya kuona dalili ya kuwa tofauti hizo zinaifitinisha CCM na wananchi.

  Ni juhudi muhimu kwa kila chama makini na kipevu kama CCM kutambua changamoto muhimu kabla ya kuelekea kipindi muhimu cha kisiasa kama cha uchaguzi mkuu wa mwakani. Lakini swali la msingi la kujiuliza ni kama kweli wanatumia njia na watu sahihi kutambua na kutatua changamoto halisi zinazoikabili.

  Tunasema hivyo kwa kuwa vitendo na tabia ya CCM ya takribani miaka minne ya uongozi wa awamu ya nne vinaonekana kukidhi utabiri wa aliyekuwa katibu wake mkuu hayati komredi Horace Kolimba.

  Kabla ya kifo chake ndugu Kolimba alisema kuwa CCM imekosa dira na muelekeo. Sidhani kama chama kiliijadili kwa kina kauli hii zaidi ya kumjadili Kolimba na kwa hakika ndio ukweli ambao ulimgharimu Kolimba na pengine unakigharimu chama sasa na kwa siasa za baadae za nchi yetu.

  Yaliyomgharimu Kolimba kipindi kile ni pamoja na lawama na kutengwa na mfumo wa imani wa chama chake kwake. Kimsingi alionekana msaliti na aliyefanya kosa kubwa kama la uhaini katika sheria za nje ya chama, sheria za nchi. Bahati mbaya Mungu alimpumzisha ndugu Kolimba kabla hajaifafanulia CCM na taifa alichokuwa nacho moyoni.

  Pengine CCM ilikuwa na mawazo kuwa jambo hilo haliwezi kurudiwa na mwanachama wake yeyote mwenye akili (timamu?) na mwaminifu wa kweli. Hatusemi kuwa hayajapata kutokea lakini tunashangazwa na upofu wa CCM kuwa kutokubali kukosolewa na kushindwa kujikosoa ndio unazalisha kina Kolimba na kukifitinisha na wananchi.

  Yaliyotokea na yanayofanywa na baadhi ya wabunge wa CCM bungeni akiwemo spika Sitta hayana tofauti na ujasiri wa hayati Kolimba. Na wasema kweli wan chi yetu watakubaliana nami kuwa chama kimerudia historia ya kuwaweka kitimoto kina Sitta na wenzake ingawa kwa tahadhari kubwa baadhi ya viongozi wamechukua hatua madhubuti za kuonesha kuwa hakuna aliyewekwa kitimoto.

  Kwa mantiki hii utagundua kuwa CCM bado ipo katika giza la miaka ya nyuma ya sitini na sabini ya siasa ya chama kushika hatamu. Katika mfumo huo wa chama kushika hatamu ni kuwa serikali na mihimili yake itapokea na kutekeleza yote yatokayo katika cham. Hapa si bunge wala raia wa kawaida anayeeleweka akiamua kuhoji usahihi wa maamuzi na tabia za kisiasa za taifa nje ya mfumo wa chama.

  Pengine utaratibu huu haukuwa na athari kipindi hiko lakini inashangaza kuwa CCM pamoja na kuwa na rasilimali watu wenye elimu na uelewa wa siasa na demokrasia wameshindwa kujua kuwa zama hizi ni mpya, zama za demokrasia ya kweli. Wamesahau kuwa Tanzania imeshajiondoa katika mfumo wa serikali ya chama na kuwa na mfumo ambao chama huweza kuongoza serikali tu na si vinginevyo.

  Pengine CCM bado wana mawazo kuwa kila mtanzania ni m-CCM na kuwa kila mwanachama wake ni mbumbumbu. Na kusema kweli hili ndio kosa kubwa linalofanywa na CCM ambalo linaifitinisha na wananchi kuliko ukosoaji wa wabunge wake kwa serikali ya chama chao, na kwa msingi huu kamati ya Mwinyi inaonekana kuwa ni kushindwa kwa CCM kujua nini hasa changamoto zinazoikabili na utatuzi sahihi kuelekea uchaguzi mkuu.

