CCM sasa yawarusha roho wabunge wake | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

CCM sasa yawarusha roho wabunge wake

Discussion in 'Uchaguzi Tanzania' started by BAK, Jul 1, 2010.

 1. BAK

  BAK JF-Expert Member

  #1
  Jul 1, 2010
  Joined: Feb 11, 2007
  Messages: 70,813
  Likes Received: 83,195
  Trophy Points: 280
  Mwandishi Wetu
  Raia Mwema
  Juni 30, 2010

  [​IMG]Watakiwa kujieleza kabla ya uteuzi
  [​IMG]Wengi wahofia kukatwa majina


  WABUNGE 275 wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameagizwa kuandaa taarifa za utendaji wao wa kazi kwa kipindi chao cha ubunge, hatua ambayo inatajwa kuwa ni kukiwezesha chama hicho kufanya uamuzi muafaka wakati wa mchujo wa wagombea wa ubunge katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika baadaye Oktoba, mwaka huu, imefahamika.

  Mchujo wa majina ya wagombea ubunge kwa tiketi ya CCM hufanyika kwenye kikao cha Halmashauri Kuu (NEC) ya chama hicho ambacho hupokea majina ya wanachama waliopendekezwa na majimbo na Mkoa ili wateuliwe na NEC-Taifa kugombea kwa tiketi ya chama hicho.


  Taarifa ambazo Raia Mwema inazo na ambazo pia zimethibitishwa na wabunge wengi wa CCM wakiwamo wa majimbo, Viti Maalumu na hata wa kuteuliwa na Rais, zinabainisha kuwa ripoti za utendaji wa kila mbunge zinapaswa kuwasilishwa katika chama hicho mara baada ya kuvunjwa kwa Bunge.

  Bunge linatarajiwa kuvunjwa na Rais Jakaya Kikwete Julai 16, mwaka huu (takriban wiki mbili kuanzia sasa) ikiwa ni Bunge lenye rekodi ya kuvunjwa mapema zaidi, rekodi ambayo inaambatana na visingizio vya kupisha mchakato wa Uchaguzi Kuu unaoanzia katika vyama vya siasa.

  Hata hivyo, pamoja na taarifa hizo za visingizio kutoka serikalini na hata kwa kuzingatia maelezo ya Spika wa Bunge, Samuel Sitta, vyanzo huru vya habari vya kuaminika vinabainisha kuwa kuwahi kuvunjwa kwa Bunge kwa sehemu kubwa kunatokana na ufinyu wa bajeti, hasa baada ya wahisani kupunguza misaada yao katika bajeti ya kitaifa.

  “Tumetakiwa kuwasilisha ripoti ya utendaji katika kipindi chetu cha ubunge,” alithibitisha mmoja wa wabunge kutoka Nyanda za Juu Kusini na akaongeza kuwa ni ripoti zinazotakiwa kuwasilishwa mara baada ya kuvunjwa kwa Bunge na Rais Kikwete, maelezo ambayo yaliungwa mkono na wabunge wengine 10 wa majimbo waliozungumza na Raia Mwema lakini hata hivyo wakikwepa majina yao kuandikwa gazetini kwa kuhofia kile walichoeleza si wakati muafaka wa kuzungumzia maagizo ya chama magazetini hasa kipindi hiki cha kusubiri kuteuliwa kugombea tena ubunge.

  Viongozi wa juu wa CCM hawakuweza kupatikana mara moja kuzungumzia masuala mawili muhimu ambayo ni kwanza; utaratibu wa uwasilishaji wa ripoti hizo za wabunge wa chama hicho lakini pili chama kitahakiki vipi taarifa za wabunge hao kama ni za kweli kwa asilimia 100 ikizingatiwa kuwa katika baadhi ya majimbo, wabunge na viongozi wa chama hicho wamegeuka kundi lenye kulinda maslahi yao binafsi.

  Hata hivyo, gazeti hili limeelezwa na baadhi ya wabunge kuwa kwa upande wa wabunge wa Viti Maalumu, taarifa zao za utendaji zitawasilishwa katika Umoja wa Wanawake wa chama hicho (UWT) na tayari wabunge hao wa Viti Maalumu wameandikiwa rasmi barua kuhusu agizo hilo.

  Uchunguzi wa gazeti hili kwa kuhusisha baadhi ya wajumbe wa NEC-CCM umebaini kuwa ripoti hizo za wabunge ndizo nguzo muhimu itakayotumika na viongozi wa CCM kujiridhisha kuwa nani aendelee kuteuliwa kugombea kwa tiketi ya chama hicho na nani aachwe.

  Aidha, kigezo hicho cha ripoti pia kinatajwa kuhusisha vigezo vingine ikiwa ni pamoja na kulinganisha nguvu za wagombea watarajiwa wa vyama vya Upinzani na huyo mtarajiwa wa CCM.

  Kwa mujibu wa taarifa hizo za wajumbe wa NEC waliozungumza na gazeti hili, katika baadhi ya majimbo wabunge wa CCM wamepoteza mvuto wa kisiasa na wengine hawana uhusiano mzuri na wana-CCM wa kawaida wakibainika kuwekeza zaidi kifedha kwa viongozi wa chama hicho hali inayotarajiwa kuwagharimu hasa baada ya utaratibu wa chama hicho kupata wagombea kubadilika kutoka kuhusisha viongozi wa jimbo pekee hadi wanachama wote wa jimbo kwenye matawi yao.

  Kwa sasa, idadi ya wabunge wa majimbo wa CCM bungeni ni 205 kati ya viti vyote vya majimbo 230, viti viwili vya majimbo vilivyokuwa vikishikiliwa na CCM viko wazi katika Majimbo ya Ruangwa mkoani Lindi na Kishapu mkoani Shinyanga. Jimbo la Ruangwa lilikuwa likiwakilishwa Sigifrid Ng’itu (marehemu) na Kishapu lililokuwa likiwakilishwa na Fred Mpendazoe aliyeikimbia CCM na kujiunga na chama chenye usajili wa muda cha CCJ.

  CCM pia ina wabunge tisa wa kuteuliwa na Rais kati ya 10 anaoruhusiwa kwa mujibu wa Katiba. Mmoja wa hao 10 ni Ismail Jusa Ladhu aliyeteuliwa kutoka Chama Cha Wananchi (CUF).

  Wabunge wengine watatu wa CCM kati ya watano ni kutoka katika Baraza la Wawakilishi Zanzibar. Idadi ya wabunge wa Viti Maalumu wa CCM ni 58. Idadi hizo za wabunge zinafanya CCM kuwa na jumla ya wabunge 275 kwa sasa kati ya nafasi 323 za wabunge kwa mujibu wa Katiba.
   
Loading...