CAG aagizwa kuwasilisha ripoti ya Escrow

CAG aagizwa kuwasilisha ripoti ya Escrow

Mwanamwana

Platinum Member
Joined
Aug 1, 2011
Posts
9,604
Reaction score
22,715
Dar es Salaam. Sakata la fedha zilizochotwa kwenye Akaunti ya Tegeta Escrow katika Benki Kuu (BoT), limechukua sura mpya baada ya Kamati ya Bunge ya Fedha za Mashirika ya Umma (PAC) kumwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali(CAG) kuwasilisha taarifa ya uchunguzi wa akaunti hiyo mbele ya PAC ifikapo Oktoba 31.

Habari za kiuchunguzi zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa PAC imemwandikia barua CAG Oktoba 24 mwaka huu iliyosainiwa na mwenyekiti wake, ikilenga kufanikisha kuwasilisha ripoti yake katika Mkutano wa 17 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, unaotarajiwa kuanza Novemba 4 mjini Dodoma, ili kuliokoa taifa lisiingie kwenye mgogoro wa kibajeti.

Soma pia: Uzi maalum wenye matukio yote yaliyojiri kwenye sakata la ufisadi wa ESCROW

"Kamati imeomba CAG awasilishe taarifa ya Escrow ifikapo Ijumaa tarehe 31 Oktoba ili iweze kuifanyia kazi kwa mujibu wa taratibu za kibunge. Hii itasaidia wafadhili kuondoa zuio la misaada," kilieleza chanzo chetu kikinukuu maelezo ya PAC kwenda kwa CAG.

"Kamati imeomba CAG awasilishe taarifa ya Escrow ifikapo Ijumaa tarehe 31 Oktoba ili iweze kuifanyia kazi kwa mujibu wa taratibu za kibunge. Hii itasaidia wafadhili kuondoa zuio la misaada," kilieleza chanzo chetu kikinukuu maelezo ya PAC kwenda kwa CAG.

Mwenyekiti wa PAC, Zitto Kabwe ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma Kaskazini alipoulizwa kuhusu kuwapo kwa hatua hiyo, alikiri kuandika barua hiyo na kusisitiza kuwa ukaguzi huo wa akaunti ya Escrow utaiwezesha kamati yake kuwa na taarifa yenye uhakika zaidi na isiyo na shaka yoyote.

Hata hivyo, habari nyingine za uhakika zinaeleza kuwa suala la akaunti ya Escrow, linazidi kuitikisa Serikali ambayo imelazimika kuanza kukopa katika soko la ndani kutokana na wafadhili kugomea misaada ya kibajeti. Hatua hiyo ya Serikali kuanza kukopa katika soko la ndani inatajwa kusababisha uchumi wa taifa kusinyaa kutokana na ukweli kwamba sasa inashindana kukopa na sekta binafsi hivyo kuongeza riba.

Uchunguzi umebainisha kuwa Wizara ya Fedha na Benki Kuu imeiambia PAC kwamba hatua ya wafadhili kuzuia misaada ya kibajeti inaathiri utekelezaji wa bajeti.

Sakata la akaunti ya Escrow kwa mara ya kwanza liliibuliwa bungeni na Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) baada ya taarifa hizo kuandikwa na vyombo vya habari ambapo Serikali kupitia Waziri Mkuu Mizengo Pinda iliagiza CAG na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa kuichunguza kisha ripoti kuwasilishwa bungeni.

Hivi karibuni mwenyekiti wa PAC alikaririwa akieleza kuwa taarifa alizopewa na ofisi ya CAG ni kwamba hadi sasa ni mhusika mmoja pekee ambaye hajahojiwa juu ya mabilioni ya fedha yaliyochotwa kwenye akaunti ya Escrow. Alisema kwa sasa kazi inayopaswa kufanywa na CAG ni kumhoji mmoja wa wahusika ambaye ni mkurugenzi wa Piper Link atakayefuatwa nchini Oman ili kukamilisha ripoti yake.

"Suala hili lina masilahi kwa taifa, nasi PAC hatutoficha taarifa hata chembe na kila hatua itakuwa ikishuhudiwa na waandishi wa habari," alinukuliwa Zitto na kuongeza kuwa PAC kwa niaba ya Bunge ndiyo iliyoomba uchunguzi wa suala hilo.

Sakata la Akaunti ya Escrow liliibuka kutokana na kile kinachoelezwa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (Tanesco) kulalamika kuwa malipo ya kununua umeme (capacity charge) wanayolipa kwa IPTL ni makubwa.

Hata hivyo, katika taarifa yake hivi karibuni, ofisi ya CAG ilisema: "Ukaguzi wa Akaunti ya Tegeta Escrow uliombwa na Katibu wa Bunge na Katibu Mkuu Wizara ya Nishati na Madini na unalenga kufanya uchunguzi wa kina utakaotoa taarifa kamili yenye kuonyesha hali halisi kuhusu akaunti maalumu ya Tegeta Escrow .

Taarifa zinaeleza kuwa IPTL ilikuwa ikimilikiwa kwa ubia na Kampuni ya VIP Engineering and Management iliyokuwa na asilimia 30 za hisa na Mechmar ya Malaysia iliyokuwa na asilimia 70.

Inadaiwa kuwa, Piper Link Investments Ltd ilinunua hisa asilimia 70 za Mechmar Septemba 2013 na majuma matatu baadaye waliziuza kwa PAP kwa Dola300,000 za Marekani sawa na Sh500 milioni.

Asilimia 30 za hisa zilizosalia ambazo zilikuwa zikimilikiwa na VIP, zilinunuliwa pia na PAP kwa Dola75 milioni.

Chanzo: Mwananchi
 
Back
Top Bottom