  Kwa msingi huo adui mkubwa wa CCM katika uchaguzi mkuu ujao ni CCM yenyewe na si wana-CCM au wachawi kitoka nje ya CCM. Na kwa kutumia alichokisema Kolimba, badala ya kujadili wabunge na wawakilishi CCM ilitakiwa kutafuta kwanza dira na muelekeo. Zipo njia nyingi lakini baadhi ni akama zifuatavyo;

  CCM lazima ikubali kujifunza kutoka katika historia na kusoma ishara za nyakati. Chaguzi za 2010 na kuendelea hazitafanana kwa kiwango kikubwa na chaguzi za kuanzia 1990 hadi 2005. kitendo cha kuendelea kuendesha siasa kwa uzoefu na upofu wa kuwa hakuna mbadala wa CCM unazidisha hatari ya kuanguka kwake.

  Profesa Shivji katika makala yake ya “Electoral Politics, Liberalization and Democracy” katika hariri ya Mukandala na Othman ya Liberalization and Politics: The 1190 Election in Tanzania anaeleza namna uchaguzi wa 1990 ulivyokuwa unakiuka demokrasia ya kweli kwa uchama kuwa mbele zaidi ya sifa za kugombea.

  Wagombea wa kipindi hiko walikuwa hawapimwi kwa uwezo wao binafsi katika kuongoza isipokuwa kilichokuwa kinapimwa na uanachama wao na ukaribu walionao kwa uongozi wa taifa na itikadi ya chama.

  Sisemi kwamba hili ndivyo lilivyo sasa lakini CCM inapaswa kujiuliza kuwa ni kwa kiasi gani imekuwa ikijizatiti kutengeneza wanachama, wagombea na viongozi ambao wananchi watawapima kwa uwezo wao binafsi na kuwakubali kuwa hawa ni wenzetu hasa? Ifanye hesabu ya wabunge wake ambao hawafanani kabisa na wananchi wa majimbo wanayowawakilisha bungeni inahatarishaje mpasuko wa CCM na wananchi wa kawaida.

  Hivi karibuni waziri mkuu Pinda aliwaasa wananchi wa Mpanda kuwa wawe makini na wagombea wanaodai kuwa wametumwa nae kwenda kugombea katika uchaguzi wa serikali za mitaa. Hii ni dalili kuwa viongozi wengi wa CCM na wabunge wanataraji au wamengia katika uongozi kwa majina ya wakubwa kitu ambacho ni sawa na kusema ukabila.

  Je ni kwa kiasi gani CCM inafahamu na kushughulikia ukabila huu? Au inasahau kuwa katika siku za sasa wapiga kura wanajiuliza kuhusu uwezo wa mtu badala ya uhusiano wake na viongozi wa kitaifa? Kwa upofu huu, wananchi wanawachukulia wabunge kuwa si miongoni mwao na kuamini kuwa chama ni cha wenyewe. Kamati ya Mwinyi imekusudia nini, kuwasogeza wananchi kwa chama chao, wabunge kwa chama chao au kukisogeza chama kwa wenye chama chao?

  Maswali haya ndio yanajenga hoja kuwa suala si wabunge kukitetea chama chao ila chama kurudi kwa wenye chama chao ambao ndio nguzo na dira. Kwa kutumia maneno ya mwalimu Nyerere kuwa “katika mfumo wa sasa Rais anaweza kutoka nje ya CCM lakini Rais bora ni lazima atoke ndani ya CCM ambayo ni ya wakulima na wafanyakazi wa hali ya chini” je, kamati ya Mwinyi imeelekezwa kuchambua changamoto hii?

  Kuelekea uchaguzi mkuu CCM lazima ijiulize kuwa ni kwa kiwango gani inajizatiti kuhakikisha kuwa inasimamisha wagombea ambao ni wakulima na wafanyakazi wa hali ya chini? Jambo hili lisingelazimisha uundwaji wa kamazi ya Mwinyi kutafuta namna bora ya kupata imani na ukaribu wa chama kwa wananchi ambao watakuwa ndio chama chenyewe.

