Buzwagi, Richmond kusuka ama kunyoa

BAK

JF-Expert Member
Feb 11, 2007
124,789
288,029
Buzwagi, Richmond kusuka ama kunyoa
Mwandishi Wetu Novemba 21, 2007
Raia Mwema

KUUNDWA kwa kamati teule ya Bunge kuchunguza sakata la zabuni ya mradi wa umeme wa dharura iliyotolewa kwa kampuni ya Richmond Development Corporation na kugubikwa na utata tokea mwanzo hadi sasa, sambamba na kuundwa kwa kamati ya kuchunguza mikataba ya madini kwa wakati mmoja, kumewachanganya na kuwatisha baadhi ya wahusika, Raia Mwema limebaini.

Habari za uhakika zinasema kwamba baada ya kufanikiwa kuzuia kwa nguvu zote kuendelea kwa mjadala na uchunguzi wa masuala hayo, wahusika wakuu wamechanganywa na hatua hiyo ya Bunge iliyoungwa mkono na wabunge wa Chama cha Mapinduzi (CCM) na wa upinzani, na hatua ya Rais Jakaya Kikwete kuunda kamati ya kuchunguza mikataba ya madini.

Pamoja na kuwapo wasiwasi kwamba huenda kamati hizo mbili zilizoundwa katika kipindi ambacho mjadala kuhusiana na sekta za nishati na madini umepamba moto dhidi ya Serikali kuhusiana na masuala hayo, wafuatiliaji wa mambo wanasema sasa watawala wamedhamiria masuala hayo mawili yafikishwe mwishoni, kwa matokeo mabaya au mazuri.

Mradi wa umeme wa dharura uliokabidhiwa kwa Richmond umeigharimu Serikali Sh. bilioni 172.9 ambazo kwa viwango vyovyote ni kiasi kikubwa cha fedha na si busara kuunyamazia.

Ofisa mmoja mwandamizi wa Serikali ameliambia Raia Mwema ya kuwa, uundwaji wa kamati hizo kwa pamoja ni salamu kwa wahusika, kuhusiana na msimamo wa Rais Kikwete katika kuwaridhisha wapiga kura wake, ambao ni zaidi ya asilimia 80, wengi wakitoka katika kundi kubwa la vijana waelewa wa mambo na ambao sasa wanahoji sana kashfa hizo.

"Baada ya Mkutano Mkuu wa CCM uliofanyika Kizota, Dodoma, Rais Kikwete alikua tayari amekwisha kupima wananchi wanataka nini. Alitumia vyanzo vyake kutoka miongoni mwa wajumbe wa Mkutano Mkuu kutoka mikoa yote na kupata picha halisi ya hisia za wananchi kuhusiana na hali ya kisiasa nchini na ndipo alipobariki kuundwa kwa kamati teule ya Bunge kuhusu Richmond na yeye kuunda ya madini," alisema mtoa habari huyo.

Anasema mbali na Rais Kikwete kuonyesha sura yake halisi katika kukabiliana na kero za wananchi, habari zinasema kwamba hata wabunge wa CCM waliwasilisha hisia za wapiga kura wao ambao katika siku za hivi karibuni walianza kuonyesha kupoteza imani na viongozi wao, na hata kufikia hatua ya kuwazomea baadhi yao katika mikutano ya hadhara.

"Itakumbukwa kwamba CCM ilikuwa na msimamo wa kutetea kwa nguvu zote suala la umeme wa dharura tokea lizue utata wakati wa matatizo ya umeme, hata pale wanasiasa wa upinzani na waandishi wa habari walipoibua suala hilo walizimwa na kubezwa, lakini ghafla hali imebadilika," anasema.

Hata hivyo, mchambuzi na mfuatiliaji wa mawimbi ya siasa nchini anasema kamati teule imeundwa kwa shinikizo la wabunge wa CCM ambao wameona dalili za kuweza kupoteza nafasi zao kwa "kushindana na upepo" kutokana na wananchi kukubaliana zaidi na hoja zinazotolewa na wapinzani.

