CCM na hatma ya Tanzania | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

CCM na hatma ya Tanzania

Discussion in 'Jukwaa la Siasa' started by kilimasera, Apr 8, 2011.

 1. kilimasera

  kilimasera JF-Expert Member

  #1
  Apr 8, 2011
  Joined: Dec 2, 2009
  Messages: 3,073
  Likes Received: 17
  Trophy Points: 135
  Sammy Makilla

  HIVI majuzi Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, alizungumzia umuhimu wa wana-CCM wenzake kutambua umuhimu na faida za kuzungumzia mambo yanayowahusu pale panapostahili na sio ovyo ovyo vichochoroni.

  Nyuma kidogo ya hapo, gazeti hili lilichapisha makala iliyokuwa na kichwa: ' Dalili za chama chenye hatari ya kusambaratika,' na baadhi ya yaliyokaririwa huko bila kificho yalidhamiriwa kuihatarisha CCM kwamba kule inakokwenda sio kuzuri.


  Tumefarijika na Waziri Mkuu kuliona hilo na kulimaizi waziwazi na kwamba kwa sasa faida na manufaa ya Watanzania kuwa na vyama vinavyojiendesha kiakili, kistadi na kimkakati sio kitu kisichofahamika tena. Na yeyote anayebisha hili ni mtu aliyezoea tu kubisha na asiyekubali ukweli unapojidhihirisha.


  Kweli idadi ya Watanzania imeongezeka. Lakini na matatizo yao vilevileyanaongezeka. Ajira ni chache (tofauti na redio ya CCM inavyodai), uzalishaji mali Tanzania sekta zote bado duni mn, umeme tatizo sugu, maji usiseme pamoja na ahadi kabakaba; taasisi babaishaji kawaida, rushwa palepale, mfumuko wa bei mtindo mmoja, kilimo kwanza bila zana zetu wenyewe usanii, viwanda vyetu vimelemazwa na tatizo la nishati na ubunifu; na maradhi kama sio 'babu' hata viongozi wenyewe wangelikuwa hatarini, na matatizo ya kawaida ya wananchi yanaachiwa kuwa matatizo mwaka nenda, mwaka rudi. Uhalisia huu wa mambo unashadidia umuhimu wa CCM kujizaa upya na kuwa na mkakati maridhawa wa kupambana nayo.


  Sifa za kiongozi bora ni jambo lililoanishwa vyema na Guru wa Menejimenti, hayati Peter Drucker katika kitabu chake cha The Effective Executive. Kiongozi bora kama alivyoainisha Prof Drucker ni mtu mwenye sita zifuatazo: Awe anajua atatoa mchango gani kwa taasisi au chama chake; anaujua na kuupanga muda ili utumike kuiendeleza taasisi yake na sio vinginevyo; anavifahamu vipaumbele vyake na hufanya kazi kwa kuvizingatia; anatambua uwezo na udhaifu wa walio chini yake na jinsi ya kuwahamasisha ili uwezo na mazuri yao yashinde udhaifu wao na juu ya yote ni mtekelezaji mambo na sio mropokaji au mwimbaji upuuzi kila wakati. Ni vyema katika kutathmini nafasi yao kisiasa hivi leo nchini, CCM ijipime na kuona kama kweli ina viongozi wa aina hiyo hapo juu na wanaolingana na majukumu yaliyoainishwa hapo juu na Profesa Drucker.


  Nina wasiwasi pia hivi leo kwa Mkutano Mkuu kuwa ndio chombo cha juu kabisa cha chama sio jambo zuri. Na vilevile utaratibu wa kofia mbili nao ninaona katika miaka hii una kasoro kubwa na walakini. Maana, matokeo yake ndiyo hayo kwamba viongozi wa zamani kwa kukosa nafasi yoyote ya uongozi katika chama wanaishia kuwa wakosoaji, wambeya na wazushi wa hili au lile.


  Ninauliza pia kwa hiyo, je, haiwezekani kuwa na Baraza la Wazee wa CCM kwa mujibu wa katiba ya chama hicho ambalo litaendeshwa kama chombo huru ndani ya chama, lakini kikiwa ni chombo cha ushauri na ukosoaji ndani ya chama tu na sio la kiutendaji? Hili halitasaidia, kuwapa nafasi viongozi wa zamani ambao hawana kazi, na sasa wanaongezeka kila siku ifutikayo kwenye kalenda?


  Kitaifa hili ni pacha na suala la kuwa na Bunge la Juu pia kwa minajili ya kuwaleta pamoja viongozi wa zamani na wanataaluma na makundi mbalimbali ya kijamii, ili bunge hilo liweze kusaidiana na bunge la wawakilishi wa wananchi. Bunge ambalo litasaidia pia kupunguza idadi kama sio kuwaondoa kabisa wabunge wa kuteuliwa kwnye bunge la sasa.


  Ninaamini katika kuangalia uwezekano wa hayo hapo juu, CCM itawapa wastaafu wake na wanaharakati wengine fursa ya kuwa na maeneo yao ya kumwaga sera na kuunga au kupinga kauli, au uamuzi wowote unaofanywa na viongozi waliopo madarakani kwa njia muafaka na ya kistaarabu zaidi. Katika miaka hii ni kosa kwa kikundi chochote katika jamii kujifanya kuwa kina akili, busara na hekima kuliko wananchi wote wakiwekwa pamoja.


  Mfano unaooneshwa na CCM hadharani hivi leo unawatia wananchi mashaka, tena mashaka makubwa sana. Wengi wanajiuliza kama chama tawalal kinashindwa kusimamia vyema mambo yake ya ndani, je, kitayamudu vipi yale ya kitaifa, tena kwenye nyakati ambazo mihogo michungu imeota kila kona ya shamba?


