Ccm haitovuko pigo la Tufani

Kakke

JF-Expert Member
Dec 4, 2010
1,883
1,482
IMG_5409.jpg


Na Enzi Talib Aboud

LICHA ya Wazanzibari kuvumilia mgogoro wa kisiasa unaozidisha ugumu wa maisha yao, bado wanaendelea kuwa watulivu huku wakijiuliza maswali mengi. Kubwa kuliko yote wanayojiuliza ni je watawala wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara wataitoa Zanzibar?

Hilo linafuatana na hoja kwamba inakuaje Dk. Ali Mohamed Shein, mwana kindakindaki wa Kizanzibari na msomi mahiri wa udaktari wa falsafa, akisomea vyuo vikuu vya Urusi na Uingereza, anakubali kupelekeshwa na wahafidhina na kuongoza Serikali ya Zanzibar iliyomgeuka yenye ombwe la utata wa Kikatiba na kisheria?

Ni dhahiri kwamba anajua muda wake wa Urais wa kipindi cha kwanza cha miaka mitano umekwisha. Anaelewa tosha kwamba kuendelea madarakani kwa kipindi cha pili cha miaka mitano si sahihi, hakuchaguliwa na wananchi katika uchaguzi uliofutwa.

Bila ya shaka kuendelea kwake Ikulu ni matokeo ya kuwekwa kwa mabavu na CCM, kwa kujiridhisha chenyewe kuwa madaraka ya nchi hayawezi kukabidhiwa Maalim Seif Shariff Hamad wa Chama cha Wananchi (CUF), kwa kuwa CCM Zanzibar walishasema “nchi haiwezi kutolewa kwa vikaratasi (kura).”

Lakini katika kitabu cha Mwalimu Nyerere “TUJISAHIHISHE” anapingana na watawala wa sasa wa CCM. Anabainisha kuwa “UKWELI” una tabia ya kulipiza kisasi kwa madhalimu wote wawe ndani ya CCM au ndani ya Serikali.

Hawawezi kuvuka na pigo la tufani, watasombwa kwa ghadhabu ya dhambi zao wanazofanya za kuipinga haki na kusimamisha batili dhidi ya wengine hasa viongozi wa upinzani wa vyama vya umoja wa Ukawa vinavyoongozwa na Maalim Seif kwa upande wa Zanzibar na Edward Lowassa kwa Tanzania Bara.

Kwa fikra finyu za CCM, wawili hawa wanaonekana wasio haki ya kutawala Zanzibar na Tanzania Bara. Maalim Seif ameporwa kwa makusudi ushindi wake na watawala wa CCM Zanzibar na Lowassa akahujumuiwa kwa staili ya “bao la mkono.”

Desturi ya haki ni kutoweza kuchanganyika na dhulma. Ndio sababu kwa kushtukizia bila ya hata watawala kufikiria kuwa yaweza kutokea Rais wa Jamhuri ya Muungano, Dk. John Magufuli akaamua kutoutii udhalimu wa CCM na kujiweka pembeni.

Baada ya kuapishwa, akathubutu kufanya mageuzi makubwa na kuvunja vipande vipande mfumo wa ufisadi uliojengeka kwa miaka kumi chini ya serikali ya Rais mstaafu Jakaya Kikwete.

Mageuzi anayosimamia yamemsuta pia Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana ambae hakuweza kuwaondoa viongozi mizigo CCM. Hata wale walohusika moja kwa moja na ufisadi wamebaki, wengine wakipewa jukumu zito kitaifa la kuandaa katiba mpya ya jamhuri.

Ujasiri wa CUF wa kuikataa Katiba hiyo umezaa muamko mkubwa wa hisia za kurudisha utaifa wa wananchi wa Zanzibar na katika ujio wa uchaguzi mkuu wa Oktoba 25, 2015 wananchi hao wameshikana na kutoa upinzani mzito kwa CCM.

Maalim Seif pamoja na kuwekewa vikwazo vingi na watawala wa CCM Zanzibar vya kutimiza dhamira yake ya kuongoza Zanzibar, ameshiriki uchaguzi kwa ujasiri zaidi na ustadi wa kupanga kampeni. Matokeo yake ni kupata ushindi wenye ushahidi wa kimahkama.

Amekuwa akipigania haki yake hiyo na kusababisha Rais Dk. Magufuli avunje ukimya walipokutana kwa mazungumzo nae kwa muktadha wa kutatua mgogoro uliotengenezwa kijasusi Zanzibar.

