Cag: Mawaziri wapya wakicheza watang'oka

mwitaz

JF-Expert Member
Feb 19, 2012
315
93
CAG: Mawaziri wapya
wakicheza watang'oka

ASEMA ATAWAKAGUA NA
KUTOA RIPOTI KATIKA
VIPINDI VITATU, VIGOGO
WENGINE 'WAPUMULIA
MASHINE'
Boniface Meena MDHIBITI na Mkaguzi Mkuu
wa Hesabu za Serikali
(CAG), Ludovick Utouh
amewaonya mawaziri
wapya na watendaji
serikalini kwamba ripoti zake hivi sasa zina nguvu
za kusimamia uwajibikaji
hivyo, wanapaswa
kusimamia vyema wizara
zao kuzuia ubadhirifu wa
fedha za umma. Kauli hiyo ya Utouh ni ya
kwanza tangu ripoti yake
ya mwaka huu kuwang’oa
mawaziri sita kati ya
wanane ambao wizara zao
zilionekana kugubikwa na ufisadi wa fedha za umma. Akizungumza jana, Utouh
alisema mawaziri
wanapaswa kufahamu
kwamba kuanzia sasa hadi
mwaka 2015, zitatoka
ripoti nyingine tatu, hivyo ni vyema wakachukua
tahadhari wakiwa ndiyo
wasimamizi wakuu wa
shughuli za wizara. Alisema kilichotokea
bungeni na hadi mawaziri
kuwajibishwa,
kimethibitisha kuwa sasa
kutakuwa na uwajibikaji
mkubwa utakaosababishwa na
ripoti zake kama watendaji
wasipofuata taratibu za
Serikali. “Mawaziri ni wasimamizi
wa wizara hata kama ni
wanasiasa, wao ndiyo
wanaowajibika
kuhakikisha mambo
yanakwenda vizuri wizarani hivyo ni muhimu
wakafanya hivyo,” alisema
Utouh. Alisema kilichotokea ni
sehemu ya uwajibikaji na
kusema hatua
iliyochukuliwa na Rais
imetokana na ripoti ya ofisi
yake kuonyesha udhaifu katika usimamizi
uliofanywa na watangulizi
wao hivyo kuwataka
kuwa makini. Utouh alisema kwa kuwa
ofisi yake inapaswa
kuandaa ripoti tatu hadi
kufikia mwisho wa Serikali
ya Awamu ya Nne ya Rais
Jakaya Kikwete watendaji hao waandamizi wa Serikali
wanakabiliwa na
changamoto kubwa ya
kutimiza wajibu wao. Alisema angalizo hilo
haliwahusu mawaziri tu,
bali hata watendaji
walioko chini yao. CAG alisema hivi sasa ofisi
yake inaandaa ripoti
nyingine mahsusi kuhusu
vitendo vya jinai, rushwa
na ubadhirifu
vilivyotokana na kile kilichowang’oa viongozi
hao tayari kwa ajili ya
kuiwasilisha kwa Taasisi ya
Kupambana na Kuzuia
Rushwa (Takukuru). “Barua ambayo Takukuru
walituandikia kuhusu wale
ambao wamezungumzwa
kwenye ripoti nimeiona na
tunaishughulikia lakini
nikwambie tu kwamba hata kama
wasingetuandikia
tungewapelekea kwa
kuwa tumekuwa
tunafanya kazi nao kwa
karibu,” alisema. Ripoti hiyo ya CAG ndiyo
iliyamlazimu Rais Kikwete
kupangua Baraza lake la
Mawaziri na kuwang'oa
sita, Dk Cyril Chami
(Viwanda na Biashara), Omary Nundu (Uchukuzi),
Ezekiel Maige (Maliasili na
Utalii), Dk Hadji Mponda
(Afya na Ustawi wa Jamii),
Mustafa Mkulo (Fedha) na
William Ngeleja (Nishati na Madini). Nafasi za mawaziri hao sasa
zimejazwa na Mbunge wa
Handeni, Dk Abdallah
Kigoda (Viwanda na
Biashara), Mbunge wa
Kalenga, Dk William Mgimwa (Fedha) na
Mbunge wa Kuteuliwa
Profesa Sospeter Muhongo
(Nishati na Madini), Dk
Harrison Mwakyembe
(Uchukuzi), Dk Hussein Mwinyi (Afya na Ustawi wa
Jamii) na Balozi Hamis
Kagasheki (Maliasili na
Utalii). Kilichowang’oa
Baadhi ya tuhuma
zilizokuwa zimeibuliwa na
CAG kwenye Wizara ya
Fedha iliyokuwa chini ya
Mkulo ni kuvunja Bodi ya Shirika Hodhi la Mashirika
ya Umma (CHC), ili kuficha
tuhuma zake ikiwemo
uuzaji wa Kiwanja Na.10
kwa Kampuni ya Mohamed
Enterprises (MeTL). Ukaguzi wa CAG ulibaini
kuwa Ofisi ya Msajili wa
Hazina na Wizara ya Fedha,
zilihusika moja kwa moja
katika uuzwaji wa kiwanja
hicho kilichopo kando ya Barabara ya Nyerere bila
kuishirikisha bodi ya CHC. Aidha, CAG alibaini kuwapo
kwa utata katika hati ya
madai ya Sh2.4 bilioni
kutoka katika kampuni ya
DRTC zinazodaiwa kuwa ni