Suala la mradi wa umeme wa dharura uliokabidhiwa Richmond kabla ya kuchukuliwa na Dowans Holdings S.A ya Falme za Kiarabu (UAE) limekua likiingizwa bungeni na wabunge wa upinzani, lakini wamekua wakizimwa na Serikali na hasa kutoka kwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, huku wabunge wa CCM wakishangilia na kuwakejeli wenzao.

Suala la mradi wa Richmond liligubikwa na hisia za kuhusika kwa baadhi ya viongozi wa Serikali, lakini mara kadhaa limekanushwa waziwazi, hali ambayo inaipa kamati hiyo kazi kubwa ya ama kuthibitisha ama kukanusha kuhusu kuhusika kwa viongozi.

Waziri Karamagi aliwahi kunukuliwa akisema kwamba hakuna kiongozi wala familia ya kiongozi inayohusika na sakata hilo ambalo wananchi wanaliona kuwa linawahusisha viongozi serikalini.Baada ya joto kupanda, hatimaye, Bunge lilikubaliana na mapendekezo ya Kamati ya Uwekezaji na Biashara iliyopendekeza kuundwa kwa kamati hiyo ili kuchunguza mradi huo; hata baada ya Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) kuwa imeusafisha katika uchunguzi wake.

Miezi michache baada ya TAKUKURU kuisafisha Richmond, Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Manunuzi (PPRA) ilitoa taarifa ikionyesha kuwapo kwa ukiukwaji mkubwa wa taratibu na sheria ya ununuzi ulioelezwa ulitokana na "shinikizo la kisiasa". Ripoti hiyo haikueleza shinikizo hilo lilitoka kwa kiongozi yupi.

Kuundwa kwa Kamati hiyo kulitokana na shinikizo la Wabunge ambao walilitaka Bunge kuunda chombo cha namna hiyo kitakachokuwa na uwezo wa kisheria wa kuupata mkataba wa kampuni ya Richmond na kuchunguza mchakato mzima uliofanywa hadi kufikia kuteuliwa kwake.

Walioteuliwa kuunda kamati hiyo ni Dk. Harrison Mwakyembe (Kyela-CCM) ambaye wenzake wememteua kuwa Mwenyekiti, na Stella Manyanya (Viti Maalum -CCM) ambaye ameteuliwa kuwa Makamu Mwenyekiti. Stela Manyanya ni mhandisi kitaaluma sawa na mjumbe mwingine Mohamed Mnyaa (Mkanyageni- CUF). Wajumbe wengine ni Lucas Selelii (Nzega-CCM) na Hubert Mntangi (Muheza- CCM).

Kamati hiyo iliyoundwa kwa mujibu wa Kanuni za Bunge kifungu cha 104 (3) na 105 inatakiwa kuchunguza na kubainisha Richmond Development Corporation ni kina nani, na ni kampuni ya shughuli zipi na hivyo kupima uwezo wake kupatiwa zabuni ya kuleta nchini na kujenga mtambo wa umeme wa gesi wa megawati 100.

Kuutathmini mchakato mzima wa jinsi zabuni waliyoshinda Richmond ilivyoshughulikiwa kuanzia Kamati ya Zabuni hadi mwisho ili kujiridhisha kuwa sheria, taratibu, miiko na maadili ya zabuni yanayotawala zabuni za aina hiyo vilifuatwa au vipi.Kuutathmini Mkataba baina ya Richmond Development Corporation na TANESCO ili kujiridhisha kuhusu uhalali wa masharti ya Mkataba huo ukizingatia gharama na masharti mengine ukilinganisha na masharti yaliyomo katika mikataba ya aina hiyo iliyofikiwa na TANESCO/Serikali.

Kubainisha huduma na misaada mbalimbali waliyopewa Richmond kama vile kufunguliwa Letter of Credit na kupima uhalali wake.

Kuziangalia na kuzitolea maoni taarifa za TAKUKURU, PPRA na taarifa zozote nyingine zilizoangalia utaratibu wa zabuni ya Richmond. Kuangalia mambo mengine yoyote yenye uhusiano na mchakato mzima wa Richmond ili kutoa mapendekezo ya kuboresha taratibu za zabuni kwa siku zijazo, kwa maslahi ya Taifa letu.

