Bilionea Asigwa
JF-Expert Member
- Sep 21, 2011
- 16,515
- 28,487
- Anasema Serikali ya awamu ya nne ilizungukwa na madalali na matapeli waliokuwa wamekamata mzunguko wa fedha.
- Asema madalali hawa walijiona miungu watu kwa sababu ya nguvu yao ya fedha na walikuwa hawaguswi.
- Asema Magufuli ajipange, maana madalali na matapeli hawa wawawezi kukubali kushindwa kirahisi.
- Asema alishauri mengi, lakini hayakutekelezwa
- Asema hatua za Magufuli zimerejesha heshima ya Serikali iliyopotea.
HATUA zinazochukuliwa na Rais John Magufuli tangu alipoingia madarakani za kurejesha nidhamu ya utumishi wa umma na kudhibiti mapato na matumizi ya Serikali, zimerejesha heshima ya Serikali na jamii ya Watanzania kwa ujumla. MTANZANIA Jumamosi limedokezwa.
Hayo yamesemwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) mstaafu, Ludovick Utouh, katika mahojiano baina yake na gazeti hili yaliyofanyikia ofisini kwake Dar es Salaam, mapema wiki hii.
Mahojiano hayo yalikuwa mahususi kwa ajili ya Utouh kutoa tathmini ya mwenendo wa utendaji kazi wa Serikali ya awamu ya tano ikilinganishwa na ule wa awamu ya nne.
Akitoa tathmini yake, Utouh alisema Serikali ya awamu ya tano imejitenga kiutendaji na ya awamu ya nne kwa kusimamia uwajibikaji wa watumishi wa umma na nidhamu ya mapato na matumizi ya fedha za Serikali hivyo kurejesha heshima iliyokuwa imepotea.
Utouh alisema anaridhishwa na mwenendo wa utendaji kazi wa Serikali ya Rais Magufuli na kwamba baadhi ya mambo anayoyafanya sasa yeye mwenyewe alipata kushauri yafanyike alipokuwa bado ofisini lakini hayakuzingatiwa.
“Haya mambo yanayofanywa sasa na Rais Magufuli na Serikali yake nilipata kuishauri Serikali ya awamu ya nne kuyafanya lakini kazi yangu ilikuwa ni ushauri tu, watekelezaji wengine. Unaposhauri ushauri unaweza kupokelewa kwa asilimia 100 au usipokelewe kabisa,” alisema Utouh.
Akizungumzia tathmini ya utendaji kazi wa Serikali ya awamu ya nne, alisema ilizungukwa na kundi kubwa la madalali aliowaita kwa lugha ya kimombo ‘middle man.’
Alisema madalali hao waliukamata mzunguko wa fedha na kusababisha kukua kwa tabaka la walionacho na wasionacho katika jamii.
“Unajua ulifika wakati madalali hawa wakajiona miungu watu kwa sababu ya nguvu yao ya fedha, walikuwa hawaguswi, jamii nayo ikawatukuza na kuwashabikia na kuwaona ni bora kuliko waadilifu.
“Kwa hali hii naona hata Rais Magufuli ana kazi ngumu ya kubadilisha dhana ya kushabikia mafisadi ambayo ilikuwa imepandwa na kumea katika fikra za wananchi,” alisema Utouh.
CAG huyo mstaafu alisema kundi hilo la madalali lilitegemea mtaji wa maneno lililoutumia kuwaunganisha baadhi ya wafanyabiashara na viongozi wa Serikali ili kutekeleza mipango ‘deal’ mbalimbali ikiwamo ya kifisadi.
Alisema kundi hilo la madalali lilionekana kuwa na nguvu na jeuri ya fedha kuliko waliyonayo wavuja jasho na watumishi wa umma.
Akizungumzia athari za kuwepo kwa kundi hilo katika Serikali ya awamu ya nne, alisema nguvu na jeuri hiyo ya fedha ya watu hao iliwavunja moyo watumishi wengi wa umma ambao nao walilazimika kuanza kushiriki vitendo vya rushwa na ufisadi ukiwamo wizi wa fedha za Serikali.
“Serikali ya Rais Kikwete (Rais mstaafu Jakaya Kikwete), imefanya mambo mengi mazuri ya kimaendeleo na ujenzi wa uchumi, lakini ilikabiliwa na changamoto ya wimbi la madalali, watu hawa waliishi kwa mitaji ya midomo yao kwa kuunganisha watu mbalimbali wakiwamo wafanyabiashara na viongozi wa Serikali kwa minajili ya kufanikisha ‘deal’ zao mbalimbali,” alisema Utouh.
Alisisitiza kuwa kama Serikali ya Kikwete ingeendelea kuwepo madarakani kwa kipindi kingine kifupi baada ya kumaliza muhula wake wa uongozi, watumishi wa umma wachache waliobaki na waadilifu serikalini nao wangelazimika kujiingiza kwenye udalali ili kujipatia fedha.
Alisema kadiri kundi la madalali lilivyokuwa likiongezeka ndivyo lilivyozidi kusababisha madhara zaidi kwa Serikali ya Kikwete kutokana na kujihusisha kwake na utapeli wa hali ya juu miongoni mwa jamii.
“Kundi la madalali na matapeli lilionekana kupeta zaidi kimaisha huku watumishi waadilifu wakiumia na ugumu wa maisha.