gharama za ulinzi na tozo la matumizi ya barabara ya
kuingilia kwenye Kiwanja
Na.192 kando ya Barabara
ya Nyerere. Upungufu pia ulionekana
kwenye uuzwaji wa Jengo
la Kampuni ya Tanzania
Motors (TMC) lililopo
Kiwanja Namba 24
kilichopo katika eneo la Viwanda la Chang’ombe
kwa Kampuni ya Maungu
Seed. Kwa upande wa Ngeleja,
alikabiliwa na kashfa
baada ya CAG kubaini
kuwa Shirika la Umeme
Tanzania (Tanesco), kwa
mwaka mmoja wa fedha linafanya ununuzi wenye
thamani ya Sh300 bilioni
hadi Sh600bilioni. Kwa mwaka wa fedha
2009/2010, Tanesco
lilitumia Sh1.8 bilioni
ukilinganisha na Sh65
milioni zilizokuwa
zimepangwa katika bajeti ya ukarabati wa gati
mojawapo katika Kituo
cha Bwawa la Mtera na
kuingia mikataba isiyo na
tija kwa taifa. Kwa Maige, ripoti ya CAG
ilieleza kuwa ofisi yake
ilipoteza Sh874,853,564
baada ya kufanya uamuzi
wa upendeleo wa kutoa
kiwango cha chini cha mrabaha kwa mauzo ya
misitu. Katika kipindi cha ukaguzi
wa hesabu za Shirika la
Hifadhi ya Taifa Tanzania
(Tanapa), ilibainika kuwa
liliingia katika mkataba na
kampuni ya CATS Tanzania Ltd unaohusiana na
matengenezo ya kawaida,
ufungaji wa vifaa vya
mawasiliano na vifaa
vingine katika mkataba wa
jumla ya Dola za Marekani milioni moja (wastani wa
Sh1.5 bilioni). Pia anatuhumiwa kuweka
mazingira ya rushwa
katika ugawaji wa vitalu
vya uwindaji, ambao
unadaiwa kutawaliwa na
dosari nyingi ikiwa ni pamoja na kutangaza
majina ya waliopata vitalu
bila kuonyesha jinsi
walivyopewa. Pia, Kamati ya Kudumu ya
Bunge ya Ardhi, Maliasili na
Mazingira ilieleza kuwa
kampuni 16 zilizopewa
vitalu hivyo hazikuomba
na kwamba vitalu hivyo vilikuwa vya daraja la
kwanza na la pili. Mbali na tuhuma hizo, Maige
hivi karibuni alidaiwa
kununua nyumba kwa
Dola za Marekani 700,000
iliyopo Mbezi Beach, Dar es
Salaam, tuhuma ambazo alizipinga na kusema kuwa
nyumba hiyo ameinunua
kwa Dola 410,000, sawa na
zaidi ya Sh600 milioni). Dk Mponda alikabiliwa na
kashfa ya Bohari ya Dawa
(MSD) ambako ukaguzi
maalumu ulibaini kuwapo
tofauti ya Sh658.9 milioni
ikiwa ni pungufu ya kiasi ambacho kilipokewa na
kuripotiwa na wizara hiyo
kwenda bohari, huku
ushahidi wa kupokewa
kwake ukiwa
haujatolewa. Pia, ukaguzi huo maalumu
ulibaini kuwapo kiasi cha
Sh4.5 bilioni zilizotoka
Hazina kwenda wizara hiyo
kununulia dawa na vifaa
vya hospitali, lakini kiasi cha Sh4.344 bilioni tu
ndicho kilichopokewa na
MSD. Nundu alikabiliwa na
kashfa ya Shirika la Ndege
Tanzania (ATCL) na mradi
wa upanuzi wa Bandari ya
Dar es Salaam huku
akituhumiwa kuipigia kifua Kampuni ya Chinese
Merchant ipewe zabuni ya
upanuzi huo wa bandari. Lakini, Nundu alimtuhumu
aliyekuwa naibu wake,
Athumani Mfutakamba
ambaye naye ameng'olewa
kwamba alikuwa
akishinikiza Kampuni ya China Communication
Construction Company
(CCCC), ipewe kazi ya
kujenga gati namba 13 na
14 katika Bandari ya Dar es
Salaam kwa kuwa ilimgharamia safari kadhaa
kwenda nje. Hata hivyo, Mfutakamba
alipoulizwa kuhusu safari
zake hizo za nje
kugharamiwa na CCCC na
baadaye kuandika ripoti
akishinikiza ipewe kazi ya kujenga gati hizo, alikiri
kusafirishwa lakini
akasema alifuata taratibu
zote za kiserikali. Dk Chami alituhumiwa
kumlinda Mkurugenzi
Mkuu wa Shirika la
Viwango Tanzania (TBS),
Charles Ekelege kutokana
na tuhuma za kuwepo ofisi hewa za ukaguzi wa TBS
zilizopo nje ya nchi. Ekelege anadaiwa
kusimamia ofisi hewa za
ukaguzi wa magari huko
Singapore na Hong Kong
na kuitia Serikali hasara ya
karibu Sh30bilioni.

Source: Mwananchi
 
Wasijetuwakam-mwakyembe!!!!!!!!Maana hao walioenguliwa kwa lazima,hasira zimewajaa!!!!
 
Back
Top Bottom