Akiwasilisha taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Biashara kuhusu utekelezaji wa shughuli za Kamati kwa mwaka 2006, Mwenyekiti wa Kamati hiyo,William Shellukindo (Bumbuli- CCM), alisema baada ya kufuatilia taarifa za Serikali na za Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Kamati haikuridhishwa na utendaji kazi wa Kampuni ya Richmond Development Corporation ya Marekani na mrithi wake Dowans Holdings S.A kwa kushindwa kukamilisha mradi wa umeme wa dharura katika muda muafaka.

Alisema utendaji kazi usioridhisha wa Richmond ni ushahidi bayana uliojitokeza polepole wa kampuni hiyo kutokuwa na uwezo wa kutosha kifedha na kukosa kabisa uzoefu katika miradi ya umeme, umezua maswali mengi miongoni mwa wananchi kuhusu umakini uliotumika kuiteua kutekeleza mradi nyeti kitaifa wa aina hiyo na wenye gharama kubwa ( Sh. Bilioni 172.9).

Wakati wa Mkutano wa Bunge la Bajeti, Mbunge wa Karatu kupitia CHADEMA, Dk. Wilbroad Slaa, alihoji kuhusu matokeo ya uchunguzi wa TAKUKURU kuhusu Richmond wakati alipochangia bajeti ya Ofisi ya Rais, akielekeza swali lake kwa Waziri wa Nchi anayeshughulikia Utawala Bora, Philip Marmo, huku akitaka taarifa ya uchunguzi iwasilishwe bungeni.

"Je, kama taarifa hizo ni za siri, ni kweli kwamba PCB inaweza ikachapisha kwenye magazeti, ikaacha kuwaamini Wabunge, ikaamini zaidi vyombo vya habari kwa sababu naona hapa sasa kuna tatizo kwamba PCB inaweza ikakwepa kutoa taarifa yake kwa vyombo vinavyosimamia Serikali, lakini ikaitoa taarifa ile kwa magazeti na Bunge halitakuwa tena na namna ya kuhoji?" alihoji Dk Slaa.

Marmo alijibu kwa kusema Takukuru muda wote inashughulikia masuala ya rushwa na kwamba rushwa ni vitendo vya jinai ambavyo mkondo wa matendo ya jinai hatimaye hufika katika hatua ya aidha mashtaka au uchunguzi kufungwa na kuelekea Mahakamani na hata siku moja sio Bungeni.

"Taarifa za PCB kwa asilimia mia moja zinahusiana na masuala au matendo ya jinai na mkondo wa matendo ya jinai hata siku moja haiwezi kuwa Bungeni isipokuwa Mahakamani. Iwapo Mbunge au raia yeyote ana ushahidi ambao anafikiri utaisaidia TAKUKURU au TAKUKURU haikufuatilia kwa makini, basi, raia hazuiwi hata kufungua mashtaka binafsi (private prosecution), sheria zetu ziko wazi," alisema Marmo na kuongeza;

"Taarifa kwa kweli sio ya siri kwa maana ya siri ya Serikali. Taarifa hii inaweza kujadiliwa mahali popote lakini ni taarifa ya uchunguzi ambao umefungwa na uchunguzi huu unahusu masuala ya jinai na kama kuna dosari zozote katika uchunguzi mwelekeo ni kwenye Mahakama na hata siku moja sio Bungeni."

Dk. Slaa aliendelea kuhoji kwa kusema baada ya taarifa ya TAKUKURU kutamka kuna uzembe na kuna mapungufu maelezo hayo yalielekezwa wapi ili sehemu ya Serikali inayohusika iweze kuchukua hatua za kinidhamu.

"Sasa Serikali ni vema ikatuambia kinapotokea kitu cha namna hii katika taarifa ya namna hiyo linaachwa linafungwa? Kama ikifungwa ni chombo gani kinachukua kutoka pale ili yale yaliyojitokeza pale ambayo sio ya kijinai yaweze kufanyiwa kazi au ndio tunaacha? Iwapo hivi ndivyo kwamba inaachwa je, dhamira ya Serikali ya kufuatilia uzembe, hata hii dhamira ya Mheshimiwa Rais ya kuita watendaji ili pale panapotokea uzembe hatua zichukuliwe, tunachukuaje hatua iwapo taarifa ya namna hiyo inafungwa haipelekwi kwenye chombo kinachohusika?" alihoji.

