CCM sasa imerudi kwa wenye chama

CCM sasa imerudi kwa wenye chama

kalulukalunde

JF-Expert Member
Joined
May 27, 2016
Posts
1,056
Reaction score
1,086
FEBRUARI 5, mwaka 1977, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kilizaliwa. Mama wa chama hiki ni TANU na ASP. CCM imepita katika historia ndefu na vipindi vingi vyepesi na vigumu mno. Chama hiki kwa sasa ni miongoni mwa vyama vikongwe vya ukombozi Afrika na Kusini mwa Jangwa la Sahara.

Katika makala haya nitaelezea dhana ya Chama kurudi kwa wenye chama/wanachama. Ndiyo, Chama ni cha wenye chama/wanachama. CCM imetokana na wananchama. Ikaishi na kuwakumbatia kwa karibu wanachama, kuna wakati chama kilikenguka na kukengeushwa. Chama kilitoka kwa wananchama na kuwasahau. CCM ikawa ya wafanyabiashara mabepari na viongozi wa chama. Chama kiliwakumbatia walio na nguvu ya kiuchumi na wenye ushawishi mkubwa kwa chama. Wanyonge na tusio na kipato tulikata tamaa ya kushika hatamu za uongozi wa chama.

Baada ya chama kujitafakari kwa kina na kutathmini mwenendo wake, chama sasa kinarudi kwetu sisi wanachama. Nitajadili kwa kina vipindi hivyo vikuu vitatu ambavyo CCM imepitia.

Alama ya Chama Cha Mapinduzi ni jembe na nyundo. Maana ya alama hii ni kuwa chama hiki ni chama cha wakulima na wafanyakazi. Chama hiki kimerithi umoja na mshikamano, utu wema na kuwajali wanyonge toka kwa mama wa Chama hiki; TANU na ASP. Kwa miaka mingi CCM imekuwa kimbilio la wanyonge.

Kila mmoja ni shahidi wa namna CCM ilivyowajali Watanzania masikini kupitia kwa viongozi wake na Serikali iliyoiongoza tangu uhuru. Azimio la Arusha liliweka misingi imara ya Chama na viongozi wanaotokana na chama kuishi maisha ambayo hawatayaweza wananchi wanyonge. Umoja na usawa wa kibinidamu ilikuwa ni dira kubwa ya Chama.

Kuthibitisha hilo hata ahadi kumi za mwanachama wa TANU zilitanabaisha. TANU ilijipambanua kuwa chama kwa ajili ya wanachama. Viongozi na wanachama walikuwa wanatakiwa kuziimba ahadi kumi za mwana-TANU na kuishi katika maisha yao ya kila siku. Moja ya ahadi hiyo ilitamka wazi kuwa ‘binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja’. Nyingine kwa kuzingatia ubaya wa rushwa na madhara yake kwa jamii, ilitamka wazi kuwa ‘rushwa ni adui wa haki, sitapokea wala kutoa rushwa’. Na nyingine inaweka imara misingi ya uongozi kuwa ‘cheo ni dhamana, sitakitumia cheo changu wala cha mtu mwingine kwa faida yangu.’

CCM mtoto wa TANU kuna wakati ilikuwa ikilaumiwa mno na makada na wanachama wa chama hiki kuwa chama kimekumbatia rushwa katika nafasi za uongozi. Ilikuwa ni vigumu mno kwa makabwela kuwania nafasi za uongozi chamani na kushinda nafasi hizo. Kwa kipindi kirefu CCM ilijawa na baadhi ya viongozi wasio waaminifu, walioendekeza ubinafsi, uchoyo, uchu wa madaraka na matumbo yao. Hawa waliichafua sana taswira ya chama kwa wanachama. Walisababisha wanachama kukata tamaa na mwenendo wa chama na kukikataa chama.

Chama kilijaribu mara nyingi kuwaengua makada hao wasiokuwa waaminifu chamani ambao walitumia vyeo vyao kwa manufaa yao bila mafanikio. Tutakumbuka kuwa kuna wakati CCM kupitia Katibu mkuu wake mstaafu, Wilson Mkama na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa wakati huo, Nape Nnauye, walitangaza mkakati kabambe wa kuvua magamba, wakilenga kuwaengua makada wake waliokuwa wakituhumiwa kwa rushwa na utovu wa nidhamu. Mkakati huo uligonga mwamba kwa kuwa chama hakikuwa tayari kufanya mageuzi makubwa ya kimfumo na kimuundo. Sabubu nyingine ni wanamtandao kujiimarisha katika kila ngazi ya chama na kufanya chama kushindwa kusimamia maamuzi yake.

Mbali na hilo, Rais wa Awamu ya Nne ambaye pia alikuwa Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais mstaafu, Jakaya Kikwete, aliwahi kutangaza mkakati wa kuwaengua viongozi wa chama na Serikali ambao wanajihusisha na biashara pia. Alitaka kutofautisha kati ya wafanyabiashara na wanasiasa.

Hii ni kwa sababu wafanya iashara matajiri walikuwa wakitumia uwezo wao wa kipesa kuwashawishi na kuwanunua wananchi ili wawapigie kura za ndio. Baadhi ya viongozi hao hawakuwa na uwezo wa kiuongozi bali walitamani nafasi za uongozi wa chama na Serikali ili waweze kutumia vyeo vyao kwa manufaa yao na si ya watu wengi. Hawa walikuwa tayari kununua au kuuza uongozi wa chama na Serikali kwa gharama yoyote ile.