  Nani asiyefahamu kuwa inaposemwa “CCM ina wenyewe” kwa tafsiri ya sasa haina maana ya “wakulima na wafanyakazi wa hali ya chini” ila wafanyabiashara, matajiri na wenye kuroga? Na hii ndio maana ikitokea wa hali ya chini yupo ndani ya mkondo wa uongozi ataulizwa je nawe ni wa mtandao upi?

  Wananchi wanajiuliza leo kuwa nini sifa ya uanachama wa mitandao hii kama si wizi, kujuana na ulozi? Wananchi wako tayari kuitetea na kuipenda CCM itakayokuwa na viongozi wanaotajwa na katiba ya CCM ibara ya 17 kuwa “wawe waliotosheka na wasiwe watu waliotawaliwa na tamaa, wanaoeneza matunda ya uhuru kwa wananchi wote kwa manufaa yao na maendeleo ya taifa kwa ujumla. Je CCM hiyo bado ipo?

  Katika mazingira ya sasa CCM isipate kigugumizi kuchukua ushauri wa mwalimu Nyerere kuwa Chama ni lazima kiwe cha wananchi na kwa manufaa ya wananchi. Ni kwa namna gani bepari ana uwezo wa kuleta mapinduzi ya kuondoa unyonyaji na ufisadi?

  Kukumbatia aina ya watu na viongozi ilionao sasa, CCM inajiweka katika mazingira magumu ya kuona na kukubali kuwa inajiweka mbali sana na wananchi wa kawaida wa Tanzania. Ndio maana kwa sasa hoja ya kujadili uamuzi wa kupunguza mshahara wa kima cha juu na kuongeza kima cha chini ni sawa na usaliti na uhaini.

  Nyerere anasema katika “The Party Must Speak for the People” kuwa chama ni lazima kiwasaidie wananchi kuelewa kinachofanywa na serikali ili waiunge mkono na kushirikiana nayo (kwa moyo mmoja) kuondoa umaskini ambao umeota mizizi. CCM iamke sasa na kubadili ilichowatumwa kina Mwinyi na wajiulize wajibu huu watauendeaje?

  Najua yapo mengi ambayo CCM inapaswa kushulika nayo sasa zaidi ya (upotofu?) wa wabunge wao kwa chama na niongeze moja kwa kifupi linalohusisha mabadiliko ya muundo na demokrasia. Kwa wakati wa sasa CCM na isikie kilio cha wanaoitakia mema Tanzania kuwa sasa idhamirie katika kukubali na kushiriki kwa uzalendo kuifanyia mabadiliko katiba yetu.

  Baadhi ya vitu vya kutilia mkazo ni suala la ruhusa ya kuwepo wagombea binafsi, tume huru ya uchaguzi, wabunge kukoma kuwa mawaziri na pengine kuwa na serkiali ya umoja wa kitaifa.

  Zipo faida nyingi ambazo zinahitaji makala nzima lakini baadhi ni kama ifuatavyo;
  Wagombea binafsi watapanua wigo mpana wa upatikanaji wa wenye sifa katika nafasi za uongozi badala ya hali ya sasa ambayo inawanyima wasiotaka kuwa wanachama wa vyama vya siasa nafasi ya kugombea na kushiriki uongozi wan chi yao

  Hili pia litazuia viongozi wa ovyo wanaotumia chaka la chama kuingia katika mfumo wa uongozi. Hapa wananchi watapima uwezo wa mtu binafsi badala ya rangi ya bendera ya chama chake na kuondoa fikra aliyoisema mwandishi Ayoub Rioba kuwa kwa sasa hata CCM ikisimamisha ng’ombe anaweza kushinda.