“Ufuatiliaji wa Serikali ulikuwa ni mdogo hivyo watu wengi wakageuka madalali na jambo la kusikitisha zaidi kwa upande wa watumishi wa umma ni kwamba ukiwa mtumishi wa umma mwadilifu wenzako wanakuona nuksi, wanakucheka na kukuambia unachelewa maisha, yote haya ni sehemu tu ya mambo ambayo yamelifikisha taifa hapa tulipo ambapo Rais Magufuli anahangaika na utumbuaji.
“Hawa madalali wamechangia sehemu kubwa ya ukwepaji kodi bandarini kwa sababu walikuwa sehemu ya katikati ya kuwakutanisha wafanyabiashara na wakubwa serikalini.
“Madalali wamechangia kwa kiwango kikubwa kuongezeka kwa rushwa serikalini, unadhani hata hayo makontena yaliyopitishwa bila kulipiwa kodi wakubwa hawakufahamu? Nahisi hata haya mambo ya dawa za kulevya yanayoichafua nchi wapo wakubwa ambao waliunganishwa na wafanyabiashara ili wasaidie upitishaji wa dawa hizo hapa nchini,” alisema Utouh.
Hata hivyo, alionya kuwa ingawa Rais Magufuli anaonekana kupata mafanikio katika kupambana na mtandao wa madalali waliokuwa wamejichomeka karibu na Serikali huku wakiwa na jeuri ya fedha, bado ana kazi ngumu mbele ya kuhakikisha anauzika.
Alisema madalali hao hawawezi kukubali kushindwa kirahisi kwa sababu mafanikio yake yaliyotokana na kufanikisha tenda za Serikali kwa njia za ujanja ujanja hivyo wanaweza kujipanga kuhujumu jitihada zake za kurejesha misingi ya uadilifu na uwajibikaji serikalini.
Aidha, aliwataka Watanzania kuunga mkono jitihada za Rais Magufuli kuangamiza mtandao wa madalali licha ya nguvu kubwa ya kisheria na kimamlaka aliyonayo rais.
MISHAHARA HEWA
Utouh alizungumzia pia tatizo la mishahara hewa kwa kueleza kuwa si jambo geni serikalini kwani hata alipokuwa na dhamana ya kuongoza Ofisi ya CAG, alilikuta.
“Mishahara hewa si jambo geni, nimelikuta na nikalipigia kelele sana na Serikali ya awamu ya nne ikajitahidi kwa uwezo wake kupunguza tatizo hilo kwani hali ilikuwa inatisha.
“Binafsi kwa sasa napenda kupongeza juhudi za Rais Magufuli za kubaini mapema tatizo hili ingawa napenda pia kuwaasa Watanzania kwamba tusikae na kushabikia tu kwamba Serikali imeokoa mabilioni ya mishahara iliyokuwa inalipwa kwa wafanyakazi hewa,” alisema Utouh.
Akizungumzia uzoefu wake katika tatizo hilo, alisema Rais Magufuli anapaswa kubaini chanzo cha kuwepo kwa watumishi hewa wanaolipwa malipo wasiyostahili tofauti na hapo jitihada zake za sasa zinaweza kuwa za bure.
“Naamini kabisa kwamba pamoja na juhudi kama hizi za kubaini watumishi hewa takribani 7,000 zitaendelea, zitafanikiwa kidogo kwa kiasi tu, lakini ndani ya miezi sita ijayo mishahara hewa inaweza kuibuka mara dufu ya ilivyo sasa,” alisema Utouh.
ALICHOBAINI KWENYE MISHAHARA HEWA
Utouh alisema jambo alilobaini kwenye tatizo la ulipaji mishahara hewa wakati akiwa bado mtumishi wa Serikali ni kushuka kwa uadilifu pamoja na mishahara duni miongoni mwa watumishi wa umma.
Alisema hali hiyo iliwashawishi watumishi wengi kujiingiza katika mitandao ovu ya wizi wa fedha za Serikali.
“Matokeo ya kushuka kwa uadilifu na mishahara midogo kwa watumishi wa umma kulichangia kwa kiasi kikubwa kujengwa kwa mtandao ovu wa kuiba fedha za Serikali. Mtandao huu ni mkubwa na unatisha kwa sababu una mikakati ya aina mbalimbali ya kuiba fedha za Serikali,” alisema Utouh.
Alisema alipokuwa mtendaji mkuu katika Ofisi ya CAG, aliishauri Serikali itafute chanzo cha kuwapo kwa malipo ya mishahara kwa watumishi hewa lakini ushauri wake haukufanyiwa kazi na yeye hakuwa na la kufanya kwa sababu kazi yake ilikuwa ni kushauri tu huku kazi ya utekelezaji ikiwa chini ya wengine.
“Sikiliza nikwambie, unapotoa ushauri unaweza kupokelewa au kutopokelewa. Nakumbuka aliyekuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Hawa Ghasia, alinifuata na kuniambia kuwa Serikali imesikia kilio changu kuhusu mishahara hewa hivyo imekuja na mwarobaini wa jambo hilo kwa kuanzisha mfumo maalumu wa kuingiza taarifa kwa watumishi kupitia njia ya kielektroniki.
“Binafsi nilimwambia kwamba mfumo huo ni mzuri lakini kwa hali ilivyo serikalini hautaweza kufanya chochote,” alisema Utouh.
Source: CAG AUTOUH: Serikali ya JK ilijaa madalali