CCM Ndiyo inaleta uhasama wa kidini

Rugemeleza

JF-Expert Member
Oct 26, 2009
668
136
Uhasama wa kale warejea baada ya uchaguzi


picture-4.jpg

Na Saed Kubenea - Imechapwa 10 November 2010

Gumzo la Wiki


UCHAGUZI mkuu wa rais, wabunge na madiwani umemalizika kwa kuibua hata yale yaliyoanza kusahaulika.
Miongoni mwa yaliyoibuka upya ambayo yalianza kusahaulika, ni mnyukano kati ya serikali na wananchi; serikali na madhehebu ya kidini na chama kilichopo ikulu na vile vilivyo nje ya utawala.

Hata baadhi ya watuhumiwa wakuu wa ufisadi nchini, Rostam Aziz na Edward Lowassa, walijitokeza katika kujibu kile walichoita, "Tuhuma za uwongo" dhidi yao.

Kwanza, hatua ya serikali kutuhumu baadhi ya viongozi wa madhehebu ya kidini nchini, kwamba wanahubiri siasa katika madhehebu yao kwa lengo la kubeba mgombea mmoja wa urais, ni ufa mpya ulioibuka kati ya serikali na madhehebu ya kidini nchini.

Mara kadhaa serikali ilituhumu baadhi ya viongozi wa madhehebu haya kumpendelea mgombea urais kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa.

Viongozi wa serikali walisema baadhi ya viongozi wa kidini wamekuwa wakiendesha kampeni za kumpinga Kikwete kwa kuwa wanamuunga mkono Dk. Slaa. Hata pale ambapo baadhi ya watuhumiwa walikana madai hayo, utetezi wao haukusikilizwa.

Msimamo huu wa serikali ulimuingiza hata rais mstaafu Benjamin Mkapa. Akihutubia mkutano wa mwisho wa kampeni katika viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam, Mkapa aliendelea kushusha lundo la tuhuma kwa viongozi wa dini.

Minyukano kati ya serikali na madhehebu ya kidini iliibuka katika chaguzi mbili zilizopita. Wakati huo, mlengwa mkuu alikuwa Profesa Ibrahim Lipumba na chama chake – Chama cha Wananchi (CUF).
Waliotuhumiwa na hata kushambuliwa hadharani kumbeba Profesa Lipumba, walikuwa viongozi wa madhehebu ya kiislamu.

Hata pale baadhi ya viongozi wa madhehebu ya kiislamu walipokana madai hayo, serikali na viongozi wa Chama Cha Mapiduzi (CCM) waliendelea kusisitiza kuwa CUF, ni chama cha kidini.

Kama ilivyokuwa mwaka 2000 na 2005, madai ya udini safari hii yalielekezwa CHADEMA. Ni kweli kwamba wengi walizipuuza tuhuma hizi kwa kuwa zilionekana ni "mkakati wa CCM kutumia kichaka cha kidini," kukimbia tuhuma zinazokabili viongozi wake.

Hata hivyo, hatua ya badhi ya viongozi wa serikali kuhoji uadilifu wa viongozi wa kidini katika kusimamia kile wanachokinena kwa waumini wao, hakiwezi kuwafanya viongozi hawa kuwa wepesi kusamehe.
Pili, mbali na uhasama kati ya serikali na baadhi ya madhehebu ya kidini, uchaguzi uliomalizika umepandikiza chuki miongoni mwa madhehebu.

Kile kilichoitwa "upendo na kuaminiana," miongoni mwa wananchi na waamini na waumini wa madhehebu ya dini, sasa kimeanza kutoweka.

Hivyo basi, pamoja na wito ulitolewa na Rais Jakaya Kikwete kutaka wananchi waungane kulirejesha taifa katika umoja, kwa jinsi mashambulizi yalivyoendeshwa, itawachukua muda mrefu viongozi hawa kusahau kilichotokea.

Tatu, kuhusu uhasama kati ya vyombo vya dola na wananchi, hili nalo haliwezi kwisha bila juhudi za dhati kufanyika.

Hakuna anayeweza kubisha kuwa katika uchaguzi huu, viongozi wa vyombo vya dola walivunja maadili ya kazi yao na kuamua kutumiwa na viongozi wa CCM na serikali yake.

Katika baadhi ya maeneo, kama vile Kilimanjaro, Mwanza, Karagwe, Kigoma, Mbeya na Shinyanga, vyombo vya dola vilijigeuza kuwa idara ya CCM. Vilitenda kile kilichoagizwa na viongozi hao.

Matokeo yake, baadhi ya wananchi waliokuwa wamesimama kidete kutaka kuona vyombo vya dola vinasimamia haki, walishambuliwa, wengine walijeruhiwa, wengine wamepata vilema vya maisha na wapo wanaoripotiwa kupoteza maisha.