Marmo alisema sheria ya Kupambana na Rushwa, uzembe pia ni kosa la jinai lakini akamtaka Dk. Slaa kuwasilisha bungeni suala hilo kwa utaratibu wake iwapo anafikiri kuna uzembe kwa jinsi suala la Richmond lilivyoshughulikiwa.

Sekta ya madini nayo imekua ikipigiwa kelele na wabunge wa pande zote wakiwamo wa CCM hasa wanaotoka maeneo yenye migodi ya madini hususan katika Kanda ya Ziwa. Lakini wabunge hao waliunga mkono kusimamishwa kwa Mbunge wa Kigoma Kaskazini kupitia CHADEMA, Zitto Kabwe, kwa kumbana Waziri Karamagi kuhusiana na mkataba wa mgodi wa dhahabu wa Buzwagi uliosainiwa Uingereza.

Lakini baada ya yote hayo yaliyotokea, wiki iliyopita Rais Kikwete alimteua Zitto kuingia katika kamati ya kuchunguza sekta ya madini siku chache kabla ya kumaliza adhabu yake ya kufungiwa Bunge. Jambo hilo linaweza kuwa na maana kuwa Rais amekejeli kwa namna, uamuzi wa wabunge kutoa adhabu hiyo ambayo imekuwa ikiigharimu CCM na Serikali.

Kuundwa kwa kamati ya madini nako kumeibua maswali mengi hasa baada ya kufungiwa kwa Zitto na uamuzi wa Serikali kuwatuma mawaziri wake na wanasiasa wa CCM kwenda kuzima vuguvugu la wapinzani ambalo dhahiri limeshindwa kukidhi haja.

Lakini pamoja, pengine, na nia nzuri ya Rais Kikwete kuunda Kamati hiyo ya Madini iliyoongozwa na Jaji mstaafu, Mark Bomani, nayo tayari kuna maswali kadhaa hususan kuhusiana na wajumbe wake ambao baadhi wanatajwa kuwa na mgongano wa kimaslahi na wahusika wa sekta ya madini ama wanasiasa, huku upande wa upinzani ukilumbana kuhusu kuwapo kwao ndani ya kamati hiyo.

Wajumbe wanaodaiwa kuzua utata hasa ni pamoja na Zitto, ambaye ndani ya chama chake kuna wanaoona kuwa si vyema yeye kuwa mjumbe kwa vile kamati hiyo inaweza kutumika kuisafisha Serikali ya CCM.

Wajumbe wengine wanaoibua mjadala wa mgongano wa kimaslahi ni Peter Machunde kutoka Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) ambaye anatajwa kuwa na uhusiano wa karibu na wa muda mrefu wa ubia wa kibiashara na Waziri Karamagi.

Wengine wanaotajwa kuweza kuwa na mgongano wa kimaslahi ni mwakilishi wa kampuni ya PriceWater Coopers, David Tarimo, ambaye ingawa Raia Mwema haikufanikiwa kujua hicho kinachogomba hadi inakwenda mitamboni, yapo madai kwamba yeye au mwajiri wake, hufanya kazi za ushauri katika baadhi ya makampuni yenye kumiliki migodi nchini.

Wengine ndani ya kamati hiyo ni Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), John Cheyo, Mbunge wa Kyela (CCM), Dk. Harrison Mwakyembe, Mbunge wa Msalala (CCM), Ezekiel Maige, Mkurugenzi wa Madai na Sheria za Kimataifa, Maria Kejo, Mwanasheria wa Wizara ya Nishati na Madini, Salome Makange, Kamishna wa Sera, Wizara ya Fedha, Mugisha Kamugisha na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Makazi, Wizara yab Ardhi, Edward Kihundwa.

Lakini alipoulizwa na Raia Mwema kuhusu madai ya kuwepo mgongano wa maslahi, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Mark Bomani alikataa kuzungumzia kwa undani suala hilo mbali ya kueleza kwamba anaridhika nayo.

"Sina tatizo na kamati yangu na hivi sasa tunaandaa ratiba na orodha ya watu tutakaowahoji, na muda wowote tutaanza rasmi kazi hiyo", alisema Jaji Bomani.
 
Back
Top Bottom