CCM kwa sasa hivi inazungumzia miaka 2 ya utawala wa Awamu ya Sita ya Rais SSH. Je, sifa zinazomwagwa zinaakisi Ilani ya CCM 2020-2025. Nitanukuu machache yahusuyo uchumi ili kuonesha tofauti ya Sera ya Uchumi wakati wa Awamu ya Tano (Uchumi wa Viwanda) na Awamu ya Sita (Dmokrasia ya Uchumi)
Kwenye hiyo Ilani ya CCM kuhusu
Mapinduzi ya uchumi kwa maendeleo ya watu (Sura ya Pili).
12. Chama Cha Mapinduzi kinatambua umuhimu wa kujenga uchumi wa kitaifa ili kuhakikisha kwamba Watanzania ndio wanufaika wakuu wa uchumi na maliasili za nchi na ndiyo wenye kauli juu ya namna uchumi unavyoendeshwa. Kwa muktadha huo CCM itaelekeza Serikali kuendelea na juhudi za kuifanya Tanzania kuwa nchi inayojitegemea kiuchumi pamoja na kuimarisha mahusiano ya kiuchumi na nchi nyingine. Juhudi maalum zitaelekezwa kuhakikisha rasilimali za asili za nchi hii, hasa ardhi, madini, gesi asilia, mafuta, maji na misitu zinanufaisha wananchi na Taifa kikamilifu.
13. Katika miaka mitano ijayo, CCM itazisimamia Serikali zake ili ziendeleze juhudi za kuleta mageuzi ya kiuchumi kwa kuendelea kujenga Tanzania ya viwanda na uchumi fungamanishi, jumuishi na shindani unaotumia sayansi na teknolojia za kisasa na ambao unahimili utandawazi na unaoweza kutumia kikamilifu fursa zake kwa kuuza zaidi bidhaa za viwandani na bidhaa nyingine nje ya nchi. CCM inatambua fika kwamba ili kutimiza azma ya kujenga uchumi shindani wa viwanda na huduma, ni lazima kila Mtanzania afanye kazi kwa bidii, kujituma, na kutumia maarifa, hekima na ubunifu.
Najiuliza maswali kadhaa:
1) Ni kwa jinsi na kiwango gani "Demokrasia ya Uchumi" inakidhi malengo na matarajio yaliyomo kwenye Ilani ya Uchaguzi ya CCM, 2020-2025?
2) Sera ya Uchumi wa Viwanda inatekelezwaje kwenye "Demokrasia ya Uchumi" wakati mwekezaji ndiye huamua nini cha kuwekeza na wapi? Nanukuu kutoka Sura ya Pili ya Ilani ya Uchaguzi
4. ... Aidha, CCM inatambua kuwa serikali inazoziongoza zina jukumu la msingi la kuhakikisha kuwa walio wanyonge katika jamii wanapata fursa ya kipekee ya kustawisha maisha yao na kuondokana na unyonge wao ili
kupunguza tofauti za matabaka.
CCM, chonde chonde msitoke kwenye reli ya maendeleo kwa kujitegemea, 2025 haiko mbali. Wapiga kura watawahukumu kwenye sanduku la kurra.
Sikiliza tathmini ya miaka 2 ya Awamu ya Tano na Sita.
(Tathmini ya Uchumi wa Viwanda)
(Tathmini ya Demokrasia ya Uchumi)