Kwa mfano, mkoani Shinyanga, taarifa zinasema, jeshi la polisi lilishambulia kwa mabomu waumini wa dini ya kiislamu waliokuwa katika nyumba yao ya ibada.

Ni baada ya kutaka msimamizi wa uchaguzi jimbo la Shinyanga Mjini kumtangaza yule waliyedai kuwa "mshindi halali wa uchaguzi."

Wananchi walidai kuwa mgombea ambaye alistahili kutangazwa ni yule wa upinzani. Lakini madi yameenea kuwa msimamizi wa uchaguzi alishinikizwa kumtangaza mgombea wa CCM.

Katika eneo hili, polisi wanatuhumiwa kushindwa kusimamia sheria kwa kuhakikisha mshindi halali ndiye anayetangazwa. Badala yake, walishirikiana na CCM kubariki uhalifu uliominya demokrasia.

Hata mgogoro kati ya vyama vya siasa na serikali, ambao umeibuka katika uchaguzi huu, hauwezi kuisha kwa kauli rejereja za rais.

Haikutarajiwa kuwa baada ya serikali kufanikiwa kumalizika minyukano ya muda mrefu kati yake na chama cha CUF visiwani Zanzibar, mgogoro ambao ulisababisha mauaji ya raia 24 hapo Januari 26 na 27 Unguja na Pemba, iruhusu kufumuka kwa jambo jipya.

Ilitarajiwa kuwa serikali ingetumia kila njia kuzuia hicho kutendeka.

Lakini sasa ni wazi kuwa mgogoro mpya utaibuka kati yake na wafuasi, wanachama na viongozi wa chama kikuu cha upinzani nchini – CHADEMA.

Tayari Dk. Slaa na chama chake wamegoma kutambua matokeo yaliyompa ushindi rais Kikwete na rais mwenyewe. Amegoma kuhudhuria sherehe za kumtangaza mshindi; kuapishwa rais na dhifa iliyoandaliwa baada ya rais kuapishwa. Anasema matokeo hayo yalichakachuliwa na yaliandaliwa maalum na Idara ya Usalama wa taifa ili kumbeba mshindani wake mkuu.

Serikali makini inayosikiliza sauti za wananchi, ilitakiwa kuwa na kazi moja tu: Kuheshimu matakwa ya raia wake. Basi! Bali kwa kuwa serikali iliyopo si sikivu, haijali maslahi ya wananchi na imejikita katika kutimiza matakwa ya kikundi kimoja, huo ndio msingi wa haya yaliyotokea.

Kuhusu Lowassa na Rostam, wawili hawa wamejitokeza kukana kile walichoita, "Madai ya kipuuzi ya Dk. Willibrod Slaa."Tuanze na Lowassa. Katika andishi lake kwa baadhi ya vyombo vya habari nchini anakana kuwa Mwanza ambako Dk. Slaa alinukuliwa akisema kuwa kunadaiwa kufanyika mkutano ulioshirikisha hata na kiongozi mkuu wa nchi.

Lakini Dk. Slaa hakusema kwamba Lowassa, Rostam na wengine wote waliotajwa walihudhuria mkutano huo. Alichosema ni kuwa chama chake kimekamata barua ya Willison Kabwe ambayo imetaja kuwapo kwa mkutano na kuhudhuriwa na viongozi hao.

Alidai kuwa barua hiyo ya Kabwe inaagiza wasimamizi wa uchaguzi katika majimbo ya Mwanza kusaidia wagombea wa CCM; chama chake kiliwasilisha barua hiyo kwa Kabwe ambaye alishindwa kuikana.

Alifika mbali zaidi. Alisema maudhui ya barua hiyo ndio msingi wa kilichotendeka katika uchaguzi nchi mzima.
Lakini badala ya Lowassa kumtaka Kabwe kuthibitisha maelezo yake, ameibuka na kumrukia Dk. Slaa, kwamba anafanya siasa za "uongo, uvumi, uzushi na kila aina ya hila kwa nia ya kujipatia ushindi."
Lowassa ni nani katika sakata hili? Anamsemea nani? Inawezekana ama hajijui au amejisahau. Yeye ni miongoni mwa mabingwa wa siasa za uzushi, uwongo na kuchafua waliosafi miongoni mwao.

Nani amesahahu kuwa tuhuma za mauaji alizoshushiwa Dk. Salim Ahmed Salim mwaka 2005 zilipikwa na kundi la mtandao uliokuwa chini ya uenyekiti wa Lowassa? Wahusika wakuu katika mkakati huo, walikuwa ni waandishi wa habari wawili, Muhingo Rweyemamu na Said Nguba. Mara baada ya kazi waliyotumwa na Lowassa kukamilika, Nguba aliteuliwa kuwa afisa habari wa ofisi ya waziri mkuu.