  La tume huru ya uchaguzi ni la muhimu kwa CCM inayobeza wapinzani wanaoipigia kelele pamoja na kwa taifa kwa jumla. Akitoa maoni yake (ya chama?) juu ya dai la CUF kuhusu tume huru ya uchaguzi katibu mwenezi wa CCM Chiligati anasema kuwa ni sawa lakini haoni umuhimu kwa kuwa hata Profesa Lipumba akiwa mwenyekiti wa tume hiyo CCM bado itashinda tu.

  Sidhani kama maoni haya ni sehemu ya kazi yake ya uensezi wa chama chake kwani ni hatari. Maoni haya yanajenga picha kuwa CCM inadhani demokrasia ni uchaguzi na kushinda uchaguzi kama alivyotafsiri mtaalamu wa siasa Schumpeter.

  Chama kikongwe na makini kama CCM lazima kielekee uchaguzi wa mwakani kikiwa kina lengo la kutafsiri demokrasia kuwa ni “ushiriki makini wa wananchi wote katika kuamua mustakabali wa taifa lao hata baada ya kipindi cha uchaguzi”. Sura ya kitaifa ndani ya tume ya uchaguzi ina maana zaidi ya kuiondoa CCM madarakani kama anavyodhani kapteni Chiligati na pengine CCM anayoieneza.

  CCM inaweza kuchelea kukubali changamoto hizi kwa upuuzi lakini matokeo yake yataliweka taifa katika hali iliyoikumba Kenya mwaka 2007. Watanzania si wajinga kusema hawana fikra au kamwe hawatachagua serikali nje ya CCM na hata mwalimu alionya 1995 kuwa “mfumo wa sasa unajenga uwezekano wa Rais wa Tanzania kutoka nje ya CCM”.

  Si lengo la makala hii kushabikia uwezekano huu ila kujiuliza je itakuwaje uwezekano huu ukitimia? Je CCM haitakimbilia kuvuruga amani ili wajenge mazingira ya kuundwa serikali ya mseto (ya umoja wa kitaifa?) na haja ya tume huru ya uchaguzi kwa miaka ijayo kama ilivyotokea Kenya na kwingineko Afrika?

  Kwa akili ya kawaida yenye kufanya kazi CCM inalazimika kupigania tume huru ya uchaguzi na serikali ya kitaifa kwa sasa kuliko vyama vya upinzani na pengine toafauti na wakati mwingine wowote. Hata hivyo wanaweza kuendelea kupuuza na basi itawapasa wakumbuke “watanzania wana mawazo ambayo si kama injini ya gari kwamba itaondoka kwa gia namba hii na kusimama kwa gia namba hii, bali mawazo yao huendeshwa na wakati na mahitaji”.

  Chaguzi za mwakani na kuendelea zitakuwa wapiga kura wengi ambao hawakuiona Tanzania ya miaka chini ya themanini na wengi wao hawana mbele wala nyuma waliotengenezwa kupitia utitiri wa shule za sekondari za kata ambazo ni ubunifu wa CCM an serikali yake.

  Kamati ya Mwinyi iachane na kuwalenga wabunge na wawakilishi kule Zanzibar na badala yake itafute au ielekezwe kutafuta changamoto hasa za CCM kuelekea uchaguzi mkuu mwakani na enzi mpya ijao.

  Wanahistoria wanasema, “ukoloni ulipingwa na wananchi lakini kiini cha ukombozi wa Afrika ulitokana na mbegu zilizopandwa na ukoloni wenyewe”. CCM isipofikiri kuwa adui wa CCM ni CCM basi itaendelea kuwa ni jumuiya iliyokosa DIRA na MWELEKEO.

  Mungu ibariki Tanzania.

  Salim Sengwira 0715883985,
  ngwirason05@yahoo.com.
   
 2. Sophist

  Sophist JF-Expert Member

  #2
  Oct 7, 2009
  Joined: Mar 26, 2009
  Messages: 3,087
  Likes Received: 1,731
  Trophy Points: 280
  Akagunju kalafa......
  Pole ndugu
   
Loading...