Kauli yake Dk. Magufuli imetafsiriwa kutokuwa tayari kuwaacha watawala wachache Zanzibar kuvuruga amani na utulivu kwa kuiteka nyara demokrasia.

Kitendo cha wananchi kupokonywa haki yao ya msingi ya kuchagua kiongozi wamtakae ni dhulma isiyovumilika kwa kiongozi yeyote aliye muadilifu.

Mgogoro wa kisiasa Zanzibar umetoa sura mbaya kwa Jumuiya ya Kimataifa na nchi za wahisani zinazoipa misaada Tanzania na nchi hizo zimeonesha nia ya kuzuia misaada hiyo. Marekani imeanza kuinyima Serikali msaada wa maendeleo ikiona demokrasia inaendelea kuminywa Zanzibar.

Ni kawaida pia kwa Marekani kuchukua hatua zaidi kama hizo na kuungwa mkono na mataifa mengine yanayofadhili nchi kama Tanzania hasa zile nchi za Muungano wa Ulaya ambazo pia zimeshaanza kuzungumzia hatua inazoweza kuichukulia Tanzania ikipuuza sharti lake la kuitaka Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) ikamilishe kazi ya kutangaza matokeo yaliyosalia ya uchaguzi wa Zanzibar.

Hapo panajitokeza swali ni kwa nini Rais Dk. Magufuli akawa hawezi kuwachukulia hatua vinara wanaotoa kauli zinazokuza mgogoro kwa kuwaweka roho juu wananchi wa Zanzibar.

Yumkin, inawezekana kwa sababu hana madaraka ndani ya chama kwa vile hajakabidhiwa Uenyekiti wa CCM ambao kikatiba anaendelea kuushikilia mtangulizi wake Dk. Jakaya Kikwete. Kikatiba, makabidhiano yatafanywa wakati wa mkutano mkuu mwaka 2017.

Kwa kasi yake ya utendaji, Dk. Magufuli asingeweza moja kwa moja kuingilia mgogoro wa Zanzibar bila ya kwanza kushauriana na Mwenyekiti Kikwete anayepaswa kumtaarifu na kumpa maelekezo Makamu Mwenyekiti Zanzibar ambae ni Dk. Shein kuhusu maamuzi ya chama, yawe ya kuacha madaraka au ya kuendelea kubaki Rais wa Zanzibar, lakini maagizo kama hayo bado hayajafanyika.

Inawezekana pia Rais anavuta muda kutathmini hali inavyoendelea Zanzibar na muingiliano wa mgogoro huo na mabadiliko yanayoendelea Tanzania Bara ya kujenga nchi, wakati kwa upande wa Zanzibar juhudi hizo zimekwama kutokana na kutokuwepo uongozi wenye ridhaa huku CUF ikiwa imeshavunja kambi ya ushirikiano katika serikali anayoongoza Dk. Shein.

Wazanzibari wamefanya maamuzi ya kuchagua Rais wanaemtaka, lakini varange na mizengwe ya CCM imesababisha ndoto zao kumpata Rais chaguo lao, zinakandamizwa.

Hali ya kisiasa Zanzibar imekuwa tete tangu Oktoba 28 baada ya Mwenyekiti wa ZEC kufuta uchaguzi wakati huo akiwa ametangaza matokeo ya majimbo 33, na kubakisha 21 ambayo 18 ni ya Pemba.

CUF wanashikilia kuwa walikuwa na ushindi wa zaidi ya asilimia 52 kwa kura zipatazo 200,700 dhidi ya 178,000 za CCM, matokeo yaliyotokana na fomu walizokuwa nazo mawakala wa vyama vyote vilivyoshiriki uchaguzi mkuu Zanzibar pamoja na waangalizi.

Asasi za wangalizi zilizokuwa zimetoa ripoti zao za awali za uangalizi wa uchaguzi wa Zanzibar, ni pamoja na Umoja wa Ulaya (EU), Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Madola (Commonwealth), Jumuiya ya Ushirikiano ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Matokeo hayo yalikuwa yameshabandikwa kwenye vituo baada ya kuthibitishwa na wasimamizi wa uchaguzi majimboni na mawakala wakuu wa wagombea urais wote.

Muandishi wetu Enzi Talib
 
CCM ni sikio la kufa, hawasikii lolote na hawajali. Ukweli kwao ndio uongo, na uongo ndio ukweli. Wako tayari wananchi wengine wote wafe wabaki wao peke yao.
 
Back
Top Bottom