Hata tuhuma zinazoelekezwa kwa Samwel Sitta, kwamba amevuruga Bunge, ameharibu chama na ameendesha siasa za makundi; muasisi wake ni Lowassa.Ni kwa sababu, Lowassa bado ana kinyongo cha kupoteza uwaziri mkuu. Lakini jingine ni hili: Lowassa ni bingwa wa kukana hata yale ambayo ametenda mwenyewe, tena hadharani.Ushiriki wake katika mkataba wa kinyonyaji wa Richmond na yaliyojiri baada ya kujiuzulu nafasi hiyo, ni ushahidi tosha wa kutoaminika kwake.

Naye Rostam ambaye amekana kama Lowassa, kuhusika na madai ya wizi wa kura, anafahamika jinsi alivyo kinyonga. Hata katika usajili wa makampuni yake mwenyewe, jina lake halionekani.

Mara kadhaa amekuwa akikana kuhusika na kampuni ya New Habari inayochapisha magazeti ya Rai, Mtanzania, The African, Bingwa na Dimba. Lakini alipobanwa na waandishi wa habari katika moja ya mikutano yake, Rostam alijisahau na kukiri kuwa kampuni hiyo ni mali yake.

Hata hivyo, nyaraka zilizopo kwa Wakala wa Serikali wa Usajili wa Biashara na Makampuni (BRELA), jina la Rostam halionekani.

Katika mazingira hayo, utetezi wa Rostam unapaswa kutiliwa shaka na hata kupuuzwa.
Lakini swali moja ni muhimu tukajiuliza: Nani ametufikisha hapa? Jibu liko wazi. Tumefikishwa hapa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Chombo hiki kilichopewa mamlaka ya kusimamia uchaguzi; kuratibu na kuendesha zoezi la uchaguzi kwa njia za wazi, kimeshindwa kazi yake. Katika maeneo mengi, NEC imeshindwa kusimamia sheria ya uchaguzi. Imeshindwa kukemea wavunjaji wa sheria na imefumbia macho malalamiko yaliyowasilishwa kabla ya matokeo kutangazwa.

Kwa mfano, katika maeneo mengi, uchaguzi umevurugika, hasa wakati wa kupokea matokeo, kuhesabu kura na kusimamia ulinzi wa kura.

Angalia jimboni Nyang'wale, wilayani Geita, mkoani Mwanza. Matokeo yaliyotolewa na NEC yanatofautiana kwa kiwango kikubwa na matokeo ya msimamizi wa uchaguzi. NEC inaonyesha katika matangazo yake kuwa Ngulu Tanganyika wa CHADEMA ndiye aliyeibuka mshindi. Inasema alipata kura 23,290.Lakini msimamizi wa uchaguzi amemtangaza Hussen Amar wa (CCM) kuwa mshindi. Huyu kwa mujibu wa mtandao wa NEC amepata kura 19,987 akiachwa nyuma na Tanganyika kwa zaidi ya kura 4,000.

Hata katika kura za urais, kumesheheni lundo la kasoro. Hivyo tukiendelea kujidanganya kwamba uchaguzi haukuwa na matatizo, bali kulikuwa na kasoro ndogo kama inavyopenda kuelezwa, tutakuwa tunajidanganya.
NEC imeichukua karibu wiki moja kuhesabu kura 8 milioni – asilimia 23 ya wapiga kura. Je, ingekuwaje kama watu 18 milioni wangejitokeza kupiga kura?

Kama waliojitokeza hawakufika hata nusu ya wapigakura, wangejitokeza asilimia 80 ya wapigakura, taifa hili lingekuwa wapi hivi sasa?

Nani angeweza kuzuia wananchi kutuhumu NEC kuwa inataka kuchakachua matokeo?
Kabla ya kutibu vidonda vya uchaguzi ni muhimu rais wa nchi angetangaza kuivunja NEC ili kuwapa imani wananchi kuwa naye yupo na ana dhamira njema na taifa.

Vinginevyo, ugonjwa huu wa kutibu majeraha utaibuka kila uchaguzi unapomalizika. Mwisho donda litakuwa sugu na litashindwa kupona. Ni vema tusifike huko.

Gazeti toleo na. 214
 
Lakini swali moja ni muhimu tukajiuliza: Nani ametufikisha hapa? Jibu liko wazi. Tumefikishwa hapa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Naomba nimsahihishe kidogo kubenea; aliyetufikisha hapa ni JK na UT kwani NEC ilifanya yote haya chini ya maagizo/maamrisho yao
 
Back
Top Bottom