TUJIKUMBUSHE KAULI TATA ZA VIONGOZI WA CCM

Marehemu Horace Kolimba aliyepata kuiongoza CCM, kwa nafasi ya ukatibu mkuu, aliwahi kutamka wazi kuwa CCM imepoteza dira na mwelekeo. Kauli hii iliyotoka kwa katibu mkuu wa chama wa wakati ule haikuwa ya bahati mbaya.

Kolimba aliona jinsi rushwa ilivyotamalaki katika chama na akahofia chama kupoteza dira na mwelekeo wake ambao kimsingi, dira na mwelekeo wa chama ni kuhakikisha chama kinabaki kuwa cha wanachama na kinatetea misingi ya haki, utu, umoja na mshikamano wa Tanzania. Ninaamini kauli hii haikutamkwa kwa bahati mbaya na katibu huyu wa chama, aliiona hatari iliyo mbele ya chama.

Kauli nyingine tata ilitolewa na Katibu Mkuu mstaafu wa CCM ambaye kwa sasa ni Makamu Mwenyekiti wa CCM bara, Philip Mangula. Yeye baada ya kustaafu nafasi ya Ukatibu Mkuu wa Chama, alirudi mkoani Iringa/Njombe na kugombea nafasi ya Uenyekiti wa Mkoa wa CCM.

Hali ilivyokuwa katika mwenendo wa uchaguzi, jinsi rushwa na mizengwe ilivyotamalaki, Mangula aliseama: “Kama chama kitafumbia macho rushwa, itafika wakati nafasi za uongozi zitatangazwa kwa mtindo wa zabuni. Mwenye pesa nyingi ndiye atakayeshinda zabuni ya uongozi.

Rushwa ilitamalaki chamani. Ikawa inawatisha hata makada wakubwa wa CCM. Waliiona hatari ya chama kuwakumbatia baadhi ya makada wanaoendekeza rushwa na kugeuza kuwa rushwa ndio mfumo rasmi wa kupata uongozi chamani na serikalini.

Aliyewahi kuwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnaye, hivi karibuni alipigilia msumari wa mwisho juu ya malalamiko ya viongozi na wanachama juu ya mwenendo na hali chama kilipofikia. Nape alisema CCM ilitolewa shimoni. Tujiulize ni shimo lipi CCM ilitumbukia? Kwanini ilitumbukia? Nani aliitumbukiza CCM shimoni?

Hapa kuna mjadala mpana zaidi. Picha tunayoipata hapa ni kwamba CCM ilitumbukizwa shimoni na makada waliotumia vyeo vyao kama dhamana ya matakwa yao. Pia, tunapata picha kuwa CCM ilitumbukizwa shimoni na viongozi wa chama walioamini na kuendekeza rushwa pasi na kujali kuwa rushwa ni adui wa haki na kukataa kupokea wala kutoa rushwa. CCM ilitumbukizwa shimoni na viongozi waliouweka kando undugu na ujamaa wa Kitanzania na kutozingatia kuwa binadamu wote ni ndugu na wana haki sawa.

HALI ILIVYO SASA

Kuwa mwana-CCM sasa ni fahari. Kuvaa sare rasmi za chama hicho sasa ni fahari pia kwa mwanachama yeyote. Ndiyo, Chama hiki sasa kimerudishwa kwetu sisi wananchama. Kero kuu ya rushwa imeshughulikiwa kwa kiwango cha kutia moyo. Urasimu, umangimeza, umungumtu sasa imebaki historia kwa chama hiki. Rushwa inadhibitiwa vya kutosha.

Kilio kikubwa kwetu sisi wanachama ilikuwa ni rushwa na kutotoa fursa sawa za uongozi. Matajiri waliokihodhi chama hiki kama mali yao binafsi sasa hawana nafasi tena. CCM imerudi kuwa ya wakulima, wafanyakazi na wanyonge wa nchi hii.

Mfano ulio rahisi ni hili zoezi la uchaguzi mkuu wa chama linaloendelea sasa, kuanzia ngazi ya shina. Miaka ya nyuma zoezi hili lilighubikwa na tambo, rushwa na kila aina ya urasimu. Ilivyo sasa ni tofauti. Zoezi hili kwa sasa linakwenda vizuri mno, licha ya fomu za kugombea kutolewa bure pia hakuna urasimu wa kuwania nafasi yoyote. Rushwa imedhibitiwa kikamilifu na mianya ya kutoa au kupokea rushwa imezibwa.

CCM kupitia kwa Rais wake wa Awamu ya Tano, John Magufuli, imerejesha imani ya Watanzania kwa chama kwa asilimia kubwa mno. Jinsi Rais Magufuli anavyopambana kutatua kero sugu za Watanzania na jinsi anavyopambana na rushwa, urasimu na ufujali, Chama hiki sana kinaonekena kuzaliwa upya na kuongeza imani kubwa kwa wananchi. Wananchi wazalendo wapenzi wa chama hiki wasema kwa sauti kuu, CCM ya Magufuli sasa imerudi kwa wenye chama. Ikiwa chama hiki kitaendelea na mwendo huu, wapinzani watasubiri sana na uchaguzi wa mwaka 2020 njia nyeupe. Tunabaki tukiamini kuwa bila CCM imara, nchi yetu itayumba.
 
Hakuna Lolote Makala Ndefu Ndani Hakuna Lolote.Ccm Ni Ile Ile Usani Usanii Utapeli Rushwa Ufisadi Ndyo Kazi Yao.Tuambie Tangia Huyu Mwenyekiti Wako Huyu Mpya Angie Lipi Kimefanyika?Zaidi Yakulindana Mf Mzuri Bashite
 
97b15bf01d4ba4e6816061db8c1ff5de.jpg
 
Back
Top Bottom