  Jambo lingine ambalo chama tawala kinafaa kujiuliza ni kwamba bila kuwa na mpango-mkakati uliotungwa kwa kuwashirikisha viongozi wote toka ngazi ya shinda hadi taifa, je, kitaweza kuhimivili vishindo vya huko tunakokwenda.


  Tukiacha maneno ya kiswahili ambayo huwa ynnatuchanganya saa zingine tujiulize je, leo CCM ikiulizwa nini VISHENI (VISION) yake itakuwa na la kujibu kitaalamu na sio kiuswahili ? Na, je, MISHENI (mission) ya CCM katika Tanzania ni nini? Kweli, CCM imerithi yaliyoachwa na waasisi wake na je, ni yote yanayofaa katika miaka hii au kuna yaliyopitwa na wakati na hawastahili kusita kuyatupa kwenye kapu la takataka za historia?


  Kwa maneno mengine uwepo wa mpango-mkakati utaisadia sana CCM kujiuliza na kujibu maswali kama vile: Chama sahihi na jumuiya zake zinataka kuwa kitu gani baada ya miaka mitatu hadi minne toka sasa; pengo lililopo kati ya matarajio na pale ilipo hivi sasa likoje; nini ulikuwa udhaifu dhidi ya uwezo au nguvu zake jana, leo na itakavyokuwa kesho; ni fursa na hatari zipi zilizo mbele yake na ni mbinu au mikakati gani ifanyike ili kuwe na fikra,mwono, mtazamo, msimamo na vitendo chanya vya kuvipa ushindi chama dhidi ya majaribio mbele yake na kikafaulu kuwapeleka Watanzania kule wanakotaka kuwa baada ya miaka mitatu hadi mine !


  Aidha, ni muhimu kwa mipango ya utekelezaji, utekelezaji wenyewe, ufuatiliaji na udhibiti wake vioanishwe na mipango mikakati ya jamii kuanzia ngazi ya mtaa, kata, tarafa, wilaya, mkoa hadi taifa kwa kuwa chama ni sehemu tu katika ulimwengu wa nchi na mambo yake.


  Kweli jumui ya za chama hicho zimefanya uchaguzi na sasa zina viongozi wake, isipokuwa ninaamini kilichofanyika ni kutanguliza gari la farasi mbele na farasi kuja nyuma. Ushuhuda wa hili ni kauli na vitendo vya viongozi wa taasisi hizo zinazotia mashaka kama viongozi wake wamefundwa na wanaijua, kuikubali na kuitekeleza visheni ya chama, kama chama kinayo visheni hiyo hivi leo! Na swali kubwa ni je tunachagua viongozi wetu kutokana na nani mtoto wa nani au ni maarufu kiasi gani au kutokana na uwezo wake kama kiongozi? Umaarufu na uwezo wa kuongoza ni vitu viwili tofauti.


  Uongozi unaoshirikisha watu kidunchu au usioshirikisha watu kabisa katika mipnagona maamuzi yake siku zote hujikuta ikiwajibika kujipanga na kujieleza upya tena na tena na mwishowe kuwa imo katika biashara ya ahadi na maneno kwa wingi, lakini hakuna cha manufaa kwa wananchi kinachofanyika. Hali ikifikia hivyo, maswali ya wananchi huzidi kuongezeka. Na wale wanaojiingiza papo kwa papo na kutoa majibu ya mkato fumba na kufumbua huwa ni wababe na mashujaa wanaostahili kuungwa mkono.


  CCM ina kila sababu ya kubakia kwenye ligi daraja la kwanza kisiasa nchini endapo itakuwa na visheni na misheni inayoeleweka na wote -viongozi kwa wafuasi; ikiogopa kugusa na kuwatumia viongozi wa 'dini' kama ebola inavyoogopeka hata na madaktari; ikijifunza kufanya kazi na watu inaowachukia au isiyowapenda sawasawa na inavyofanya kazi na wale inaowapenda;


  ikikubali kuwa mazuri pia yanapatikana nje ya chama na wanachama; ikikubali kuwa kila Mtanzania anaipenda nchi yake kama vile wanaCCM wanavyoipenda wao; itakapowatumia na kutumia ushauri wa wataalamu badala ya ushauri wa watoto wa mjini; haitakuwa kazi kwa wachezaji wapya kuingia kwenye timu hiyo kama vile wachezaji wanaotaka kutoka itakavyokuwa rahisi kwao kutoka; viongozi wataacha umimi, ubinafsi na uchama hata usipostahili; viongozi watakapokuwa kwa ajili ya wote na sio wachache; itakapotambua uaula wa mambo na kuyafanya kwa wakati; viongozi watakapotumia muda walionao kujenga badala ya kujibomoa au kuwabomoa wengine na itakapotambua akili ni nywele na kila mtu ana zake!


  Mzungu wa kula hafunzwi. Na mwana CCM ikijiganga huku ikijua au ikiwa haijui kuwa inaumwa na gonjwa la 'ndivyofunavyofikiri' kama vile yule mtu anayekwenda kunywa kikombe kwa babu -tofauti kubwa itaonekana kwa faida ya nchi hii na watu wake! Kwa hali yoyote ile Tanzania ya kesho itakuwa imara zaidi ikiwa na CCM yenye siha na afya kuliko CCM inayougua maradhi ya kila aina!


  Pepe: sammy.makilla@columnist.com

  CHANZO: Mwananchi
   
 2. d

  demokrasia Member

  #2
  Apr 8, 2011
  Joined: Apr 6, 2011
  Messages: 52
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  Exellent. You are inteligent man.Your views are ojective.
   
Loading...